Septemba 30 ni kusimikwa Makardinali wapya 21:Ishara ya umoja wa Kanisa
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Dominika tarehe 9 Julai 2023 Baba Mtakatifu Francisko aliwateua Makardinali wapya 21 kati yao Makardinali watatu kutoka bara la Afrika ambao ni Askofu mkuu mwandamizi Protase Rugambwa wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania, Askofu mkuu Stephen Ameyu Martin MULLA, Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini pamoja na Askofu mkuu Stephen Brislin wa Jimbo kuu la Cape Town, Afrika Kusini. Makardinali wapya hao watasimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Baraza la Makardinali utakaoadhimishwa Jumamosi tarehe 30 Septemba 2023 mjini Vatican. Katika muktadha huo hata Jumuiya ya Watanzania kama ilivyo kwa Jumuiya za Nchi mahali ambapo wanatoka Makardinali wapya, wanajiandaa vema kufanya sherehe kubwa kwa ajili ya kuwapongeza makardinali wapya.
Makardinali wapya wanaingizwa kwenye Jimbo Kuu la Roma
Kwa maana hiyo Makardinali wapya wataingizwa kwenye Jimbo kuu la Roma kama ishara ya kuonesha Mshikamano na Umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia yaliyoenea kila kona ya dunia. Ikumbukwe katika muktadha wa Tanzania Baba Mtakatifu Francisko alimteuwa Askofu mkuu Protase Rugambwa mnamo tarehe 13 Aprili 2023 kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania. Awali alikuwa ni Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, huduma aliyobobea kwa miaka mingi kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2008. Wakati huo huo Baba Mtakatifu Benedikto XVI, tarehe 18 Januari 2008 akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, na tarehe 26 Juni 2012 akateuliwa kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na wakati huo huo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu. Tarehe 9 Novemba 2017 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Baada ya kulitumikia Baraza kwa vipindi viwili na muda wake ulipogota ukomo, kadiri ya Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” tarehe 13 Aprili 2023, Baba Mtakatifu amemteuwa Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu wenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania.
Makardinali wengine kutoka mabara mengine
Makardinali wateule wengine ni Askofu mkuu Robert Francis PREVOST, O.S.A., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa; Askofu mkuu Claudio GUGEROTTI, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki; Askofu mkuu Víctor Manuel FERNÁNDEZ, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Askofu mkuu Emil Paul TSCHERRIG, Balozi, Askofu mkuu Christophe Louis Yves Georges PIERRE, Balozi, Askofu mkuu Pierbattista PIZZABALLA, Patriaki wa Madhehebu ya Kilatini mjini YerusalemuAskofu mkuu Ángel Sixto ROSSI, S.J., wa Jimbo kuu la Córdoba; Askofu mkuu Luis José RUEDA APARICIO, wa Jimbo kuu la Bogotá; Askofu mkuu Grzegorz RYŚ, wa Jimbo kuu la Łódź,; Askofu mkuu José COBO CANO, wa Jimbo kuu la Madrid,; Askofu mkuu Sebastian FRANCIS, wa Jimbo kuu la Penang; Askofu Stephen CHOW SAU-YAN, S.J., Askofu wa Hong Kong: Askofu François-Xavier BUSTILLO, O.F.M. Conv., wa Jimbo la Ajaccio, Askofu msaidizi Américo Manuel ALVES AGUIAR, wa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno pamoja na Padre Ángel FERNÁNDEZ ARTIME, s.d.b., Mkuu wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco. Askofu mkuu Agostino MARCHETTO, Balozi; Askofu mkuu mstaafu Diego Rafael PADRÓN SÁNCHEZ, wa Jimbo Cumaná; Padre Luis Pascual DRI, OFM Cap., Muungamishi wa Madhabahu ya Mama Yetu wa Pompei, Buenos Aires nchini Argentina.