Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, kuanzia tarehe 11 Novemba hadi 12 Novemba 2023 linaadhimisha Siku ya 73 ya Shukrani Kitaifa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, kuanzia tarehe 11 Novemba hadi 12 Novemba 2023 linaadhimisha Siku ya 73 ya Shukrani Kitaifa   (©Deyan Georgiev - stock.adobe.com)

Maadhimisho ya Siku ya 73 ya Shukrani Nchini Italia: Kilimo

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, kuanzia tarehe 11 Novemba hadi 12 Novemba 2023 linaadhimisha Siku ya 73 ya Shukrani Kitaifa kwa kunogeshwa na kauli mbiu "Mtindo wa Ushirika kwa Maendeleo ya Kilimo.” Mafundisho ya Maandiko Matakatifu yanapendekeza kanuni ya udugu wa kibinadamu kama dhana yenye uwezo wa kuangazia medani mbalimbali ya shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na sekta ya kilimo, mamlaka ya kulima na kutunza ardhi (Rej. Mwa 2:15).

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 12 Novemba 2023 mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana alisema, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, kuanzia tarehe 11 Novemba hadi 12 Novemba 2023 linaadhimisha Siku ya 73 ya Shukrani Kitaifa kwa kunogeshwa na kauli mbiu "Mtindo wa Ushirika kwa Maendeleo ya Kilimo.” Mafundisho ya Maandiko Matakatifu yanapendekeza kanuni ya udugu wa kibinadamu kama dhana yenye uwezo wa kuangazia medani mbalimbali ya shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na sekta ya kilimo, mamlaka ya kulima na kutunza ardhi (Rej. Mwa 2:15) inamhusisha binadamu katika ngazi ya mtu binafsi, familia na katika mifumo mbalimbali ya ushiriano. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” anaweka mbele ya watu wa Mungu Injili ya Msamaria Mwema ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaothamini tofauti msingi zilizopo na kwamba, huu ni mwongozo makini katika kushinda uadui na hivyo kukuza na kuendeleza tabia ya kutunzana na kushirikiana kama alivyofanya Mtume Paulo kwa kushirikiana na Akila pamoja na mkewe Prisila, wakakaa na kufanya kazi kwa pamoja kwa maana walikuwa ni mafundi wa kushona mahema. Rej Mdo 18:1-4.

Siku ya 73 ya Shukrani Kitaifa nchini Italia, Kilimo!
Siku ya 73 ya Shukrani Kitaifa nchini Italia, Kilimo!

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanasema, “Wale wote wanaothubutu kuwekeza katika biashara waelewe kwamba, jamii wanamofanyia biashara huwakilisha lililo jema kwa kila mmoja na si tu muundo unaoruhusu kufikia matakwa ya mtu binafsi. Utambuzi huu peke yake huwezesha kujenga uchumi wenye mtazamo kweli wa kuhudumia jamii na kuandaa programu za ushirika wa kweli baina ya wadau mbalimbali katika uzalishaji. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakazia pamoja na mambo mengine mchango unaotolewa na shughuli za aina hii katika kuongeza thamani ya kazi, kukuza hisia ya uwajibikaji kwa mtu binafsi na kwa jamii, maisha ya kidemokrasia na tunu msingi za utu wa binadamu ambazo ni muhimu katika maendeleo ya soko na ya jamii. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linakiri kwamba, kilimo cha kifamilia mara baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kilichangia sana kukuza ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kujikita katika ushirika uliokuza sekta ya kilimo nchini Italia. Katika muktadha huu, Kanisa pia lilichangia sana katika mchakato wa kukuza sekta ya kilimo nchini Italia, licha ya changamoto na matatizo yaliyojitokeza kwa baadhi ya watu kuelemewa na ubinafsi wao na hivyo kushindwa kutambua haki msingi za washirika wao na matokeo yake, wakatumia fursa hii kuwanyonya na kuwadhulumu. Lakini sekta ya kilimo cha ushirika ikipewa kipaumbele cha kwanza inaunda fursa za kukutana, kushirikiana, na kukuza uwezo wa washiriki na hivyo kuweza kufikia malengo ya kiuchumi, kijamii na kimaadili yanayotafutwa kwa pamoja ili kuwajengea watu wa Mungu matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Kilimo cha kifamilia kina mchango mkubwa katika uchumi
Kilimo cha kifamilia kina mchango mkubwa katika uchumi

Kanuni ya udugu wa kibinadamu ni muhimu sana katika shughuli za kilimo ili kuweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga asilia kwa umoja na mshikamano wa pamoja. Kumbe, Siku ya 73 ya Shukrani Kitaifa ni fursa ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya udugu wa kibinadamu unaowasaidia watu wa Mungu kushirikishana kazi na hivyo kukuza na kudumisha moyo wa ushirikiano na mshikamano na hivyo kutoa motisha kwa vijana wa kizazi kipya kupenda kuishi vijijini. Katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, watu wa Mungu nchini Italia wanahimizwa kufanya mang’amuzi ya pamoja ya jinsi ya kushirikiana na kushikamana, ili kugundua tena ile thamani ya ushirika, tayari kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kulinda na kutunza vyanzo vya maji, ardhi pamoja na nishati. Huu ni mwaliko wa kushirikiana pia zana za kilimo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili wote kwa pamoja waweze kuokolewa, hii ni amana na utajiri wa kudumu unaowafanya watu wa Mungu kujisikia kwamba, wanawajibika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote bila kusahau ulinzi na usalama wa jirani zao.

Siku ya 73 ya Shukrani
12 November 2023, 11:08