Kumbukumbu ya Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska, 5 Oktoba
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, Jumatatu tarehe 18 Mei 2020 alisema, Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake, alijitahidi kuwafunulia watu, huruma na upendo wa Mungu, kama Kristo Yesu alivyomfunulia Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska wa Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma. Tangu sasa, Mtakatifu Faustina Bikira, atakuwa anaadhimishwa katika Kumbukumbu ya Hiyari na Kanisa zima, kila mwaka ifikapo tarehe 5 Oktoba! Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa katika tamko lililotolewa tarehe 18 Mei 2020 lilitangaza kwamba kuanzia sasa waamini wataweza kuadhimisha Kumbukumbu ya Hiyari kwa Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska wa Ekaristi Takatifu, Bikira, baada ya jina lake kuingizwa kwenye Kalenda ya Kirumi. Huu ni wakati wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa sababu rehema zake hudumu vizazi hata vizazi kwa hao wanaomcha! Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificat” anatafakari kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya binadamu wote na kwamba, kazi hii inatoa mwangwi wake kwenye maisha ya kiroho yanayosimuliwa na Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska, Bikira, ambaye kwa njia ya zawadi kubwa kutoka mbinguni, alibahatika kukutana na Kristo Yesu, ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu Baba na akawa shuhuda na chombo cha kutangaza na kueneza Ibada ya Huruma ya Mungu.
Mtakatifu Faustina alizaliwa Głogowiec, karibu na mji wa Łódź, nchini Poland kunako mwaka 1905 na kufariki dunia huko Cracovia kunako mwaka 1938. Mtakatifu Faustina alibahatika kuishi katika Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma kwa muda mfupi. Alionesha moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa wito na zawadi mbali mbali za maisha ya kiroho, akajitahidi kuishi kwa uaminifu mkubwa kwa zawadi zote hizi. Katika Shajara ya moyo wake, Madhabahu ambayo aliyatumia kukutana na Kristo Yesu, mwenyewe anasimulia jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyomwezesha kwa ajili ya faida ya watu wengi zaidi. Kwa kumsikiliza Kristo Yesu ambaye ni Upendo na Huruma aliweza kutambua kwamba, hakuna dhambi yoyote ya binadamu ambayo ingeweza kushinda huruma ya Kristo inayobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu. Na tangu wakati huo, akawa ni muasisi wa Ibada ya Huruma ya Mungu ambayo leo hii imeenea sehemu mbali mbali za dunia. Alitangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu, wakati wa Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.
Tokea hapo, Jina la Mtakatifu Faustina likapata umaarufu wa ajabu kutoka sehemu mbalimbali za dunia mwitikio wa kutangaza na kushuhudia Ibada ya Huruma ya Mungu ambayo imeleta mageuzi makubwa katika maisha ya waamini. Ni kutokana na muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa kusikiliza maombi yaliyowasilishwa na watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia na baada ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu amana na utajiri wa maisha ya Mtakatifu Faustina, ameridhia na kutamka kwamba: Mtakatifu Maria Faustina (Helena) Kowalska, Bikira aingizwe kwenye Kalenda ya Kirumi na atakuwa anakumbukwa na waamini wote tarehe 5 Oktoba ya kila mwaka, kama Kumbukumbu ya Hiyari. Maagizo haya yanapaswa kuingizwa kwenye Kalenda na Vitabu vya Liturujia kwa ajili ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu na Sala ya Kanisa kwa kuzingatia maelelezo yaliyotolewa kwenye Tamko hili. Kumbe, nyaraka hizi zinapaswa kutafsiriwa, kuthibitishwa na hatimaye kupitishwa na Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa na mwishoni, kuchapishwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki.