Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 20 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na Rais Miguel Díaz-Canel Bermúdez wa Cuba. Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 20 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na Rais Miguel Díaz-Canel Bermúdez wa Cuba.  (AFP or licensors)

Rais Miguel Díaz-Canel Bermúdez wa Cuba Akutana na Papa Francisko Mjini Vatican

Baba Mtakatifu pamoja na Rais wa Cuba katika mazungumzo yao ya faragha, wamegusia kuhusu umuhimu wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Cuba katika kukoleza ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wamegusia pia hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II kuanzia tarehe 21 hadi 26 Januari 1998, kumbukizi ya miaka ishirini na mitano iliyopita. Wamezungumzia kuhusu mchango wa Kanisa katika huduma, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu Cuba!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 20 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na Rais Miguel Díaz-Canel Bermúdez wa Cuba, ambaye baadaye amebahatika pia kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, aliyekuwa ameambatana na Monsinyo Daniel Pacho, Katibu mkuu msaidizi wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Baba Mtakatifu pamoja na Rais wa Cuba katika mazungumzo yao ya faragha, wamegusia kuhusu umuhimu wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Cuba katika kukoleza ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wamegusia pia hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II kuanzia tarehe 21 hadi 26 Januari 1998, kumbukizi ya miaka ishirini na mitano iliyopita. Baadaye katika mazungumzo yao, wamejikita zaidi katika hali halisi ya maisha ya watu wa Mungu nchini Cuba sanjari na mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini humo na hasa zaidi katika huduma ya upendo. Baadaye wamegusia pia masuala ya Kimataifa na Kikanda na kwamba, kuna haja kwa Cuba kuendelea kujizatiti zaidi katika kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kumbukizi ya Miaka 25 ya Hija ya Kitume ya Mt. Yohane Paulo II
Kumbukizi ya Miaka 25 ya Hija ya Kitume ya Mt. Yohane Paulo II

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alisema, hija yake ya Kitume nchini Cuba kuanzia tarehe 21 hadi 26 Januari 1998 ilipania pamoja na mambo mengine: Kuwaimarisha na kuwatia shime watu wateule wa Mungu nchini Cuba katika imani, matumaini na mapendo pamoja na kushiriki katika maisha yao ya kiroho; katika mapambano, furaha na mateso, kusherehekea, kama washiriki wa familia kubwa ya Mungu fumbo la upendo wa kimungu na kuufanya uwepo zaidi katika maisha na historia ya wananchi wa Cuba wenye kiu ya Mungu na maadili ya kiroho. Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Cuba alikuwa ni hujaji wa upendo, ukweli na matumaini, akiwa na shauku ya kunogesha mchakato wa Uinjilishaji mpya kuhusu maisha na utume wa Kristo Yesu ulimwenguni na Mama Kanisa kuendelea kujikita katika huduma makini kwa binadamu. Ujumbe wa Injili anasema, Mtakatifu Yohane Paulo II unawaongoza watu wa Mungu katika upendo, sadaka, maisha ya kujitoa, dhabihu na msamaha, ili kama mahujaji wawe ni watu wenye matumaini kwa maisha yajayo. Jambo la msingi kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanamfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao, kuyapyaisha tena kadiri ya kweli za Kiinjili, ili waweze kumfuasa Kristo Yesu kwa uaminifu, wapate maana ya maisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Miaka 25 ya Hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Cuba
Miaka 25 ya Hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Cuba

Hii ni hija iliyomwezesha Mtakatifu Yohane Paulo II kukutana na kuzungumza na familia na vijana, ambao kimsingi wanapaswa kuwa ni wadau katika mageuzi ya maisha ya kiroho, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi yanayosimikwa katika upendo, ukweli na matumaini kwa watu wa Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni shuhuda wa kinabii, uliogusa undani wa watu wa Mungu, dhamiri nyofu, uhuru wa kuabudu; ujasiri wa kufikiri na kutenda mintarafu mwanga wa Injili. Hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II iligusia umuhimu wa Cuba kujifunua kwa Jumuiya ya Kimataifa na Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na Cuba kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, vikwazo vya kiuchumi, waathirika wakuu ni watu wa kawaida. Ni katika muktadha wa kumbukizi ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II afanye hija yake ya kitume nchini Cuba kuanzia tarehe 21 hadi 26 Januari 1998, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua ya kichungaji watu waaminifu wa Mungu, kuwashukuru, pamoja na kuwahimiza kuendeleza ujenzi wa matumaini unaojikita katika mizizi ya watu wa Cuba na ile ya Kikristo kwa kuwa wazi, wakarimu na watu wenye mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kwamba, barua hii ni kielelezo cha uwepo wake wa karibu na ushirika kwa watu wa Mungu nchini Cuba.

Papa Francisko amekutana na kuzungumza na Rais wa Cuba
Papa Francisko amekutana na kuzungumza na Rais wa Cuba

Katika kumbukizi ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipofanya hija yake ya kitume nchini Cuba, Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba, lilimwalika Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, kuhudhuria tukio hili adhimu ambalo limeacha alama za kudumu katika maisha ya watu waminifu wa Mungu nchini Cuba, ilikuwa ni fursa ya kutoa pia salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Cuba kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa matumaini kwa taifa lao kwa kujikita zaidi katika uvumilivu, haki na busara kwa kukabiliana na changamoto mamboleo kwa ari na moyo mkuu, kwa kuendelea kuzama zaidi katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na zile za watu wa Cuba, ili kujenga jamii bora zaidi inayosimikwa katika uhuru kwa kutambua kwamba, uhuru unakwenda sanjari na wajibu kwa jirani na katika historia ya watu wa Mungu nchini Cuba. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutumia fursa hii ya kumbukizi ya Miaka 25 ya Hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Cuba, kuwahimiza kujikita zaidi katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na zile za watu wa Cuba, ili kukuza na kuimarisha ushuhuda wa sadaka ya upendo na mshikamano kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Cuba, hususan maskini na wahitaji zaidi.

Kardinali Beniamino Stella alimwakilisha Papa katika maadhimisho haya.
Kardinali Beniamino Stella alimwakilisha Papa katika maadhimisho haya.

Hizi ni tunu msingi zinazotoa utambulisho wa watu wa Mungu nchini Cuba yaani: Ukweli na uwazi, Ukarimu na Mshimamano wa upendo. Hii ni changamoto ya kuendelea kufanya hija ya pamoja, katika shida na mahangaiko yao, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu pamoja na Bikira Maria, Mama yake, wako pamoja na watu waaminifu wa Mungu nchini Cuba. Baba Mtakatifu alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu na ushirika. Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda. “Yer. 17:7-8. Mwishoni mwa barua yake ya kichungaji kwa watu wa Mungu nchini Cuba, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wateule wa Mungu nchini Cuba kuendelea kujiaminisha mbele ya Mungu, huku wakijitahidi kuzamisha mizizi katika maisha yao kwa ujasiri na uwajibikaji ili waendelee kuzaa matunda katika imani, matumaini na mapendo.

Yohane Paulo II Cuba

 

21 June 2023, 15:00