Parolin:Papa ana matarajio makubwa ya mkutano na vijana wa WYD
Massimiliano Menichetti
Vijana ambao wamewasili Lisbon wanamngojea Francisko kuadhimisha Siku ya 37 ya Vijana Duniani pamoja, ambayo ni ya kwanza baada ya janga la Uviko-19. Francisko anaondoka kuelekea Ureno akiwa na ufahamu kwamba “mikusanyiko kama hii ina nguvu kubwa ndani yake, hata nguvu ya kubadilisha maisha kwa wengine”. Hivyo ndivyo Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican anashirikisha vyombo vya habari vya Vatican juu ya mawazo ya Baba Mtakatifu atakayekutana, kusikiliza na kuzungumza na vijana waliotoka sehemu mbalimbali za dunia kwa ajili ya maadhimisho haya makubwa ya imani. Baba Mtakatifu atakuwa katika mji mkuu wa Ureno kuanzia tarehe 2 hadi 6 Agosti, itakuwa ni safari yake ya 42 ya kimataifa kwa sababu ya WYD. Katibu wa Vatican pia anawataka wale wote ambao hawawezi kushiriki kimwili katika Siku hii “kujisikia kushiriki na wahusika wakuu kikamilifu” na anaeleza kwamba kituo cha Fatima kilikusudiwa kuwa karibu na wagonjwa, wanaoteseka na kuombea amani.
1. Mwadhama, Francisko atakuwa pamoja na vijana wa WYD huko Lisbon, Ureno. Je, Papa anajiandaa vipi kwa mkutano huu?
Baba Mtakatifu ana matarajio mengi kwa Siku hii ya Vijana Duniani inayokuja huko Lisbon, na katika ujumbe kadhaa wa video tayari amewaalika vijana kuungana naye katika hija hii na kujiandaa na tukio hili la Kikanisa hasa katika sala na kuombea, Papa, kwa ajili ya vijana wote ambao tayari wameondoka kuelekea Lisbon katika siku hizi, wakiwa na imani, kwa kufahamu kwamba mikutano hii, mikusanyiko hii ina nguvu kubwa ndani yao wenyewe, hata nguvu ya kubadilisha, kwa wengine, maisha. Yeye mwenyewe hivi majuzi alisema “tunakua sana Siku kama hizi!”. Kwa hiyo Baba Mtakatifu anajiandaa kwa ajili ya Siku ya Vijana Duniani ijayo yenye mvuto wa matumaini makubwa na anawatia moyo vijana kuwa na mtazamo sawa kwa nyakati zote atakazoishi nao. Wiki chache zilizopita pia alipokea, tuseme, mfuko ambao mahujaji vijana huko Lisbon watapokea.
2. Siku za Vijana Duniani zilizaliwa kutokana na uvumbuzi wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Mkutano huu wa ulimwengu unamaanisha nini mnamo 2023?
Ningesema kwamba chaguo la Yohane Paulo II bila shaka lilikuwa ni chaguo la kinabii, angalizo la kinabii, ambaye alisema kwa usahihi kabisa kwamba Kanisa linataka kusindikizana vijana, linataka kuwasindikiza na kuwatangazia Injili ili kurahisisha kukutana kwao na Kristo; kwamba Kanisa lazima lijisikie kujitolea zaidi, katika kiwango cha ulimwengu, katika kupendelea vijana, kwa kupendelea mahangaiko na wasiwasi wao, matumaini yao na pia kuendana na matarajio yao, daima katika mtazamo huu wa kukutana na Kristo aliye Njia, Kweli na Uzima. Kwa hiyo, angalizo hili la kinabii linaonekana kwangu kudhihirika katika umuhimu wake wote hata katika siku zetu. Hata leo, angalizo hili la kinabii linahifadhi umuhimu wake wote kwa sababu linataka kuthibitisha kujitolea kwa Kanisa kwa vizazi vichanga. Ulimwengu wetu, ambao unapitia mabadiliko makubwa, ambao umejua uzoefu wa kutisha wa janga la Uviko na ambao unakabiliwa na migogoro mingi, leo, katika sayari nzima, ni muhimu zaidi kuliko hapo awali kwa vijana kukutana na uso wa Yesu Kristo, kwamba wajue Neno lake la wokovu na kuwa wanafunzi wake. Na hivyo, Siku ya Vijana Duniani bado inathibitisha kuwa chombo muhimu na tukio la uinjilishaji kwa ulimwengu wa vijana. Na pia kuna kipengele cha udugu wa ulimwengu wote, ukweli kwamba vijana hawa, kutoka nchi tofauti na kwa hiyo na tamaduni tofauti, lugha, maisha, wanaweza kukutana na kubadilishana uzoefu wao, kubadilishana zawadi zao. Hivyo hatuna budi kushukuru ikiwa uzoefu huu umeendelezwa kwa miaka 40 na ikiwa leo una nafasi kubwa ya kujikita kwa undani kwa maisha ya vijana.
