Tafuta

Kardinali Luis Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji amemteua Mheshimiwa Padre Alfred Stanslaus Kwene, Afisa mwandamizi, Tume ya Uinjilishaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kuwa ni Mkurugenzi mpya wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, PMS. Kardinali Luis Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji amemteua Mheshimiwa Padre Alfred Stanslaus Kwene, Afisa mwandamizi, Tume ya Uinjilishaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kuwa ni Mkurugenzi mpya wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, PMS. 

Padre Alfred Stanslaus Kwene Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari Tanzania

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu tarehe 2 Juni 2023 amemteua Mheshimiwa Padre Alfred Stanslaus Kwene, Afisa mwandamizi, Tume ya Uinjilishaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kuwa ni Mkurugenzi mpya wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, PMS, katika tamko Namba 2125/23 la tarehe 2 Juni 2023. Padre Kwenye anachukua nafasi ya Padre Jovitus Mwijage aliyemaliza muda wake wa huduma

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu tarehe 2 Juni 2023 amemteua Mheshimiwa Padre Alfred Stanslaus Kwene, Afisa mwandamizi, Tume ya Uinjilishaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kuwa ni Mkurugenzi mpya wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, PMS, katika tamko Namba 2125/23 la tarehe 2 Juni 2023. Padre Alfred Stanslaus Kwene anachukua nafasi ya Padre Jovitus Mwijage aliyehitimisha muda wake wa uongozi kama Mkurugenzi mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, PMS nchini Tanzania. Katika tamko lililotiwa mkwaju na Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., linampongeza kwa utume hu una kumwombea mafanikio katika majukumu haya mapya. Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, PMS., yapo manne ambayo ni: Shirika la Uenezaji wa Imani, Shirika la Mtakatifu Petro, Shirika la Utoto Mtakatifu na Shirika la Umoja wa Kimisionari. Shirika la Uenezaji wa Imani linawajibu wa kuendeleza Katekesi na kuwasaidia Makatekista katika kutekeleza dhamana na majukumu yao ndani ya Kanisa. Shirika la Mtakatifu Petro linashughulika katika kuleta na kukuza miito kwenye nchi za kimisionari sanjari na kuwategemeza watawa wanaochakarika usiku na mchana katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Na hatimaye ni Shirika la Utoto Mtakatifu linalosimamia malezi na ukuaji wa watoto kiimani, kimaadili na utu wema, kwa kukazia dhana ya umisionari kati ya watoto wadogo na Shirika la Umoja wa Kimisionari linaendeleza utume kwa wote.

Kardinali Lui Antonio Golkim Tagle, akiwa AMECEA, Tanzania
Kardinali Lui Antonio Golkim Tagle, akiwa AMECEA, Tanzania

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 3 Juni 2023 alikutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwa kukazia: Utume wa kimisionari, Karama ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, na Matarajio na ndoto za upyaisho wa huduma ya uinjilishaji kwa Kanisa zima. Baba Mtakatifu ameishukuru mihimili yote ya utume wa uinjilishaji ndani ya Kanisa mintarafu mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutambua kwamba, kila Mkristo amepokea karama za Roho Mtakatifu hivyo anatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa wale wote wanaoguswa na mafungamano na upendo wa Kristo Yesu, wanawiwa kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa huruma na upendo wa Kristo Yesu, unaobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu. Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa uinjilishaji anayeleta amani na utulivu kwenye ghasia na mchanganyiko wa mambo. Tarehe 16 Mei 2023, Mama Kanisa ameadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hii pia imekuwa ni Siku ya Kuwaombea Mapadre: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Mwenyezi Mungu amependa kukutana na binadamu wote kwa njia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini wote kuendelea kujiaminisha kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kusema “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako.”

Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kiini cha huruma na upendo wa Mungu
Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kiini cha huruma na upendo wa Mungu

Baba Mtakatifu anasema, Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kielelezo cha mpango wa Mungu katika ukombozi wa mwanadamu kwani kwa kumtoa Mwanaye wa pekee, ili kila mtu amwaminiye, asipotee, bali awe na uzima wa milele. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya upendo usiokuwa na kifani wa Baba wa milele, mwaliko kwa kushiriki furaha yake isiyokuwa na mwisho; anawasimamisha wale walioteleza na kuanguka, anawafufua kutoka kwa wafu. Na mapenzi ya Baba yake wa mbinguni ni haya ili kwamba wote aliopewa Yesu na Baba yake wasipotee, bali wafufuliwe siku ya mwisho. Kristo Yesu alionesha masikitiko makubwa kwa dhambi zilizotendwa na binadamu, lakini akaonesha huruma, upendo na msamaha kama kielelezo cha Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu, mwaliko kwa mihimili yote ya uinjilishaji kufuata mfano wa Baba mwenye huruma, kama kielelezo na kiini cha utume wa uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa, ili upendo wa Mungu uweze kuwafikia watu wote, bila mtu awaye yote kuachwa nyuma! Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa, kama ambavyo umeshuhudiwa na Mwenyeheri Pauline Marie Jaricot, Muasisi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, na ambaye alikuwa na Ibada ya pekee kabisa kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Papa Francisko akizungumza na wajumbe wa Mashirika ya Kimisionari
Papa Francisko akizungumza na wajumbe wa Mashirika ya Kimisionari

Baba Mtakatifu Francisko amekugusia pia Karama ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, kwa nyakati hizi na kwamba, yanapaswa kuwa ni nyenzo muhimu ya uinjilishaji na uwajibikaji wa kimisionari unaotekelezwa na kila mbatizwa pamoja na kuyaenzi Makanisa mapya mahalia, kwa kukuza na kuhamasisha roho ya kimisionari miongoni mwa watu wa Mungu. Kumbe, ni wajibu wao, kumwomba Roho Mtakatifu ili awawezeshe kuhamasisha, kuunda na kujenga ari na mwamko wa kimisionari, ili kila mbatizwa aweze kuwajibika barabara katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kutokana na watu kutopea kwa imani kuna haja tena ya uinjilishaji mpya na wongofu wa kichungaji. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, yasigeuzwe kuwa ni chombo cha kugawa fedha kwani matokeo yake ni mihimili ya uinjilishaji kugeuka na kuanza kumezwa na malimwengu pamoja na rushwa na ufisadi wa mali ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko ameonesha matarajio na ndoto za upyaisho wa huduma ya uinjilishaji kwa Kanisa zima. Upyaisho huu unajikita katika mchakato wa umoja na ushirikiano, ili kuwa ni chachu inayosaidia kunogesha ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa kwa kuunga mkono juhudi za matendo ya uinjilishaji: Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kujenga ushirika na udugu wa kimisionari unaotekelezwa kwa njia ya miundo ya Mabaraza ya Maaskofu na Majimbo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Itakumbukwa kwamba, waasisi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa alikuwa ni Askofu, Padre na Waamini wawili walei, mwaliko wa ushiriki mkamilifu wa watu wote wa Mungu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kimisionari. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wote wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwa huduma makini kwa watu wa Mungu, licha ya matatizo na magumu wanayokabiliana nayo katika maisha na utume wao, lakini wakisukumwa na moyo pamoja na ari ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, huku wakisindikizwa kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Padre Kwenye PMS Tanzania
11 July 2023, 15:21