Daraja la Ushemasi kwa Frt Mligo:Aliyeitwa hachelewi kuitika wito!
Na Angella Rwezaula, - Vatican & DonBosco Mligo,Camaldoli.
Bwana Mungu anazidi kuita kila wakati watumishi wake wa karibu, kila saa na wakati anapotaka yeye mwenyewe kwa mapenzi yake tu ili shamba lake lipate watenda kazi wengi kwa maana ni wachache. Tunajua vema Ushemasi ni huduma ya Neno la Mungu, ya liturujia na ya matendo ya upendo na kama asemavyo Mtakatifu Paulo katika barua kwa (1Timoteo 3,13) kuwa Mashemasi wanaofanya kazi yao vyema wanajitengenezea nafasi nzuri ya kuheshimiwa. Nao kwa kiasi kikubwa sana wanajihakikishia imani yao katika Kristo Yesu. Yafuatayo ni mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican na Frt Donbosco Mligo wa Shirika la Wabenediktini Wakamaldoli huko Arezzo nchini Italia kabla ya kupewa Daraja la Ushemasi manmo tarehe 11 Julai 2023, katika Misa itakayoongozwa na Askofu Andrea Migliavacca wa Jimbo Katoliki la Arezzo na ambaye atatoa daraja la Ushemasi.
Kwa ufupi unaweza kujitambulisha wewe ni nani, ulizaliwa wapi, familia yako na wito wako?
Il kujua tulipo ni muhimu pia kujua tuliko toka na tunakokwenda. Hii ni kutokana na ukweli anaoelezwa kwamba: “Historia ni mwalimu wa maisha, jana ni historia, leo ni zawadi lakini kesho ni fumbo/ matumaini” (Na mwalimu Oogway. Ninaipenda sentesi hiyo katika kufungua historia yangu ya hapa duniani ambayo ilianza tarehe 04/10/1986 katika kijiji cha Luvuyo, parokia ya Matola Jimbo Katoliki la Njombe – Tanzania kwa wazazi wangu Yohanes Abraham Mligo & Osmunda francis Ngailo ambao iliwapendeza niitwe jina la Donbosco Mligo (Yohane Bosco Mligo yaani wakichukua jina la mtakatifu mkubwa sana mwanzilishi wa Wasalesiani). Nilizaliwa na kulelewa katika misingi ya Imani ya Kanisa Katoliki iliyoletwa na Wamissionari Wabenediktini, lakini pia Wakonsolata, Wafransiskani, Wasalesianni na wengineo.
Suala la utambuzi wa miito yetu kwa kawaida ni mgumu, je wito wako wa kumfuasa Kristo ulianza namna gani?
Baada ya Elimu ya msingi nilijikuta katika mielekeo minne ya maisha: kulitumikia Kanisa, kuwa mtumishi wa serikali, mtumishi wa kampuni binafsi(coca-cola) au kuendelea na shule (private/serikali). Katika mazingira hayo (…) binaafsi niliona umuhimu wa kutulia bila kuelekea upande wo wote kwanza. Hivyo nilibaki nyumbani kutafakari nikijifunza maarifa ya nyumbani pamoja na wazazi kwa muda wa miaka miwili. Kisha nikaendelea na masomo ya Katekesi kwa miaka mitatu huku nikitafuta shirika la kitawa ambalo ningeweza kujiunga baadae. Baada ya katekesi nikajiunga na seminari ya maandalizi (pri-form one) ya kibenediktini ya Nakagugu-Hanga. Nikaendelea na masomo katika seminari ya Mtakatifu Maria Mbalizi huko Mbeya na Mafinga, nikajiunga na shirika hili la wamonaki wabenediktini wakamaldolesi mnamo tarehe 21 Machi 2010 kama mkandidati, kunako 21 Machi 2011 nikawa mpostulanti na tarehe 21 Machi 2012, nikawa mnovisi katika jumuiya ya Mtakatifu Romualdo Mafinga huko Mufindi , Iringa nchini Tanzania. Mnamo mwaka 2012 – 2023 umeendelea mchakato wa malezi stahiki na masomo nikiwa nyumba Mama nchini Italia, lakini hata hivyo mnamo tarehe 3 Novemba 2013 nilifunga Nadhiri za kwanza na hatimaye mnamo tarehe 3 Mei 2021 zile nadhiri za daima katika Jumuiya yetu iliyoko Camaldoli nchini Italia. Sikuishia hapo bali kuanzia mwaka 2018 hadi sasa 2023 ninapozungumza nimekuwa nikiendelea na masomo ya falsafa na taalimungu katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Anselmo, jijini Roma.
Katika kuelekea siku yako ya kupewa daraja la ushemasi, ni hisia gani uliyo nayo hasa kufikia hatua hii ambayo itakupeleka moja kwa moja kwenye upadirisho kwa mapenzi ya Mungu?
Hisia kubwa kelekea la daraja la Ushemasi tarehe 11Julai 2023 ni shukrani kubwa kwa Mungu kwa kuwa na wazazi wema walioniandaa vema katika safari hii ndefu bila wao wenyewe kujua (…), lakini pia ninaishukuru Jumuiya yangu ya Wamonaki Wabenediktini Wakamaldolesi, waalimu, walezi, ndugu jamaa na marafiki kwa mapokezi, malezi, misaada pamoja na maandalizi mazuri kufikia hatua hii muhimu ambayo hatua kwa hatua baada ya Huduma ya Ushemasi ni matarajio ya kuelekea Darala la Upadre.
