Askofu Msaidizi Joseph Mugenyi Sabiiti Ang'atuka Kutoka Madarakani: Fort Portal
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Joseph Mugenyi Sabiiti wa Jimbo Katoliki la Fort Portal, nchini Uganda la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Itakumbukwa kwamba, Askofu Mstaafu Joseph Mugenyi Sabiiti wa Jimbo Katoliki la Fort Portal alizaliwa tarehe 9 Mei 1948 huko Nyansozi, Uganda. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe Mosi Juni 1975 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Fort Portal, Uganda. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 2 Januari 1999 akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Fort Portal, Uganda na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 24 Aprili 1999.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Julai 2023 akaridhia ombi lake la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Kanisa linamshukuru na kumpongeza Askofu Mstaafu Joseph Mugenyi Sabiiti wa Jimbo Katoliki la Fort Portal, Uganda kwa kulitumikia Kanisa kama Padre kwa miaka 48, na kama Askofu akiwa na dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 24.