Vijana Katika Ulimwengu wa Kidigitali: Ushuhuda wa Imani, Matumaini na Mapendo
Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB., - Vatican.
Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni kuanzia tarehe 1 hadi 6 Agosti 2023, Jimbo kuu la Lisbon, Ureno, imenogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 3 Agosti 2023 katika hija yake ya Kitume nchini Ureno amegusia kuhusu: Matatizo, changamoto na matumaini ya vijana wa kizazi kipya. Amekazia umuhimu wa elimu na masomo ili kujenga ulimwengu ulio bora zaidi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican hususani wewe kijana unayetusikiliza, Baba Mtakatifu Francisko katika waraka wa kitume wa “Christus Vivit” yaani “Kristu anaishi” anatuambia kuwa: Mtandao na mitandao ya kijamii imeunda njia mpya ya kuwasiliana na kuunganisha. Mitandao hii ni “uwanja wa wazi ambapo vijana hutumia muda wao mwingi na kukutana kwa urahisi... Mitandao inatoa fursa ya ajabu ya mazungumzo, kukutana na kubadilishana kati ya watu, pamoja na kupata taarifa na maarifa. Zaidi ya hayo, ulimwengu wa kidigitali ni mojawapo ya ushirikiano wa kijamii na kisiasa na uraia hai, na unaweza kuwezesha usambazaji wa taarifa huru zinazotoa ulinzi madhubuti kwa walio hatarini zaidi na kutangaza ukiukaji wa haki zao. Katika nchi nyingi, mtandao na mitandao ya kijamii tayari inawakilisha jukwaa imara la kuwafikia na kuwashirikisha vijana, hasa katika mipango na shughuli za kichungaji”(ChrV 87).
Maneno haya ya Baba Matakatifu Francisko yanatuongoza katika kutafakari pamoja nanyi jinsi ya kushuhudia imani yetu ya kikristo na kuishi katika upendo hasa kwa Mungu na kwa jirani katika ulimwengu huu wa kidigitali. Nini umuhimu wa Mitandao ya kijamii leo na ni changamoto zipi ambazo tunakumbana nazo hasa sisi vijana. Kanisa linasema nini kuhusu mitandao ya kijamii na intaneti. Haya ni maswali ambayo tutafakari pamoja na kuona ni jinsi gani tunaweza kuyajibu. Tunatambua kuwa maendeleo ya teknolojia yamefanya kuwa na uwezekano wa aina mpya ya mwingiliano kwa mwanadamu na kurahisisha sana maisha yetu. Mitandao ya kijamii haswa ni mazingira ambayo watu hutangamana, kubadilishana uzoefu, na kukuza uhusiano tofauti na hapo awali. Mitandao ya kijamii leo hii ni sehemu muhimu kabisa ya utambulisho na njia ya maisha ya vijana. Mtandao una uwezo mkubwa wa kuwaunganisha vijana na watu wote katika umbali wa kijiografia kama hapo awali. Kubadilishana habari na maadili sasa kunawezekana zaidi. Upatikanaji wa zana za kujifunzia mtandaoni umefungua fursa za elimu kwa vijana katika maeneo ya mbali na umeleta maarifa ya ulimwengu.(rej. Sinodi ya Maaskofu, Hati ya Mwisho “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya wito” no. 4). Na vilevile pia imerahisisha utendaji kazi, huduma za kibiashara, matangazo, kununua na kuuza vitu mbalimbali kwenye duka la online; huduma mbalimbali za kijamii mfano kulipia bills, kununua umeme, malipo mbalimbali unaweza kufanya ukiwa nyumbani kwako na kila kitu kikaenda vizuri na muda mfupi. Haya yote ni matokeo ya ukuaji wa teknolojia.