3. Kanisa linaweza kujifunza nini kutoka kwa vijana leo?
Ninaamini kwamba Kanisa lina mbele yake changamoto kubwa ya uenezaji wa imani, usambazaji wa imani kwa ulimwengu kwa ujumla. Na ninaamini kwamba katika kazi hii ambayo Kanisa linayo, vijana wana jambo la kutuambia. Katika ulimwengu wa leo sio wachache ambao hawamjui Yesu Kristo au labda wamemkataa, kwa hiyo idadi ya wale ambao wamepoteza imani yao na kujifanya kana kwamba Mungu hayupo inaongezeka. Papa amezungumza mara kwa mara juu ya mapumziko haya ya uenezaji wa imani kati ya vizazi vya watu wa Mungu, akielezea kuwa ni kawaida kwao kuhisi karibu kukatishwa tamaa na Kanisa na kuacha kujitambulisha na mapokeo ya Kikatoliki. Idadi ya wazazi ambao hawabatizi watoto wao, wasiowafundisha kusali au wanaoenda katika jumuiya nyingine za imani inaongezeka (EG 70). Hapa, hali hii, ambayo tunapaswa kutambua na ambayo ni lazima kuzingatia, inaathiri kwa karibu kuwepo kwa vijana ambao hubeba ndani yao maswali, mashaka mengi na maswali mengi ambayo hawawezi kujibu. Kwa hiyo, kile ambacho vijana wanachoomba kwa Kanisa ni kwamba, Kanisa lifanye upya bidii yake ya kitume na bila woga, lichukue njia hiyo ya uwongofu wa kichungaji na kimisionari, unaotamaniwa sana na Baba Mtakatifu. Ni lazima kuwa wabunifu, ni muhimu kupata ujasiri na lugha sahihi ya kumwasilisha Yesu Kristo kwa vijana wa leo, katika upya wake wote, katika wakati wake wote, kwa namna ambayo hata vijana wa wakati huu, ambao wana usikivu, mitindo, njia za kufanya mambo tofauti na wenzao wa zamani, wanaweza kukutana nayo na kuishi uzoefu wa imani ya kina, na kutokana na uzoefu huu wa imani ya kina ndipo hutokea hamu ya kuwashirikisha wenzao wote. Kwa hiyo ni mwaliko wa kutokuwa watulivu ndani ya kuta zetu bali tuwe wamisionari wa kweli kwa vijana na kuwashirikisha zaidi katika safari hii ya imani.
4. Kuna migogoro mingi sana ambayo ulimwengu unapitia: vita, umaskini, kutojali, kuachwa, ubinafsi, kutokuwa na dini ... Je, vijana wanaweza kushinda changamoto hizi?
Ndiyo, na ninaamini kwamba dalili inatujia kwa usahihi katika Ujumbe ambao Baba Mtakatifu alihutubia vijana kwa ajili ya WYD, ambapo anawasilisha Maria ambaye, baada ya tangazo, anainuka haraka na kwenda (Lk 1:39) kwa binamu yake Elizabeth, kumsaidia katika mahitaji yake. Hapa, basi Mama Yetu anatuonesha, anaonyesha vijana zaidi ya yote, njia ya ukaribu na kukutana. Na ninaamini kwamba vijana, haswa wanapotembea njia hizi, njia hizi za ukaribu na kukutana, wana uwezo ndani yao wa kukabiliana na kusaidia kutatua na kushinda changamoto nyingi za jamii yetu. Ninajua, ninakumbuka shuhuda za vijana wengi ambao, kama vile Mama Yetu, hawakuogopa kuacha starehe zao ili kuwa karibu na wale walio na shida, hawajifungii wao wenyewe lakini wanachagua kuweka vipaji vyao, vipawa vyao, uwezo wao kwa matumizi mazuri, kile ambacho wamepokea kwa ajili ya wengine na kutafuta kupitia chaguzi, ambazo zinaweza kuonekana hata chaguo zenye mipaka, hata kama ni ndogo lakini kufanya mema kukua duniani. Hapa, naamini kuwa huu ndio mchango ambao vijana wanaweza kutoa katika changamoto kubwa za wakati wetu.
