Tafuta

Tarehe 19 Novemba 2023, familia ya watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Tanzania wakaungana ili kumwimbia Mungu wimbo wa pongezi kwa Askofu mkuu mstaafu Ruzoka Tarehe 19 Novemba 2023, familia ya watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Tanzania wakaungana ili kumwimbia Mungu wimbo wa pongezi kwa Askofu mkuu mstaafu Ruzoka 

Shukrani kwa Kwa Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka, Karibu Tabora Hakuna Mkwara!

Ilipogota tarehe 19 Novemba 2023, familia ya watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Tanzania wakaungana ili kumwimbia Mungu wimbo wa pongezi kwa Askofu mkuu mstaafu Ruzoka na shukrani kwa Mungu kwa matendo makuu aliyomkirimia katika maisha na utume wake kama Padre na Askofu. Jambo kubwa na la msingi ni kumpata, kumwona na hatimaye kumkabidhi Jimbo Kardinali Protase Rugambwa ambaye sasa ndiye Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora.

Na Henry Kilasila, Tabora na PadreRichard A, Mjigwa, C.PP.S. -Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Aprili 2023 alimteuwa Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, nchini Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Askofu Mkuu Rugambwa alizaliwa tarehe 31 Mei 1960 huko Bunena-Bukoba nchini Tanzania, akapata Daraja Takatifu ya Upadri kutoka mikononi mwa Mtakatifu Yohane wa Pili alipotembelea Tanzania tarehe 2 Septemba 1990 na kuwa Padri wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara. Kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alifanya utume wake kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu mjini Vatican. Baba Mtakatifu Benedikto XVI, tarehe 18 Januari 2008 akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, na tarehe 26 Juni 2012 akateuliwa kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na wakati huo huo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu. Tarehe 9 Novemba 2017 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Baada ya kulitumikia Baraza kwa vipindi viwili na muda wake ulipogota ukomo, kadiri ya Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” tarehe 13 Aprili 2023, Baba Mtakatifu akamteuwa Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu wenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania. Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 9 Julai 2023 aliwateuwa Makardinali wapya 21 kati yao Makardinali watatu ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao. Makardinali wapya wamesimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali tarehe 30 Septemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kardinali Tagle amempongeza Kardinali Rugambwa kwa ni lulu ya pekee
Kardinali Tagle amempongeza Kardinali Rugambwa kwa ni lulu ya pekee

Na tarehe 4 Oktoba 2023 Makardinali wapya wakashiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu: “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Makardinali kimsingi ndio walinzi wa imani na washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukoleza juhudi za toba, haki, amani na maridhiano; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora zaidi. Askofu mkuu Protase Rugambwa alikuwa ni kati ya Makardinali wale ishirini na moja walioteuliwa na kusimikwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 30 Septemba 2023. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Novemba 2023 akaridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu mkuu Paulo Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania na kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Baba Mtakatifu akamteuwa Kardinali Protase Rugambwa, kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora. Askofu mkuu mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka katika mahojiano maalum na Radio Vatican alipenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyemkirimia afya na imani na sasa anang’atuka kutoka madarakani. Analishukuru Taifa la Mungu nchini Tanzania tangu mwanzo alipoteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kigoma na hatimaye, kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora. Anamshukuru Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Benedikto XVI na sasa Papa Francisko waliombidiisha katika dhamana ya uongozi bhila kuwasahau watu wa Mungu na wote wenye mapenzi mema hadi wakati huu anapokabidhi “kijiti” kwa Kardinali Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora.

Watu wa Mungu wanamshukuru Mungu kwa zawadi ya Askofu mkuu Ruzoka
Watu wa Mungu wanamshukuru Mungu kwa zawadi ya Askofu mkuu Ruzoka

