Mhashamu Askofu Jean Pascal Andriantsoavina Jimbo Katoliki la Antsirabé,
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Askofu msaidizi Jean Pascal Andriantsoavina wa Jimbo Katoliki la Antananarivo kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Antsirabé, nchini Madagascar. Kabla ya uteuzi huu Askofu Jean Pascal Andriantsoavina alikuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Antananarivo nchini Madagascar. Itakumbukwa kwamba, Askofu Jean Pascal Andriantsoavina alizaliwa tarehe 24 Machi 1969 Mitsinjo, Jimbo Katoliki la Majunga, nchini Madagascar. Baada ya malezi na majiundo ya Kikasisi, tarehe 5 Agosti 2000 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Antananarivo. Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa Paroko-usu; Mlezi wa vijana Jimbo kuu la Antananarivo. Baadaye akapelekwa na Jimbo lake kujiendeleza kwa masomo ya juu kwenye Taasisi ya Sayansi ya Biblia, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian kilichoko mjini Roma ambako alifaulu kujipatia Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Maandiko Matakatifu.
Kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2011 akateuliwa kuwa ni Mwalimu wa Taaluma, Seminari kuu ya Falsafa huko Antsirabè. Kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2019 akateuliwa kuwa ni Gambera wa Seminari kuu ya Falsafa huko Antsirabè. Kuanzia Mwezi Machi 2019 alikuwa akishiriki shughuli mbalimbali za kichungaji Parokiani pamoja na kutafsiri Biblia kwenye lugha ya Kimalgasi. Tarehe 8 Julai 2019 akateuliwa na Papa Francisko kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Antananarivo, nchini Madagascar na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 11 Agosti 2019. Tarehe 10 Julai 2023 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa Askofu Jean Pascal Andriantsoavina kuwa ni Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Antsirabé, nchini Madagascar.