Papa Francisko akutana na Rais Kassym-Jomart Tokayev wa Kazakhstan
Vatican News
Papa Francisko Ijumaa tarehe 19 Januari 2024 amekutana mjini Vatican na rais wa Jamhuri ya Kazakhstan, Bwana Kassym-Jomart Tokayev, ambapo mara baada ya mkutano huo, Rais pia amekutana na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, akifuatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Vyombo vya habari Vatican, imebainisha kuwa majadiliano yalikuwa ya upole, na shukrani ilioneshwa kwa uhusiano mzuri wa nchi mbili kati ya Vatican na Kazakhstan.
Katika mazungumzo hayo hasa, walibainisha kuwa Papa na Rais waliakisi ushirikiano wa pande zote katika eneo la mazungumzo ya kidini na matumaini yalioneshwa kwa jukumu kubwa la waamini katika maisha ya Taifa kwa ajili ya manufaa ya wote. Taarifa pia ilibanisha kuwa “Mazungumzo pia ya kikanda na kimataifa baadaye zilijadiliwa, kwa umakini maalum kwa migogoro na masuala ya kibinadamu, ikizingatiwa umuhimu wa dhamira ya haraka ya kukuza amani na utulivu duniani.”
Hata hivyo ikumbukwa kuwa Baba Mtakatifu Francisko alifanya ziara ya Kitume katika taifa la Asia ya Kati huko Kazakhstan mnamo Septemba 2022, kwa hafla ya Kongamano la Saba la Viongozi wa Dini za Ulimwengu na Dini za Jadi, kuadhimisha Safari yake ya 38 nje ya nchi kama Papa. Wakatoliki ni asilimia 1 tu ya wakazi wa Kazakhstan, ambao asilimia 70 ni Waislamu na asilimia 25 ni Wakristo, hasa Waorthodox wa Urussi.