5. Hatua ya Fatima imeongezwa kwenye siku ya WYD. Je, ziara hii kwenye mahali patakatifu pa Maria inamaanisha nini?
Ni ziara muhimu ambapo Baba Mtakatifu atakutana na vijana wagonjwa na kusali pamoja nao Rozari Takatifu. Wakati muhimu. Nadhani Papa anataka kurudia ujumbe wa Mama Yetu kwa watoto watatu wachungaji, wakati alipotokea huko nyuma mnamo 1917. Yalikuwa maneno ya faraja, yalikuwa maneno ya matumaini katika ulimwengu wa vita, sio tofauti sana na hali halisi ya sisi tunayopitia leo. Na Mama Yetu aliwaalika wachungaji wadogo na kupitia kwao watu kusali na kukariri, hasa, Rozari Takatifu kwa ujasiri mkubwa ili kupata amani ulimwenguni. Hivyo Baba Mtakatifu Francisko, ambaye daima anabeba moyoni mwake janga la wale wanaohusika katika migogoro, kwa ziara hii ya Madhabahu ya Fatima wakati wa WYD, anatuomba tusife moyo na kudumu katika sala na katika sala maalum ya Rozari Takatifu.
6. WYD inaweza na lazima iwe muda wa kusikiliza. Je, unadhani nini kinaweza kutokea kutokana na mkutano huu?
Hapo ni neema ya Mungu itendayo kazi ndani ya mioyo ya wanadamu na katika mioyo ya vijana, lakini ningependa kusisitiza kwamba kuna nyakati tatu za kukutana ambazo zinaonekana kuwa muhimu sana kwangu. Ya kwanza ni kumsikiliza Bwana, wito wake. Wakati muhimu sana katika maana hii ni Mkesha, adhimisho la Mkesha Jumamosi jioni, ambapo pia kuna wakati wa kuabudu Ekaristi. Kukutana na Bwana aliyepo katika Ekaristi na kujiruhusu akutane naye katika Ekaristi kunamaanisha kuwa tayari kusikiliza Neno lake pia: kukutana kunatokea ambapo inaweza kweli kubadilisha maisha ya vijana wengi. Wakati wa pili wa kusikiliza ni ule wa kumsikiliza Papa. Tunajua ni kwa kiasi gani Papa ana uwezo wa kuwasiliana na kuwa sawa na vijana, ana uwezo wa kuzungumza nao, kuwapa maneno yanayoweza kutikisa wao, kuwatia moyo watoe kilicho bora zaidi. Hata kukutana na Mrithi wa Petro, kama shahidi na mwalimu wa imani, kunaweza kuwa hatua ya mabadiliko katika maisha ya vijana. Na wakati wa tatu ni ule wa kukutana na kuwasikiliza vijana wao kwa wao: kila Siku ya Vijana Ulimwenguni pia ni hafla ya kukutana, kama nilivyosema, vijana wanaokuja kutoka nchi zingine, kujua jinsi wenzao wanavyoishi utofauti wao na jinsi gani tunaweza kutajirishana.
7. Nini cha kusema kwa vijana wengi ambao hawatakuwa Lisbon, hata kama wanataka?
Ndiyo, tunajua kwamba wakati Siku ya Vijana Duniani inafanyika Lisbon pia kutakuwa na matukio ya ndani na itawezekana kufuatilia WYD kupitia mitandao ya kijamii. Wale ambao hawawezi , kwa sababu mbalimbali kwenda Lisbon wanapaswa, ninawaalika kuungana kiroho na Papa na wenzao walioko Ureno na kuishi, hata kama kutoka mbali, kuishi uzoefu huu kwa nguvu kwa kusali pamoja nao na kwa ajili yao, kwa wale walio Lisbon. Na kwa hiyo wao pia lazima wajisikie kuwa sehemu hai ya WYD hii! Nimalizie kwa kusema kwamba, kama Baba Mtakatifu alivyosema, Siku za Vijana Duniani si "fataki", yaani, nyakati za shauku, pengine za shauku kubwa ambazo hata hivyo zimejificha zenyewe: hazitoshi, ni lazima kuunganishwa katika maisha ya vijana ya kawaida. Kwa hiyo, kabla ya kila WYD lazima kuwe na kazi ya kichungaji ya majimbo na parokia zinazoitwa kuandaa mikusanyiko ya ulimwengu, ambayo lazima ifuatiliwe. Ninaamini kwamba kwa wakati huu vijana wote, hata wale ambao hawawezi kuwepo kimwili Lisbon, lazima wajisikie kushiriki na wahusika wakuu kikamilifu.