Masomo ya Biblia Yanayopaswa Kutumika Kwa Nia Mbalimbali "Continentiam"
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa limechapisha Tamko linaonesha Masomo ya Biblia yanayopaswa kutumika katika Ibada ya Misa Takatifu “ad postulandam continentiam” kwa ajili ya nia mbalimbali. Kwa sasa Baraza linaendelea kutuma masomo haya kwenye Mabaraza ya Maaskofu sehemu mbalimbali za dunia. Ikumbukwe kwamba, maneno “ad postulandam continentiam” yaliyowekwa kwenye Misale ya Kiroma yanatumika kuonesha kwa ujumla wake kile ambacho mbatizwa anaitwa na kutumwa kutenda, kwani wale wote waliobatizwa katika Kristo Yesu wamemvaa Kristo. Rej. Gal 3:27. Lengo la masomo haya ya Biblia ni kuadhimisha mafumbo ya Kanisa kwa ukamilifu ili kuomba neema, kwa moyo safi, usiokuwa na tamaa ya kutawala, kumiliki, kushinda, kuchunguza tamaa za mtu kwa namna isiyozuilika, ili kutosheleza tamaa za mtu binafsi na mara nyingi kwa gharama ya watu dhaifu. Katika Misale ya Kiroma neno “Continentia” linatumika kama njia ya jumla kuonesha mambo yote ambayo kila mtu aliyebatizwa ameitwa kufanya ili kumvaa Kristo (Rej. Gal 3:27), kupambana na kila aina ya uovu, akijua kwamba mwili wake ni hekalu la Roho Mtakatifu, njia ya kumtukuza Mwenyezi Mungu (Rej. 1Kor 6:19), kufuata njia ya maisha, katika hatua na Roho Mtakatifu (taz. Gal 5:25), katika kushika Amri za Mungu. (taz. Sir 2:20, 21 na Ez 36:27), na sio njia ya kumkasirisha Mwenyezi Mungu kwa kushikamana na tamaa na kazi za mwili (Rej. Gal 5:19).
Waamini wanaalikwa kuwa ni nuru katika Kristo Yesu, ili wengine wapate kumtukuza Mwenyezi Mungu (Rej. Yn 15:12-17) kwa kuona ndani ya Mkristo maisha mazuri katika mambo yote, na hasa katika upendo, na kwamba hii si kazi ya kibinadamu pekee. Mwamini anahimizwa kuwa na kuishi kwa ajili ya Kristo Yesu; kwa kusulubisha mwili wake pamoja na maovu na tamaa yake (taz. Gal 5:24), bila kuudharau mwili wowote, ni lazima mwamini aombe na kupata neema ya kuishi kwa Roho Mtakatifu (Rej. Gal 5:24; 25), kwa kupokea moyo mpya na roho mpya (Rej. Ez 36:26), kwa kutoa miili yao kwa Mwenyezi Mungu katika kila tukio na katika kila hali ya maisha kama dhabihu iliyo hai, takatifu na inayokubalika mbele zake (taz. Warumi 12:1). "Kuna giza katika mioyo ya wanadamu," Baba Mtakatifu Francisko aliyasema hayo wakati wa salam zake za Noeli kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake maarufu kama “Urbi et Orbi”, tarehe 25 Desemba 2019, na akaongeza kusema "lakini nuru ya Kristo Yesu ni kubwa zaidi." Tamko linaonesha Masomo ya Biblia yanayopaswa kutumika katika Ibada ya Misa Takatifu “ad postulandam continentiam” kwa ajili ya nia mbalimbali. Haya ni masomo kutoka katika Agano la Kale, Agano Jipya, Zaburi na Kiitikizano pamoja na Injili.