2023.10.09 Misa kwa washiriki wa Sinodi iliyoongozwa na Patriaki Béchara Boutros Raï katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. 2023.10.09 Misa kwa washiriki wa Sinodi iliyoongozwa na Patriaki Béchara Boutros Raï katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.  (Vatican Media)

Kard.Boutros Raï”:Katika Sinodi Kristo anajifanya kuwapo,kutenda na kubadilisha historia

Katika Ibada ya Misa iliyoongozwa na Kardinali Béchara Boutros Raï kwa washiriki wa Sinodi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro,tarehe 9 Oktoba 2023 amejikita na Injili ya Siku kwa mtazamo wa Instrumentum Laborius kuwa Hali ya dunia ya leo na hali za watu maskini na wanaoteswa yanaamsha ukweli wa huruma ya Kristo ambaye alituchagua.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kadinali Béchara Boutros Raï, O.M.M., Patriaki wa Antiokia ya Wamaroni ameongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa washiriki wa Sinodi ya Kisinodi inayoendelea mjini Vatican, Jumatatu tarehe 9 Oktoba 2023. Kwa kuongozwa Injili ya siku, Patriaki Boutros Rai amesema Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Baada ya mfululizo wa uponyaji - mtu aliyepooza, mwanamke aliye na ugonjwa wa kutokwa na damu, ufufuo wa binti wa mtu mashuhuri, uponyaji wa vipofu wawili na bubu - Yesu, akiona umati wa watu waliomfuata kutoka sehemu moja hadi nyingine, alihisi huruma na kuwaambia wanafunzi wake: “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Kwa hiyo salini kwa Bwana wa mavuno ili atume wafanyakazi katika mavuno yake.”

Changamoto za dunia hii

Kardinali Rai alisema kuwa: Nitahamasishwa na tafakari hii kutoka katika Instrumentum Laboris au Kitendea kazi ili kubaini mavuno na wafanyakazi. Mavuno ambayo yanatupatia changamoto katika mkutano wa sinodi yamebainishwa kama ifuatavyo. Kwa mfano, ujenzi wa amani ya haki ambapo vita vinasababisha kumwaga damu katika dunia yetu; kutunza nyumba yetu ya kawaida katika uso wa mabadiliko ya tabianchi; mapambano dhidi ya mfumo wa kiuchumi unaozalisha unyonyaji, ukosefu wa usawa na upotevu; usaidizi kwa wale wanaoteswa hadi kufia imani; uponyaji wa majeraha yanayosababishwa na unyanyasaji, ngono, kiuchumi, taasisi, mamlaka, dhamiri; kukuza hadhi na utu wa kawaida wa binadamu, unaotokana na ubatizo unaotufanya kuwa wana na binti wa Mungu; Kama hiyo haitoshi kuna kuimarisha kwa mahusiano ya kidugu na Makanisa na jumuiya nyingine za kikanisa; mazoezi ya utamaduni wa kukutana na mazungumzo na waamini wa dini nyingine; upendo wa upendeleo kwa maskini, waliotengwa, watu wenye ulemavu; uendelezaji wa uchungaji wa kutosha kwa watu waliopata talaka na walioolewa tena; watu walio katika ndoa za wake wengi; kuwaweka vijana katika kitovu cha mikakati ya kichungaji; kuongeza mchango wa wazee katika maisha ya jumuiya ya Kikristo na jamii.

Kristo ndiye kiini cha yote

Kwa hiyo ni kweli kwamba mavuno ni mengi! Kwa upande wa watenda kazi wa mavuno, kwa mujibu wa Instrumentum Laboris  yaani kitendea kazi ni wale waliotumwa na Kristo na kuongozwa na Roho Mtakatifu, mhusika mkuu wa utume uliokabidhiwa kwa Kanisa na kwa hiyo wa njia nzima ya sinodi.  Tunasoma katika Instrumentum Laboris kwamba katika mkutano wa Sinodi Kristo anajifanya kuwapo na kutenda, kubadilisha historia na matukio ya kila siku, anatoa Roho ambaye analiongoza Kanisa kupata mwafaka wa jinsi ya kutembea pamoja kuelekea Ufalme na kusaidia wanadamu kuendelea katika mwelekeo wa kitengo.

Bwana atufanye kuwa watenda kazi

Patriaki Rai aidha alisema kuwa: Watenda kazi wa mavuno ni maaskofu, mapadre, mashemasi, wanaume na wanawake waliowekwa wakfu, walei waliobatizwa na kwa hiyo  wote wanahitaji kufundishwa katika njia ya sinodi ya kuendelea. Inahusu mafunzo katika maisha ya ushirika, utume na ushiriki, na pia katika sinodi ya kiroho ambayo ni kiini cha kufanywa upya kwa Kanisa. Hali ya dunia ya leo  hii na hali za watu wakiwemo maskini, waliopotea, wanaoteswa, waliotupwa, waliokatishwa tamaa, wakimbizi, waathirika wasio na hatia wa vita, waliopotea, wasio na makao, waliojeruhiwa katika hadhi yao, yote hayo yanaamsha ukweli wa huruma ya Kristo ambaye alituchagua mmoja baada ya mwingine ili kutengeneza majeraha haya na kupigania ulimwengu uwe  bora, wa kuishi nyumba yetu ya pamoja kwa amani na utulivu. Kwa kuhitimisha amesema Tunaombe katika liturujia hii ya kimungu kwamba Bwana wetu atufanye kuwa watenda kazi wanaostahili katika mavuno yake. Amina. Tumsifu Yesu Kristo.

Mahubiri ya Kardinali Rai Oktoba 9 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kwa washiriki wa Sinodi
09 October 2023, 10:13