Uhuru wa Kidini Ni Sehemu Muhimu Sana ya Haki Msingi za Binadamu Uheshimiwe
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na kuhuzunishwa sana na kitendo cha mtu mmoja tarehe 28 Juni 2023 kuchoma baadhi ya kurasa za Quran Tukufu kwenye mlango wa msikiti mkuu huko Stockholm nchini Sweden. Kamwe uhuru wa kidini usitumike vibaya kwa ajili ya kudhalilisha watu wengine ndani ya jamii, vitendo vya namna hii vinapaswa kukemewa na kulaaniwa na wapenda amani duniani kote. Kitendo hiki kinachoonesha chuki za kidini kimelaaniwa na kushutumiwa na nchi mbalimbali duniani. Hii ni sehemu ya mahojiano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Bwana Hamad Al-Kaabi, Mkurugenzi mkuu wa Gazeti la Al-Ittihad linalochapishwa kila siku kwenye Falme za Kiarabu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba, binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Rej. DH 2.
Vatican inalaani kwa nguvu zote unajisi, uharibifu au kutoheshimu vitu vya kidini, alama na maeneo ya ibada. Uchomaji wa hivi karibuni wa baadhi ya kurasa za Quran Tukufu, siku ya kwanza ya maadhimisho ya Sikukuu ya Waislam ya Eid al-Adha unatia wasiwasi kutokana na umuhimu wa siku hii tukufu kudhararuliwa. Baba Mtakatifu Francisko alisitikitishwa na kuhuzunishwa na kitendo hiki na kusema kwamba, “Kitabu chochote kinachochukuliwa kuwa kitakatifu na watu wake lazima kiheshimiwe kwa heshima kwa waamini wake, na uhuru wa kujieleza usitumike kamwe kama kisingizio cha kudharau wengine.” Kwa hivyo, kukufuru kwa makusudi imani za kidini, mila au vitu vitakatifu ni shambulio la utu wa waamini. Hiki ni kielelezo cha baadhi ya watu ndani ya jamii kukosa uvumilivu wa kidini, kwa kutumia vibaya zawadi ya thamani kubwa ya uhuru wa kidini, ili kuwachefua waamini wa dini nyingine. Vitendo vya namna hii, vinachochea chuki na uhasama; hali ya kutovumiliana na hatimaye, kuanza kujielekeza katika ubaguzi mkubwa katika jamii. Imani ya kweli inayopata chimbuko lake katika kweli za ndani, huwawezesha waamini kuvumilia makosa na hata kusamehe. Kwa hakika, waamini wana jukumu kubwa katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaodumisha utu wa binadamu; kulinda haki msingi za binadamu na kuendeleza mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, ulimwengu mamboleo unahitaji wajenzi wa amani na wala si watengenezaji wa silaha; kunahitajika wajenzi wa amani na wala si wachochezi wa migogoro; ulimwengu unawahitaji wazima moto na sio wachoma moto; ulimwengu unawahitaji watetezi wa upatanisho na wala si tu wanaotishia uharibifu na maafa. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulizingatia hasa: mema ya kiroho kwa kila mtu; ukweli na haki; Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kanisa linawajibu wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, linahimiza umuhimu wa kulinda dhamiri nyofu pamoja na wajibu wa kimaadili. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba: wanaendeleza Mafundisho ya Kanisa kuhusu haki msingi za binadamu zisizoondosheka na katika sheria za muundo wa jamii. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufunda dhamiri za watu, ili kutambua utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. DH.1.