Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu: Hujaji wa Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, O.C.D., alizaliwa tarehe 2 Januari 1873 huko Alençon, Ufaransa, na baadaye akahamia mjini Lisieux, Ufaransa, na kufariki dunia tarehe 30 Septemba 1897. Jina lake la kitawa ni Thérèse Françoise Marie Martin, maarufu pia kama Theresa wa Lisieux. Anaheshimiwa na Mama Kanisa kama Bikira na Mwalimu wa Kanisa. Hata katika udogo wake Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alijitokeza kama mtaalam wa elimu ya upendo inayosimikwa katika unyofu wa hali ya juu na jinsi ambavyo kwa neema alivyoelewa na kutekeleza Injili ya Kristo Yesu katika maisha yake ndani ya monasteri ya Wakarmeli Peku. Theresa alitamani sana kuwa Mtume ili kuokoa roho za watu wengi. Alitamani awe mhubiri, mmisionari na shuhuda. Hata hivyo ilikuwa tu baada ya yeye kujitoa mwenyewe na kujikabidhi kwa upendo wenye huruma ndipo alipogundua wito ambao Mungu alimwitia. Alisema hivi “Nimeelewa kwamba upendo hushikilia miito yote. Natambua kwamba tamaa zangu zote zimetimilika. Nimepata wito wangu. Katika moyo wa Kanisa, mama yangu, mimi nitakuwa upendo.” Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “C'est la Confiance” yaani “Ni Uaminifu” uliotolewa kwa heshima ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwake huko Alençon nchini Ufaransa anasema, Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anaonesha jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa: Upendo na imani katika huruma ya Mungu. Katika waraka wake wa “Njia ndogo ya tumaini na upendo” anawahimiza Wakristo kuamini katika upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo sanjari na kujipatia uzoefu wa kukutana na Kristo Yesu kwa uwazi kwa njia ya wengine. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 25 na Papa Pio XI akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 17 Mei 1925 na tena Mama Kanisa akamtangaza kuwa ni Mlinzi na Msimamizi wa Utume wa Kanisa.
Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Wenyeheri na Watakatifu katika maadhimisho ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, tarehe 7 Januari 2024 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga Mwaka wa Jubilei ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu pamoja na Jubilei ya Miaka 100 tangu alipotangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Katika mahubiri yake amekazia kuhusu: Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; Fumbo la Umwilisho; Nyota angavu ni kielelezo cha upendo wa Mungu; maisha ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Jubilei ya miaka 150 tangu alipozaliwa na miaka 100 tangu alipotangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Kardinali Semeraro anasema Mamajusi kutoka Mashariki walikuwa ni wataalamu wa nyota, watu mashuhuri na matajiri, waliofahamika katika nchi zao, lakini wakajitaabisha kufunga safari na kuanza kumtafuta Mtoto Yesu, Mfalme wa Wayahudi na hatimaye, walipomwona wakamzawadia: Ubani unaonesha Umungu wa Kristo; Manemane ni ushuhuda wa ubinadamu wa Kristo utakaokabiliwa na mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Dhahabu ni kielelezo cha Ufalme wa Kristo Yesu, yaani; Ufalme wa kweli na uzima; Utakatifu na neema; haki, upendo na amani. Kila mwamini anahimizwa kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama chemchemi ya furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Mtoto Yesu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kama ilivyokuwa hamu ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu. “Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” Lk 10:20. Hii ndiyo furaha na imani inayobubujika kutoka kwa waamini, kwa sababu, Mtoto Yesu aliyezaliwa ni ufunuo wa Fumbo la Umwilisho, yaani Uso wa huruma na upendo wa Mungu, tayari kujisadaka hadi kifo cha Msalaba. Kumbe, Jina takatifu la Yesu ni kielelezo cha huruma na upendo wake wa daima. Kristo Yesu ni nyota angavu ya upendo wa Mungu, mwaliko kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu upendo wa Kristo Yesu. Mamajusi walimfikia na kutimiza matakwa yao ya kumwabudu Neno wa Mungu aliyefanyika mwili; hekima katika utoto; nguvu katika udhaifu wa Mtoto Yesu, kielelezo cha ukuu na ukweli wa mwanadamu. Huyu ndiye waliyempatia zawadi za nyoyo zao kwa sababu walimwamini, Mtoto Yesu!
Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alistawisha matamanio yake, kwa kutambua wema na ukuu wa Mungu katika maisha yake; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, alitamani kuona utume wake unaendelea hata mbinguni kwa ajili ya kumpenda Kristo Yesu na kuwasaidia wengine kumpenda pia; na kuendelea kutenda kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kwa ajili ya wokovu wa roho za watu, changamoto na mwaliko kwa waamini kushiriki katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu. Kwa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Wenyeheri na Watakatifu amehitimisha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu pamoja na Jubilei ya Miaka 100 tangu alipotangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Amekumbusha kwamba, Jubilei ya Mwaka 2025 inanogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini” baada ya dhoruba ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na patashika nguo kuchanika kutokana na vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia. Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa Kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumbe, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025, waamini wanahamasishwa kujikita katika sala, chemchemi ya baraka na neema zote. Sala ya maombi inayokita mizizi yake katika msamaha sanjari na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha; sala ya kushukuru kwa kila jambo na mwishoni ni sala ya kusifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa uwepo wake wa daima. Jubilei ya Mwaka 2025 ni fursa ya toba na wongofu wa ndani.