Ilipogota tarehe 19 Novemba 2023, familia ya watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Tanzania wakaungana ili kumwimbia Mungu wimbo wa pongezi kwa Askofu mkuu mstaafu Ruzoka na shukrani kwa Mungu kwa matendo makuu aliyomkirimia katika maisha na utume wake kama Padre na Askofu. Jambo kubwa na la msingi ni kumpata, kumwona na hatimaye kumkabidhi Jimbo Kardinali Protase Rugambwa ambaye sasa ndiye Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora. Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam katika mahubiri yake amekiri kwamba, ni Maaskofu wachache waliobahatika kuishi na watangaluzi wao na kwamba, Askofu mkuu mstaafu Ruzoka, alibahatika kupewa talanta tano ambazo amezitumia: kufundishia, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu amemkirimia kila mtu talanta kadiri ya uwezo wake na kwamba, kila mtu ana uwezo wa kuzalisha faida bila ya kuona wivu wala husuda kwa kile kiwango alichopewa na Mungu. Askofu mkuu mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka amebahatika katika maisha na utume wake kama Padre na Askofu kutumia vyema talanta zake tano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, Askofu mkuu mstaafu Ruzoka, ataendelea kuchakarika kumsindikiza Kardinali Protase Rugambwa katika utume wake mpya bila kinyongo, wala kwa kushinikiza, kwani akifanya hivi, “atakufa mapema kwa msongo wa mawazo.” Ni dhamana na wajibu wake kama Askofu mkuu mstaafu: kujadiliana, kuelekeza na kumwachia uhuru wa kutekeleza kadiri ya vipaumbele vyake.

Kardinali Pengo amempongeza na kumshukuru Askofu mkuu Mstaafu Ruzoka
Kardinali Pengo amempongeza na kumshukuru Askofu mkuu Mstaafu Ruzoka

Kwa upande wake Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu amewaambia watu wa Mungu nchini Tanzania kwamba, hii ni siku njema na yenye furaha kwani alikuwa amewapelekea salam na baraka za kitume kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko sanjari na salam na matashi mema kutoka katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Kardinali Tagle anamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha, utume na uhai wa Jimbo kuu la Tabora na hasa kwa huduma iliyotukuka kutoka kwa Askofu mkuu mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka. Kardinali Tagle amewahakikishia watu wa Mungu Jimbo kuu la Tabora kwamba, Kardinali Protase Rugambwa ni zawadi, baraka na kito cha thamani kubwa, wamtumie kwa busara kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu na kwamba, ataliendeleza Kanisa la Jimbo kuu la Tabora kwa kujenga juu ya msingi wa watangulizi wake daima akijielekeza katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari kwa kukazia umoja, ushiriki na utume katika huduma kwani kila mtu amekirimiwa talanta kwa ajili ya ujenzi na ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Tabora na Tanzania katika ujumla wake.

Watu wa Mungu wanamshukuru Mungu kwa zawadi ya Kardinali Protase
Watu wa Mungu wanamshukuru Mungu kwa zawadi ya Kardinali Protase

Naye Askofu mkuu mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka katika salam zake amekazia ujenzi wa Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume. Ametoa shukrani zake za dhati kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu pamoja na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki walioshiriki katika malezi na makuzi na hivyo kumfunda na kumfanya jinsi alivyo na hatimaye, akabahatika kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 20 Julai 1975, Mdo 10:34 na hata katika mazingira ya wakati wake, kwa hakika Mungu hana ubaguzi. 1989 alipoteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo la Kigoma, akajiaminisha mbele ya Mungu. Na Baba Mtakatifu Benedikto XVI alipomteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, akamwambia Mungu “Nitalitii Neno lako.” Akaamua kuubeba Msalaba wake na kumfuasa Kristo Yesu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Askofu mkuu mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka ametumia fursa hii kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume wake hata pale alipolazimika kufanya maamuzi magumu na kwamba, daima wawe tayari kuanza upya chini ya Kristo Yesu. Anamshukuru Mungu kwa neema, baraka na zawadi ya Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, tangu sasa atakuwa mtii na Padre wake mwaminifu. Tarehe 18 Novemba 2023, Askofu Msaidizi Methodius Kilaini aliongoza Masifu ya Jioni kwenye Kituo cha Hija cha Ifucha Nghoro kilichoko Jimbo kuu la Tabora.

Baadhi ya Maaskofu walioshiriki katika kumpongeza Askofu mkuu Ruzoka.
Baadhi ya Maaskofu walioshiriki katika kumpongeza Askofu mkuu Ruzoka.

