Padre Daniel Pellizzon, Katibu Muhtasi wa Papa Francisko
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Daniel Pellizzon kuwa Katibu wake muhtasi na hivyo kuchukua nafasi ya Padre Gonzalo Aemilius aliyemaliza muda wake wa huduma kwa Baba Mtakatifu Francisko na atapangiwa majukumu mengine. Padre Daniel Pellizzon alizaliwa tarehe 24 Januari 1983 mjini Buenos Aires, nchini Argentina. Kati ya mwaka 2011 hadi mwaka 2012 alishirikiana kwa karibu sana na Baba Mtakatifu Francisko wakati huo akiwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires kupanga na kuratibu pango hifadhi binafsi la Nyaraka za Baba Mtakatifu Francisko. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 3 Novemba 2018 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.
Kama Shemasi wa mpito na baadaye kama Paroko-usu kwa muda wa miaka mitano, amekuwa akiwasindikiza mahujaji katika hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Mtakatifu Cayetan huko Liniers. Hadi kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu wake alikuwa ni Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bikira Maria, Mama wa Huruma. Hayo yamebainishwa na Askofu mkuu Jorge Ignacio García Cuerva wa Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina ambaye amefafanua kwamba, Padre Daniel Pellizzon mwanzoni mwa Mwezi Agosti, 2023 ameanza utume wake mpya mjini Vatican. Anawaalika watu wa Mungu Jimbo kuu la Buenos Aires kumsindikiza Padre Daniel Pellizzon katika utume wake mpya ndani ya Kanisa.