Wakati huo huo, hata hivyo, jinsi mawasiliano yanavyozidi kuathiriwa na akili ya bandia (Artificial Intelligence), kunatokea haja ya kugundua tena kukutana kwa mwanadamu katika kiini chake. Kumbe kumekuwa pia na changamoto nyingi katika mtandao na mitandao ya kijamii, kama tunavyosoma katika ule waraka wa kitume wa “Christus Vivit” yaani “Kristu anaishi” kuwa: “Vyombo vya habari vya kidigitali vinaweza kuwaweka watu kwenye hatari ya uraibu, kutengwa na kupoteza hatua kwa hatua kuwasiliana na ukweli halisi, kuzuia maendeleo ya mahusiano ya kweli kati ya watu. Aina mpya za vurugu zinaenea kupitia mitandao ya kijamii, kwa mfano unyanyasaji wa mtandaoni. Mtandao pia ni njia ya kueneza ponografia na unyonyaji wa watu kwa madhumuni ya ngono au kupitia kamari”. (ChrV 88). Wakati maendeleo ya teknolojia leo yamerahisisha sana maisha yetu; kila mmoja hasa vijana tunaitwa kuwa na busara katika matumizi yake. Katika hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa kwa maprofesa na wanafunzi wa chuo cha Roma Tre mwaka 2017 alisema: ‘tunahitaji kujiuliza sisi wenyewe maswali kuhusu kile kilichopo kwenye mitandao kama ni kizuri na kinapelekea katika maadili yanayofaa kwa maono ya mwanadamu na ya ulimwengu, maono ya mtu katika vipimo vyake vyote, haswa yule anayepita vitu vyote (yaani Mungu)’. Tukifanya hivi tutakuwa na uwezo wa kupata fursa kubwa zaidi katika kukutana na kushikamana sisi sote kwa pamoja, ambayo pia ni zawadi kutoka kwa Mungu. Hivyo tunaalikwa kuwa makini na mitandao ya kijamii maana inaweza kutusaidia kukua au kinyume chake kutupotosha na kuishia kututenga na majirani zetu, kutoka kwa wale walio karibu nasi.
Vijana tunaalikwa kutambua athari zinazoweza kujitokeza katika matumizi mabaya ya vyombo vya mawasiliano na hasa katika mitandao ya kijamii, kwani tunaweza kujikuta tukiwa wahanga wa nyanyaso na mmong’onyoko wa maadili na utu wema. Tukumbuke kuwa uwezekano mkubwa zaidi wa mawasiliano uweze kutuletea uwezekano mkubwa wa kukutana na kuleta mshikamano kwa kila mtu, kuishi pamoja, kuchanganyikana na kukutana, kukumbatiana na kusaidiana. (rej. Evangelii gaudium 87). Ewe kijana ningependa kukuachia mambo matano muhimu yatakayokuongoza kuwa shuhuda wa kweli wa imani yako katika ulimwengu wetu wa leo wa kidigitali: Tafuta vyombo vya habari (kama vitabu, filamu, vipindi vya televisheni, muziki na akaunti za Youtube n.k,.) vile vinavyounga mkono maadili ya Kikatoliki: vinavyoendeleza wema kama vile upendo, huruma, uaminifu, heshima, na haki. Fahamu athari zinazotokana na mitandao ya kijamii, kumbuka mitandao hii inaweza kuunda imani, mitazamo na tabia zetu. Ni muhimu kuzingatia jumbe tunazopokea na jinsi zinavyoweza kutuathiri. Jiulize, "Je, vyombo vya habari hivi vinaendana na imani yangu ya Kikatoliki? Je, vinakuza wema na ukweli, au vinanipeleka mbali nazo?" Tumia mitandao ya kijamii kuimarisha imani yako: Kuna nyenzo nyingi zinazopatikana mtandaoni ambazo zinaweza kukusaidia kujifunza zaidi kuhusu Ukatoliki, kama vile tovuti, podcast na chaneli za YouTube. Tumia nyenzo hizi kuongeza uelewa wako wa imani yako na kuungana na Wakatoliki wengine. Fanya mazoezi ya udhibiti na kiasi: Ni rahisi kujihusisha na ulimwengu wa kidigitali na kutumia saa nyingi kutazama mitandao ya kijamii. Hata hivyo, ni muhimu kujizoeza kiasi na kutenga muda kwa ajili ya maombi, kutafakari, na shughuli nyinginezo zinazorutubisha nafsi yako. Kuwa na ushawishi chanya: Tumia akaunti zako za mitandao ya kijamii na uwepo mtandaoni ili kukuza maadili ya Kikatoliki na kuwa ushawishi chanya kwa wengine. Shiriki maudhui ya kuinua, shiriki katika mazungumzo ya heshima, na tumia jukwaa lako kueneza upendo na huruma.