Tafuta

Nembo ya Mfuko wa  Centesimus Annus. Nembo ya Mfuko wa Centesimus Annus. 

Centesimus Annus:Toleo jipya la Kozi ya Mafundisho Jamii ya Kanisa kuanza Januari 20

Mfuko wa Vatican wa Centesimus Annus Pro Pontefice unatarajia kufanya toleo jipya la Kozi ya Mafundisho Jamii ya Kanisa,kwa kuongozwa na mada ya:Mchango wa Mafundisho Jamii ya Kanisa katika ulimwengu kati ya mgogoro na mabadiliko.”Kozi hiyo itaanza Jumamosi tarehe 20 Januari 2024.

Na Angella Rwezaula- Vatican.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mfuko Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” wamebainisha kuwa wanatarajia kufanya Toleo jipya la Kozi ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kuongozwa na mada ya: “Mchango wa Mafundisho Jamii ya  Kanisa katika ulimwengu kati ya mgogoro na mabadiliko.” Kozi hiyo itaanza  mnamo Jumamosi tarehe 20 Januari 2024. Mikutano hiyo inajumuisha kuwa na vipengele saba, vitatu vya kukaa moja kwa moja na vinne vitafanyika  kwa njia ya mtandao. Vikao vitatu vya kukaa moja kwa moja mjini Roma vitafanyika katika Nyumba ya Mchungaji mwema (Casa Bonus Pastor,) iliyopo katika Njia ya Aurelia 208, Roma, na kufanyika  Jumamosi tarehe 20 Januari kuanzia saa 3.30 asubuhi hadi saa 11.30 jioni.

Kwa njia hiyo tarehe za siku tatu za kukaa  moja kwa moja ni  tarehe 20 Januari 2024;  tarehe 24 Februari 2024 na tarehe 23 Machi 2024. Wakati huo huo, vikao kwa njia ya mtandao (online)vitafanyika kuanzia saa 12.30 jioni hadi saa 2.30 usiku. Tarehe za mikutano hiyo minne kwa njia ya mtandao zitakuwa ni siku ya Alhamisi tarehe 1 Februari 2024; Alhamisi tarehe 15 Februari 2024; Jumatano tarehe 28 Februari 2024 na hatimaye Alhamisi tarehe 14 Machi 2024.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kutoka Chama cha Mfuko wa Centesimus Annus  Pro Pontefice ni kwamba “Kwa wale wote ambao wangependa kushiriki wanaweza kupata maelezo kamili katika hati zilizoambatanishwa au kupitia: https://www.centesimusannus.org/corsi/corso-in-dottrina-sociale-della-chiesa/.

Na mwishoni mwa kozi, cheti cha ushiriki kilichotiwa saini na Rais wa Mfuno wa Centesimus Annus Foundation na Mkurugenzi wa Kisayansi wa kozi hiyo itawasilishwa.”

Hata hivyo kwa maelezo zaidi ni kwamba  Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, ulianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo  tarehe 5 Juni 1993. Hii ni kumbu kumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo la mfuko huo ni kufanya upembuzi kufafanua na kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuwasaidia: wafanyabiashara na wataalam katika medani mbalimbali za maisha; kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Vatican katika kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mfuko huu umeendelea kuwa nyenzo muhimu sana ya ushuhuda wa uwepo fungamani wa Kanisa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Mfuko huu unawajumuisha viongozi wa Kanisa Katoliki, wasomi na wataalamu kutoka katika nyanja mbalimbali.

Kozi ya Mafunzo ya Mafundisho Jamii ya Kanisa kuanzia 20 januari 2024
17 January 2024, 17:53