Tafuta

Mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika UN,Askofu Mkuu Gabriele Caccia na Mohammed Al Hassan,wakati wa afla ya kutia saini huko New York. Mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika UN,Askofu Mkuu Gabriele Caccia na Mohammed Al Hassan,wakati wa afla ya kutia saini huko New York. 

Mons.Caccia:waliokimbia makazi yao waendelee kupata usaidizi wa kibinadamu

Vatican inaendelea kuhangaishwa sana na vita vya umwagaji damu nchini Ukraine na linakariri ombi lake kwamba silaha zinyamazishwe, likiwahimiza “wahusika wakuu wote wa maisha ya kimataifa na viongozi wa kisiasa wa mataifa kufanya kila linalowezekana ili kukomesha vita.Hayo yamesema na Askofu Mkuu Caccia kwenye hafla ya Mkutano wa 88 wa Baraza Kuu la UN.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Ofisi za Usalama wa Umoaj wa Mataifa, Askofu Mkuu Gabriele Caccia akiwa katika hafla ya Mkutano wa 88 wa Baraza Kuu, kuhusu hali katika maeneo yanayokaliwa kwa muda ya Ukraine alitoa hotuba yake tarehe 18 Julai 2023. Akianza hotuba hiyo alisema kuwa “Vatican  inaendelea kuhangaishwa sana na vita vya umwagaji damu nchini Ukraine na linakariri ombi lake kwamba silaha zinyamazishwe, ikiwahimiza “wahusika wakuu wote wa maisha ya kimataifa na viongozi wa kisiasa wa mataifa kufanya kila linalowezekana ili kukomesha vita. Siku chache zilizopita, Papa Francisko aliona jinsi vita vya sasa vya Ukraine, kama vita vyote, ni janga kubwa kwamba  "kwa watu na familia, kwa watoto na wazee, kwa watu waliolazimishwa kuondoka katika nchi yao, kwa miji na vijiji, na kwa  kazi ya uumbaji, kama tulivyoona kufuatia uharibifu wa bwawa la Nova Kakhovka.”

Askofu Mkuu Caccia aidha alisema kuwa “pamoja na kuyashukuru mataifa ambayo yamewahifadhi na kuwasaidia wakimbizi, Vatican inasihi kwamba waliokimbia makazi yao waendelee kupata usaidizi wa kibinadamu hadi waweze kurejea nyumbani kwa usalama, kwa hiari na kwa heshima. Kwa upande mwingine, Vatican inatoa wito kwamba hakuna juhudi zozote zinazoweza kuepukika katika kuandaa muungano wa haraka wa familia zote zilizotenganishwa na ghasia za sasa nchini Ukraine, kuhakikisha kwamba maslahi bora ya watoto walioathiriwa yanaheshimiwa.”

Katika kukabiliana na mateso hayo, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika UN alisisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa “lazima isikue ikijitoa katika vita bali ifanye kazi pamoja kwa ajili ya amani.” Aidha aliongeza kuwa “Katika suala hilo Papa Francisko amemkabidhi Kardinali Matteo Zuppi jukumu la kuongoza utume  unaolenga kusikiliza na kutambua ishara za kibinadamu ambazo zinaweza kuwa mwongozo kuelekea njia ya amani. Vatican pia  inatoa wito kwa pande zote kuunga mkono juhudi hizo za kibinadamu ili kupunguza baadhi ya mateso makubwa yanayosababishwa na vita hivi vya kuchukiza. Zaidi ya hayo, kuna hitaji la dharura, kama Baba Mtakatifu Francisko asemavyo, “kutumia njia zote za kidiplomasia, hata zile ambazo hazijatumika hadi sasa, kukomesha janga hili la kutisha. Vita vyenyewe ni kosa na la kutisha!” Vatican  kwa mara nyingine tena inatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, na kuanza mazungumzo kuelekea amani ya haki na ya kudumu”, alihitimisha.

Hotuna ya Askofu Mkuu G Caccia huko New York Marekani 18 Julai 2023
19 July 2023, 15:40