Waraka wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu Kwa Watu wa Mungu
Na Askofu Flavian Matindi Kassala, - Vatican.
Mababa wa Sinodi katika Waraka wao kwa watu wa Mungu mara baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu wamejikita katika ushirika, Utamaduni wa ujenzi wa ukimya ili kusikilizana na kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja na ushirika; wongofu wa kichungaji na kimisionari, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu inayosimikwa katika huduma; Upendo wa Kanisa unabubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kanisa linahitaji ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watoto wake wote hasa wale wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; ni mwaliko wa kuwasikiliza waamini walei na familia na kuendelea kujikita katika utambuzi wake wa kisinodi; kwa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kuimarisha mahusiano na mafungamano. Hii ndiyo njia hasa ya Sinodi ambayo Mwenyezi Mungu anaitarajia kutoka kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Kristo Yesu ndiye tumaini la pekee kwa waja wake. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 29 Oktoba 2023 anahitimisha rasmi maadhimisho ya Awamu ya Kwanza ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu. Ufuatao ni Waraka wa Kikao cha XVI cha Kawaida cha Sinodi ya Maaskofu kwa watu wa Mungu.
Wapendwa Kaka na Dada zetu, Tunapoelekea kukamisha awamu hii ya kwanza ya Kikao cha 16 cha Sinodi ya Maaskofu, tunapenda kumshukuru Mungu pamoja nanyi kwa nyakati nzuri na zinazotajirisha tulizoshiriki. Tumekuwa na kipindi cha Baraka katika mshikamano wa dhati na ninyi nyote. Tunatiwa nguvu nanyi kwa njia ya Sala zenu, hali tukishiriki matarajio yenu, maswali yenu, na hata mashaka yenu. Kama Baba Mtakatifu Francisko alivyotuomba miaka miwili iliyopita tulipoanza kipindi kirefu cha kusikilizana na kutafakari kwa ndani, kikiwa wazi kwa watu wote wa Mungu, bila kumwacha yeyote nje, na kusafiri pamoja chini ya msaada wa Roho Mtakatifu, kama wafuasi wa kimisionari wanaomfuasa Yesu Kristo. Kwa awamu hii ya kwanza na ya muhimu kwa mchakato mzima, tumekutana Jijini Roma tangu tarehe 30 Septemba. Kwa namna nyingi awamu hii imekuwa na matukio yasiyotarajiwa. Kwa mara ya kwanza, kwa mwaliko wa Papa Francisko, akinamama na akinababa wamealikwa, kutokana na hadhi ya ubatizo wao, kukaa katika meza moja na kushiriki, si tu katika mijadala, bali pia katika kuupigia kura mwenendo mzima wa Kikao cha Sinodi ya Maaskofu. Tumesikiliza kwa makini na kwa pamoja, katika utofauti wa miito yetu, karama zetu na utume wetu, chini ya Neno la Mungu na uzoefu wa wenzetu. Tukitumia njia ya Mawasiliano katika Roho, tumeshirikishana kwa unyenyekevu utajiri na umaskini wa jamii zetu kutoka mabara yote, tukitafuta kuvumbua Roho Mtakatifu anataka kusema nini kwa Kanisa leo. Pia tumeonja umuhimu wa kudumisha mashirikishano kati ya utamaduni wa Kilatini na ule wa Ukristo wa Mashariki. Mijadala yetu imetajirishwa pia kwa kiasi kikubwa kwa ushiriki wa ndugu zetu waalikwa toka Makanisa mengine na jumuiya zingine za kikanisa.
Mikusanyiko wetu imefanyika vile vile katika mazingira ya mahangaiko ya kidunia, ambayo madonda na kashfa zake vimetugusa nyoyo zetu kwa uchungu mkubwa, vikitia uzito wa aina yake katika kazi yetu, ikizingatiwa kwamba baadhi yetu wanatoka katika nchi zilizokubwa na vita hivyo. Tumewaombea wahanga wa vurugu hizo, bila kuwasahau wale wote ambao mhangaiko ya maisha na pia unyama wa udanganyifu umewalazimisha kufuata njia hatari ya ukimbizi. Tumewahakikishia mshikamano na ushirikiano wetu akinamama na akinababa wote duniani wanaoshughulika na ujenzi wa haki na amani. Kwa mwaliko wa Baba Mtakatifu, tumefanikiwa kuwa na nafasi kubwa ya ukimya ili kujenga usikivu wa pamoja na hitaji la ushirika wa Kiroho kati yetu. Wakati wa ufunguzi wa mkesha wa kiekumene, tulionja jinsi kiu ya umoja inavyoongezeka katika ukimya wa tafakari juu ya Kristo msulubiwa. Kwa kweli, msalaba ndiyo kiti pekee che Yeye, ambaye baada ya kujitoa kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu, aliwakabidhi wafuasi wake kwa Baba Yake, ili “wawe wamoja” (Yn. 17:21). Katika muungano thabiti wa matumaini yaletwayo na Ufufuko wake, tuliikabidhi kwake nyumba yetu sote ambamo vilio vya dunia na vya maskini vinazidi kuwa muhimu sana: “Laudate Deum!” (“Msifuni Mungu”), kama Papa Francisko alivyotukumbusha mwanzoni mwa kazi yetu. Siku kwa siku, tulionja msukumo wa mwito kuelekea mazungumzano ya kichungaji na kimisionari. Kwani utume wa Kanisa ni utangazaji Injili bila kujitazama lenyewe, bali kwa kujiweka katika huduma ya upendo upeo ambao kwao Mungu aliupenda ulimwengu. (rej. Yohane 3:16). Wakati watu wasio na makazi waishio karibu na viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro wanaulizwa matarajio yao kwa Kanisa wakati wa Sinodi hii, walijibu “Upendo!”. Upendo huu unapaswa kubaki daima kama moyo uwakao wa Kanisa, upendo wa ki-Utatu na ki-Ekaristi, kama Papa alivyokumbusha tarehe 15 Oktoba, wakati kikao chetu kikiwa katikati, akitumia ujumbe wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu. Ni “kuaminiana” kulikotupatia usikivu na uhuru wa ndani tuliojichotea, bila kusita kwa uhuru na kwa unyenyekevu kuoneshe tunapoafikiana, tunapotofautiana, matamanio na maswali yetu.