Askofu Kilaini amesema, lengo la masifu haya ni kumshukuru Mungu kwa zawadi na utume wa Askofu mkuu mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka kwa maisha na utume wake kuanzia akiwa Padre hadi anapostahafu kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora. Imekuwa ni siku ya kutafakari makuu ya Mungu, utajiri, hekima, huruma, neema na baraka na kwamba, yote yamefanyika kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu Mwenyezi anayewalinda na kuwatunza waja wake, kwani Yeye ni Alfa na Omega; Mwanzo na Mwisho ni vyema na haki kujiweka mikononi mwake, kwani miaka 75 si haba! Bila ya kukata wala kujikatia tamaa, bali kukoleza umoja, upendo na mshikamano na hasa ile nguvu ya kukaa pamoja ili kuwaongoza watu wa Mungu. Mungu ni mwema na ameweza kuunganisha maisha na utume wa Kardinali Protase Rugambwa, Kardinali Laurian Rugambwa, Mtakatifu Yohane Paulo II na kwa namna ya pekee na Askofu mkuu mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka tangu akiwa mwanafunzi Seminari Ndogo ya Itaga, Tabora, akamwachia Jimbo Katoliki Kigoma na sasa amekuwa ni mrithi wake Jimbo kuu la Tabora. Kumbe, Kardinali Protase Rugambwa anayo dhamana na wajibu wa kumtunza Askofu mkuu mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka katika uzee wake. Kanisa linamshukuru na kumpongeza Askofu mkuu mstaafu kwa kazi na utume wake Jimbo Katoliki la Kigoma, Jimbo kuu la Tabora bila kusahau mchango wake katika Urika wa Maaskofu Katoliki Tanzania. Kwa hakika alijitahidi kufanya yote kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, kielelezo na matumaini makubwa kwa Majandokasisi!

Askofu mkuu mstaafu Ruzoka alitumia vyema karama zake kwa ajili ya Kanisa
Askofu mkuu mstaafu Ruzoka alitumia vyema karama zake kwa ajili ya Kanisa

Wakati huo huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kulinda kwa nguvu na gharama zote uhuru wa wananchi wa kutoa mawazo, imani na uchaguzi katika dini, hivyo itahakikisha kunakuwa na amani na utulivu ili uhuru huo wa kuabudu na kutoa mawazo uwepo muda wote. Dkt.Biteko amesema hayo Dominika tarehe 19 Novemba, 2023 wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za kumpongeza Mhasham Askofu mkuu mstaafu Paul Runangaza Ruzoka na kumpokea rasmi Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu mkuu mpya wa Jimbo kuu la Tabora Sherehe zilizofanyika katika Jimbo kuu la Tabora. "Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan muda wote amekuwa akisisitiza haki kwa wananchi wote, na ili kuishi katika misingi ya utangamano haki lazima itawale. Rais anataka wananchi wasikilizwe; tunaweza kutofautiana katika maoni na mitazamo lakini kamwe tusivunje umoja wa kitaifa, tuwaunganishe watanzania na tupambane kuwaondoa wananchi katika umaskini na kuwaletea nafuu kubwa ya maisha." Amesema Dkt.Biteko. Dkt. Biteko amesema kuwa, Mheshimiwa Rais, msisitizo wake ni kupeleka maendeleo kwa wananchi wote bila kuangalia tofauti zao, ikiwemo maji, barabara, umeme, shule na pia lengo lake kuu ni kuendelea kuwaunganisha wananchi wa Tanzania ili kuleta umoja wa Kitaifa.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania

Vilevile, Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais, Dkt.Samia yupo tayari muda wote kushirikiana na taasisi za kidini nchini kuwaletea maendeleo wananchi. Ameendelea kusema kuwa, Serikali itaendelea kuhubiri haki na maridhiano kama msingi wa amani wa nchi na pia itaendelea kuhamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kujiletea maendeleo kwani bila kazi hakuna Taifa. Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko amesema kwamba, Rais ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Askofu mkuu mpya wa Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa kama ambavyo amekuwa akitoa ushirikiano kwa mtangulizi wake Mhasham Askofu mkuu mstaafu Paul Runangaza Ruzoka. Kwa upande wa Askofu mpya wa Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa na Mhasham Askofu mkuu mstaafu Paul R. Ruzoka wameshukuru kwa ushirikiano ambao Serikali imeendelea kuutoa kwao na wameahidi kutoa pia ushirikiano kwa Serikali. Sherehe hizo zilihudhuriwa na Maaskofu, watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Tabora; Viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Burian na Mbunge wa Nzega Vijijini, Hamis Kigwangala. Pia walihudhuria Viongozi mbalimbali wa Madhehebu ya Dini kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Shukrani Jimbo Kuu Tabora
21 November 2023, 14:41