Tukiwa katika hitimisho la mahojiano yetu unataka kuwapa ujumbe gani wasomaji na wasikilizaji wa Habari za Radio Vatican kuhusiana na safari ya kiroho yenye milima mabonde na tambarare lakini yenye kuwa na furaha ya Injili?
Ujumbe wangu zaidi kwa wasomaji/wasikilizaji ni kwamba aliyeitwa hachelewi na kuitika wito ni kila siku na saa ya maisha yetu na hatua kwa hatua, maana Mungu huita kwa wakati na kwa njia aonayo Yeye kuwa inatufaa kadiri ya mazingira yetu, hali zetu na nyakati zetu. Kwa hiyo huuu ni mwaliko kwetu sote katika Kutambua, kutumia na kutunza njia ambazo Mungu anazitumia kutuita na kututuma katika shamba la utumishi wake, ili mpango wake wa wokovu kwa watu wote utimie.
Tarehe 11 Julai ni Siku kuu ya Mtakatifu Benedikto Msimamizi wa Bara la Ulaya
Ndugu msomaji wa makala hii tumashukuru Mungu kwa wito huo ambapo Jumanne tarehe 11 Julai 2023 Ndugu DonBosco Mligo atapewa daraja la Ushemasi, sanjari na siku kuu ya Mtakatifu Benedikito wa Norcia (Nursia) (480-547), aliyekuwa ni mmonaki wa Italia na ambaye aliandika kanuni za kitawa na zikaenea katika monasteri nyingi sana za Kanisa la Ulimwengu na pia la Kiorthodox. Anajulikana na kuheshimiwa tangu zamani kama abati mtakatifu ambaye alitangazwa na Mtakatifu Papa Paulo VI kuwa Msimamizi Mkuu wa Ulaya mnamo tarehe 24 Oktoba 1964. Inawezekanaje kusahuliwa na Neno “Ora et Labora” yaani “Kufanya kazi na Kusali”, mambo mawili ambayo yanapaswa kwenda pamoja katika maisha ya kila mtawa wa kike na kiume na zaidi hata kwa yule anayejiita mkristo. Kwa maana hiyo kwa ufupi maisha ya Mtakatifu Benedikto da Nursia, alikuwa ni ndugu pacha wa Mtakatifu Skolastika, alizaliwa tarehe 12 Septemba 480, katika familia tajiri ya Roma. Baba yake, Eutropius Anicius, alikuwa kapteni mkuu wa Warumi katika eneo la Nursia, wakati mama yake alikuwa Claudia Abondantia Reguardati, malkia mdogo wa kijiji hicho. Aliishi miaka ya utoto kijijini Nursia, akiathiriwa na wahamiaji kutoka Dola la Roma Mashariki ambao katika karne III walikimbia dhuluma wakashika maisha ya kiroho katika mapango waliyojichimbia mwambani kandokando ya kanisa dogo.
Mtakatifu Benedikto ni Pacha na Mtakatifu Scolastika
Mtakatifu Benedikito alipofikia umri wa miaka 12 hivi mapacha walitumwa Roma kwa masomo, lakini walichukizwa na anasa za jiji hilo, alivyosimulia Papa Gregori I katika kitabu cha pili cha Majadiliano. Hivyo akaacha masomo, nyumba na mali ili avae kanzu ya kimonaki akampendeze Mungu tu. Alipofikia miaka 17 alitawa kwenye bonde la mto Aniene karibu na Eufide (leo Affile), halafu alielekea Subiaco, alipokutana na mmonaki wa monasteri ya jirani ambayo abati yake Adeodatus alimvika kitawa akamuonyesha pango kwenye mlima Taleo. Huko aliishi miaka 3 kama mkaapweke hadi Pasaka ya mwaka 500. Halafu akakubali kuongoza wamonaki wengine karibu na Vicovaro, lakini, baada ya kunusurika kuuawa kwa sumu, akarudi Subiaco, alipobaki karibu miaka 30, akihubiri neno la Mungu na kupokea wanafunzi wengi zaidi na zaidi, hata akawa anaongoza monasteri 13, kila mojawapoi kiwa na wamonaki 12 na abati. Karibu na mwaka 529 baada ya upinzani mkali wa padri jirani aliyejaribu kumuua na kupotosha wafuasi wake, aliamua kuhama akaelekea Cassino ambapo, juu ya mlima alianzisha monasteri ya Montecassino juu ya mabaki ya mahekalu ya Wapagani.
Kauli mbiu ya shirika la Wabenediktini ni: "Ora et Labora" "kusali na kufanya kazi"
Na huko Montecassino Mtakatifu Benedikto alitunga kanuni yake mwaka 540 hivi kama nilivyokwisha eleza hapo juu. Akifaidika na zile zilizotangulia, hasa Kanunu ya Mafundisho iliyoandikwa na mmonaki asiyejulikana, lakini pia ya Mtakatifu Basili Mkuu, Mtakatifu Yohane Kasiano, Pakomi na Sesari, aliunganisha nidhamu na heshima kwa mtawa na vipawa vyake, ili kuunda shule ya utumishi wa Bwana, kwa maana hiyo kauli-mbiu ya shirika lake ni Ora et labora yaani kusali na kufanya kazi. Hadi kifo chake aliishi Montecassino, huku akitembelewa na waamini na watu wengi maarfu. Alifariki mnamo tarehe 21 Machi 547, siku arubaini hivi baada ya dada yake Skolastica ambaye alizikwa pamoja naye katika kaburi moja huko Montecasino.