Barua na Waraka kutoka katika Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi na Kimisionari hatua muhimu kuelekea Sinodi ya Mwaka 2024. Barua na Waraka kutoka katika Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi na Kimisionari hatua muhimu kuelekea Sinodi ya Mwaka 2024.   (Vatican Media)

Kuelekea Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu Mwezi Oktoba 2024

Kuelekea Maadhimisho ya Sinodi Mwezi Oktoba 2024. Huu ni mwaliko kwa wale wote walioshiriki katika hatua mbalimbali za Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu wawe ni mashuhuda wa amana na utajiri mkubwa uliowasaidia kujenga ushirika wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, waamini wameitwa na kutumwa na Kristo ambaye ni neema na kiini cha furaha. Hii ni sehemu ya mchakato wa kuimarisha Kanisa la Kisinodi na lile la kimisionari: Ushuhuda wa Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni kabisa kwa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2024, Jumamosi tarehe 9 Oktoba 2021, alitoa hotuba elekezi, ambayo ni msingi wa maadhimisho ya Sinodi katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Watu wa Mungu wakajitambua kuwa wao ni sehemu ya Kanisa la Kisinodi, tayari kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Kristo Yesu, kwa kushirikiana na binadamu wote, kusikiliza kwa makini kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kuyaambia Makanisa. Huu ni wakati wa kuanza tena kufanya hija hii ya kitume kama mwendelezo wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa kunako mwaka 2021 na itafikia kilele chake ni Mwezi Oktoba 2024. Hii ni sehemu ya barua kutoka katika Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi na Kimisionari hatua muhimu kuelekea Sinodi ya Mwaka 2024. Sekretarieti kuu ya Sinodi imekwisha kuchapisha mwongozo utakaotumika katika Maadhumisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu. Sekretarieti kuu inatambua ufinyu wa muda, lakini utashi wa kuendelea na maadhimisho haya ni mkubwa kwa sababu Kanisa linatambua kwamba dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ndiyo njia inayoliingiza Kanisa katika mapambazuko ya Milleni ya tatu ya Ukristo.

Kujenga utamaduni wa kumsikiliza Roho Mtakatifu
Kujenga utamaduni wa kumsikiliza Roho Mtakatifu

Kuelekea Maadhimisho ya Sinodi Mwezi Oktoba 2024. Huu ni mwaliko kwa wale wote walioshiriki katika hatua mbalimbali za Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu wawe ni mashuhuda wa amana na utajiri mkubwa uliowasaidia kujenga ushirika wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, waamini wameitwa na kutumwa na Kristo ambaye ni neema na kiini cha furaha. Ni katika muktadha huu, wajumbe wanahamasika kushirikisha zawadi hii kwa watu wengi zaidi. Itakumbukwa kwamba, muhtasari wa Sinodi ya Mwaka 2021 hadi mwaka 2024 ulioridhiwa na Mababa wa Sinodi katika lugha mbalimbali unapatikana kwenye mtandao wa Sekretarieti kuu ya Vatican kwa anuani ifuatayo: www.synod.va.

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari

Nyaraka hizi ni rejea kwa watu wa Mungu kwa wakati huu na kazi hii itabidi ifanyike tena katika ngazi kuu tatu: Katika ngazi ya Mabaraza ya Maaskofu Kitaifa, Kikanda na hatimaye Kimabara. Kwa mfano katika Afrika Mashariki, awamu ya kwanza inapaswa kuwa ya Maaskofu Kitaifa; Awamu ya Pili ni katika ngazi ya AMECEA na awamu ya tatu ni katika ngazi ya Kimabara yaani SECAM na hatimaye itakuwa ni kwa Kanisa zima na tema kuu ni “Dhana ya Sinodi.” Kuna mambo msingi yanapaswa kujadiliwa katika Kanisa mahalia kwa kushirikiana na Sekretarieti kuu ya Vatican kwa mfano: Majiundo ya Wakleri, Tafiti za kitaalimungu na kichungaji kuhusu Mashemasi; Ushemasi wa wanawake na kwamba, Orodha ya tema mbalimbali ambazo ni matunda ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu zitawasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko. Timu ya wataalam kutoka katika Makanisa mahalia itashirikiana na wajumbe kutoka katika Sekretarieti kuu na hatimaye, taarifa yake kuwasilishwa rasmi wakati wa Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi mwezi Oktoba 2024. Jambo la msingi kwa Makanisa mahalia ni kujiuliza, Je, wanawezaje kuwa Kanisa la Kisinodi katika Utume? Msukumo wa kimisionari wenye uwezo wa kubadilisha, desturi na namna ya kutenda kwa ajili ya uinjilishaji wa ulimwengu mamboleo, badala ya Kanisa kutaka kujilinda lenyewe sanjari na wongofu wa kichungaji. Hapa kuna ngazi mbili zinazopaswa kujadiliwa: Uwajibikaji wa watu wa Mungu katika Kanisa mahalia. Rejea inaweza kufanywa kwa kuzingatia Sura 8-12; 16 na 18. Ngazi ya Pili ni uwajibikaji wa watu wa Mungu kati ya Makanisa pamoja na Askofu wa Roma. Rejea ni katika sura 13; 19 na 20. Huu ni mwaliko kwa Makanisa mahalia kuchangia kwa vitendo kuhusu dhana ya Sinodi.

Sinodi: Ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu
Sinodi: Ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu

Huu utakuwa ni mchango kutoka katika Tume za Sinodi pamoja na kuwashirikisha watu wa Mungu wenye man’amuzi, ujuzi na karama mbalimbali katika maisha na utume wa Kanisa. Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ni rejea katika hatua hii, kwa kukusanya maoni kutoka katika majimbo mbalimbali. Wataalam wa Taalimungu na Sheria za Kanisa wahusishwe, bila kuwasahau watalaam kutoka katika Sayansi za Jamii walioko katika eneo lao. Muhtasari wa kurasa 8 utumwe kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu tarehe 15 Mei 2024 ili kuweza kuandaa “Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris. Ushiriki mkamilifu wa watu wote wa Mungu unaendelea kuhimizwa, lengo ni kuendelea kupyaisha utamaduni wa kusikiliza na kujadiliana hasa na wale ambao wanajisikia wako pembezoni mwa vipaumbele vya Kanisa. Wahusika wakuu ni wajumbe wa Sinodi katika ngazi mbalimbali, Baraza la Maaskofu litakuwa ni mratibu mkuu katika ngazi ya Makanisa mahalia, litaratibu muda na mbinu za kufanyia kazi, litaandika muhtasari utakaowasilishwa kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi tarehe 15 Mei 2024. Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yaendelee kuhamasisha na kuhimiza ushiriki na ushuhuda wa watu wa Mungu, bila kufanyiwa muhtasari, utumwe wote jinsi ulivyo kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu hadi kufikia tarehe 15 Mei 2024.

Sinodi Oktoba 2024
12 December 2023, 15:23