Na sasa? Tunatumaini kuwa miezi iliyobaki kuelekea awamu ya pili mwezi Oktoba 2024 itaruhusu kila mmoja kushiriki kwa uhakika upana wa ushirika wa kimisionari ukiwakilishwa na neno “Sinodi”. Hili si suala la ki-ideolojia, bali uzoefu uliojikita katika mapokeo ya kitume. Kama Papa alivyotukumbusha mwanzoni mwa mchakato huu, “ushirika na umisionari una hatari ya kubaki bila uhalisia, isipokuwa tukiwekeza katika utendaji wa kikanisa unaodhihirisha uhalisia wa kisinodi (…) ukihimiza uhusika wa kweli wa kila mmoja na wa wote.” (Oktoba 9, 2021). Kuna changamoto mbalimbali na maswali mengi: muhtasari huu wa awamu ya kwanza unaelezea mahali tulipokubaliana, unadhihirisha maswali yaliyobaki wazi, na unaonesha jinsi kazi yetu itakavyoendelea. Kanisa linalazimika kumsikiliza kila mmoja katika mwendelezo wa tafakari yake, likianza na walio maskini zaidi. Hii inahitaji njia ya wongofu kwa sehemu yake, ambayo ndiyo njia pia ya sifa: “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.” (Luka 10:21)! Inamaanisha kuwasikiliza wale wote walionyimwa haki ya kuongea katika jamii au wale wanaojisikia wametengwa, hata na Kanisa; kuwasikiliza walio wahanga wa ubaguzi wa rangi katika hali mbalimbali – hasa hasa katika maneo fulani ya wenyeji ambao tamaduni zao zimedhulumiwa (zimeporwa). Zaidi ya yote, Kanisa la nyakati zetu linawajibika kuwasikiliza, katika kiroho ya mazungumzano, wale aliokuwa wahanga wa madhurumu yaliyofanywa na washiriki wa mwili wa Kanisa, na kukubali kimkakati kuhakikisha kuwa hili halirudiwi tena.
Kanisa pia lina wajibu wa kuwasikiliza walei, waume kwa wake, wote wakiwa wameitwa katika utakatifu kwa njia ya ubatizo: kwa ushuhuda wa makatekista, ambao katika sehemu nyingi ni watangazaji wa kwanza wa Injili; watoto katika upole na uchangamfu wao, vijana katika shauku yao, kwenye maswali na maombi yao; watu wazima kwa ndoto, busara na kumbukumbu zao. Kanisa linahitajika kusikiliza familia, katika mahitaji yao ya elimu, katika ushuhuda wao wa kikristo wanaoutoa kwa dunia ya leo. Linahitajika kukaribisha sauti za wale wanaohitaji kushirikishwa utume wa walei na kushiriki tafakari na mifumo ya utoaji maamuzi. Ili kusonga mbele katika tafakari ya kisinodi, Kanisa kwa namna ya pekee linahitaji kukusanya zaidi maneno na uzoefu wa watumishi wa daraja: mapadre, wasaidizi wa kwanza wa maaskofu, ambao huduma yao ya kisakramenti haikwepeki kwa ajili ya maisha ya mwili mzima; mashemasi, ambao, kupitia utume wao, wanaonesha huduma ya Kanisa zima kwa walio wanyonge zaidi. Kanisa linahitaji pia kukubali kusikiliza sauti za kinabii za Maisha ya wakfu, walinzi aminifu wa mwito wa Roho. Linahitajika pia kuwa angalifu kwa wote wale ambao hawashiriki Imani yake lakini wanatafuta ukweli, na ambao ndani mwao Roho, ambaye, “anagawa kwa kila mmoja uwezekano wa kuhusianishwa na fumbo hili la pasaka” (Gaudium et spes 22, 5), yumo pia na anatenda. “Dunia tunamoishi, na ambayo tunaalikwa kuipenda na kuitumikia, pamoja na pingamizi zake, inalidai Kanisa lidumishe ushirikiano katika nyanja zote za utume wake. Ni kwa uhakika kwamba njia hii ya kisinodi ndimo Mungu anamolitegemea Kanisa la milenia ya tatu” (Papa Francisko, Oktoba 17, 2015). Hatuna haja ya kuogopa kujibu mwito huu. Maria, Mama wa Kanisa, wa kwanza katika safari, anaisindikiza hija yetu. Katika furaha na katika uchungu, anatuonesha Mwanae na anatualika tumwamini. Na Yeye, Yesu, ni tumaini letu pekee!