Tafuta

2023.11.11 Kanisa Kuu la Mama Immaculate la Tyler Texas, Marekani. 2023.11.11 Kanisa Kuu la Mama Immaculate la Tyler Texas, Marekani. 

Askofu Strickland amesimamishwa uchungaji jimbo la Tyler

Uamuzi wa Papa umechapishwa baada ya kumalizika kwa ziara ya kitume katika Jimbo la Tyler iliyokabidhiwa kwa maaskofu wawili wa Marekani.

Vatican News

Baba Mtakatifu Francisko amemsimamisha katika huduma ya Kichungaji ya  Jimbo Katoli la Tyler nchini Marekani ,Askofu Joseph E. Strickland, mwenye umri wa miaka 65, na wakati huo huo  kumteua Askofu Joe Vásquez, wa Austin, kuwa msimamizi wa kitume wa Jimbo lililoachwa wazi. Uamuzi huo ulikuja baada ya ziara ya kitume iliyoamriwa na Papa mwezi Juni iliyopita katika jimbo la Tyler na kukabidhiwa kwa maaskofu wawili wa Marekani.

Ujumbe kutoka kwa Kadinali Di Nardo

Kadinali Daniel Nicholas Di Nardo, Askofu mkuu wa mji mkuu wa Galveston-Houston, alitoa barua yake ambapo alibainisha kuwa maaskofu waliofanya ziara hiyo, walikuwa ni Askofu Dennis Sullivan, wa Camden, na askofu mstaafu Gerald Kicanas, wa Tucson, ambao walifanya uchunguzi wa kina katika nyanja zote za utawala na uongozi wa Jimbo la Tyler pamoja na Askofu Joseph Strickland.

Baada ya miezi kadhaa uamuzi umetolewa

Kwa mujibu wa ripoti hiyo inaendelea kusomeka kuwa, “Kutokana na ziara hiyo pendekezo lilitolewa kwa Baba Mtakatifu kwamba kuendelea kwa huduma ya Askofu Strickland hakungewezekana. Baada ya miezi kadhaa ya kutafakari kwa kina na Baraza la Kipapa la Maaskofu na Baba Mtakatifu, uamuzi ulifikiwa wa kuomba Askofu Strickland ajiuzulu. Baada ya kupokea ombi hilo, Askofu Strickland alikataa kujiuzulu wadhifa wake mnamo tarehe 9 Novemba, 2023.” Kwa hiyo ilikuwa ni uamuzi wa Papa wa kumwondolea majukumu yake. "Wakati tukingojea masharti maalum  zaidi kwa jimbo la Tyler, Baba Mtakatifu amemteua Askofu  Joe Vásquez wa Jimbo la  Austin, kama msimamizi wa kitume wa Jimbo la Tyler. Kardinali DiNardo anahitimisha kwa barua yake na kusema kuwa, “Tunamkumbuka Askofu Strickland katika sala zetu - na pia tunawaombea mapadre i na waamini wa jimbo la Tyler na Askofu Vásquez".

Askofu wa Tyler amesimamishwa shughuli za uchungaji
11 November 2023, 16:45