Askofu Mkuu Luis Miguel Munoz Cardaba, Balozi Mpya wa Vatican Nchini Msumbiji
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Msumbiji. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Sudan na Eritrea. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba alizaliwa tarehe 25 Agosti 1965 huko Vallelado, nchini Hispania. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 28 Juni 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Alijiendeleza na hatimaye kubahatika kupata Shahada ya Uzamili katika masomo ya taalimungu, Sheria za Kanisa pamoja na Sheria na Taratibu za Uendeshaji wa Kesi Mahakamani, “Giurisprudenza.”
Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba alianza kutoa huduma za Kidiplomasia mjini Vatican hapo tarehe 1 Aprili 2001. Tangu wakati huo akatumwa kwenye Balozi za Vatican nchini Ugiriki, Mexico, Ubelgiji, Italia, Australia, Ufaransa na Uturuki. N ilipofika tarehe 31 Machi 2020 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi wa Sudan na Eritrea na kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican tarehe 25 Julai 2020. Na hatimaye, 23 Januari 2024 Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba kuwa ni Balozi mpya wa Vatican nchini Msumbiji.