Askofu mkuu Germano Penemote, Balozi wa Vatican Nchini Pakistan
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi tarehe 12 Agosti 2023 amemweka wakfu Monsinyo Germano Penemote kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Pakistan. Askofu mkuu Germano Penemote anakuwa ni Padre wa kwanza kutoka Angola kuteuliwa kuwa Balozi wa Vatican. Kardinali Parolin kwa mara ya kwanza anatembelea Angola na kwamba, amewapelekea salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa Ondjiva, Kunene nchini Angola, Kardinali Parolin katika mahubiri yake amekazia zaidi kuhusu: Ukuu wa Mungu kwa kumchagua, kumweka wakfu na kumtuma; furaha ya kuwekwa wakfu kama Askofu kwa ajili ya wokovu wa roho za watu, Balozi wa Vatican, Mjumbe wa Upendo, Upatanisho, Haki na Amani sanjari na umuhimu wa Balozi wa Vatican kwenye Makanisa mahalia. Kardinali Parolin amesema kwa mara ya kwanza anatembelea Angola, ili kushiriki furaha ya watu wa Mungu nchini Angola kwa kuwekwa wakfu Monsinyo Germano Penemote, na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye asili ya wito wake aliyemchagua, akamweka wakfu na kumtuma ili aweze kuwa ni chombo cha wokovu wa wanadamu, kumbe yeye kwa sasa ni chombo cha furaha kuu inayodhihirishwa katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa tayari kuzaa matunda katika matendo mema sanjari na kuvuta roho za watu kwa Kristo Yesu.
Kama Askofu anaitwa kushirikiana kwa karibu zaidi na Kristo Yesu kwa ajili ya wokovu wa roho za watu, kama Balozi anaitwa kuwa ni chombo cha upatanisho kati ya binadamu na Mwenyezi Mungu. Ameitwa na anatumwa kuwa ni ishara na chombo cha haki, amani na upatanisho. Anaalikwa kuchochea mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili kuimarisha amani, mshikamano na ustaarabu kwa kutambua kwamba, Mungu ni upendo! Kama Askofu mkuu na Balozi wa Vatican anatumwa kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu unaobubujika kwa namna ya pekee kutoka pale juu Msalabani. Anaitwa na kutumwa kuwa ni chombo cha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam nchini Pakistan ambao ni wengi kwa idadi, ili haki msingi za binadamu pamoja na uhuru wa kuabudu vinaheshimiwa. Kumbe, kama Balozi wa Vatican anaitwa na kutumwa kuwa ni mtetezi wa amani, huku akifundisha, akiongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kristo Yesu ni chimbuko la kazi ya uumbaji na ukombozi. Kama Balozi wa Vatican anakuwa ni Mwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hivyo anapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi na Maaskofu mahalia pamoja na watu wote wa Mungu katika ujumla wao.
Mabalozi wa Vatican wakumbuke daima kwamba, Baba Mtakatifu anawapenda na kuwathamini kwani anatambua fika dhamana na utume wa Mabalozi wa Vatican kwenye Makanisa mahalia. Kumbe, anapaswa kutekeleza dhamana na utume wake kwa unyenyekevu, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa; kuendeleza Mamlaka Fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” na hivyo kuwa ni chombo cha wokovu wa wanadamu. Kardinali Pietro Parolin amehitimisha mahubiri yake kwa kumweka, Askofu mkuu Germano Penemote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili hatimaye aweze kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Askofu mkuu ili utume na dhamana yake ipate ufanisi na hatimaye iweze kuzaa matunda mema! Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Germano Penemote alizaliwa tarehe 24 Oktoba 1969 mjini Ondobe nchini Angola. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 6 Desemba 1998 akapewa daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Ondijiva, lililoko nchini Angola. Askofu mkuu Germano Penemote alijiendeleza na hatimaye kufaulu kujipatia Shahada ya Uzamivu kwenye Sheria na Taratibu za Uendeshaji wa Kesi Mahakamani, “Utroque Iure.” Tarehe 1 Julai 2003 akaanza utume wa diplomasia ya Kanisa na kufanikiwa kutumwa nchini; Benin, Uruguay, Slovakia, Thailand, Hungaria, Perù na Romania. Tarehe 16 Juni 2023, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Pakistan.