Askofu Jovitus Francis Mwijage wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Mheshimiwa sana Padre Jovitus Francis Mwijage kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bukoba. Hadi kuteuliwa kwake, alikuwa ni Mkurugenzi mtendaji wa Umoja wa Mapadre Wazalendo Tanzania, UMAWATA, Mjumbe wa Baraza la Seminari kuu Tanzania na pia Mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Uchumi ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS. Askofu mteule Jovitus Francis Mwijage alizaliwa tarehe 2 Desemba 1966 Jimboni Bukoba baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, tarehe 20 Julai 1997 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo, akabahatika kutekeleza dhamana na utume wake kama Paroko-usu Parokia ya Mwemage na Mwalimu na Mlezi Seminari Ndogo ya Rubya, Jimbo Katoliki la Bukoba.
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2011 alitumwa na Jimbo Katoliki la Bukoba kwa ajili ya kujiendeleza kwa masomo ya juu na hivyo kujipatia shahada ya uzamivu kwenye historia ya Kanisa kunako mwaka 2011. Kati ya mwaka 2011-2012 alikuwa ni Jaalimu wa historia ya Kanisa, Seminari kuu ya Segerea. Tangu mwaka 2012 hadi mwaka 2023 aliteuliwa kuwa ni Mkurugenzi mtendaji wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, Tanzania. Na tangu mwaka 2012 hadi uteuzi wake, alikuwa ni Mkurugenzi mtendaji wa Umoja wa Mapadre Wazalendo Tanzania, UMAWATA na pia kuanzia mwaka 2020 ni Mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Uchumi ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS.