Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 7 Januari 2024 alikutana na kuzungumza na Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin-Archange Touadéra, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 7 Januari 2024 alikutana na kuzungumza na Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin-Archange Touadéra,   (ANSA)

Rais wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati Akutana na Papa Mjini Vatican

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin-Archange Touadéra, ambaye amekuwepo madarakani tangu tarehe 30 Machi 2016 amekutana na Papa Francisko. Baadaye, Rais amekutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Viongozi hawa wawili, wameridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia na mchango wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 7 Januari 2024 alikutana na kuzungumza na Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin-Archange Touadéra, ambaye amekuwepo madarakani tangu tarehe 30 Machi 2016. Baadaye, Rais amekutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Viongozi hawa wawili, wameridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili pamoja na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Afrika ya Kati. Itakumbukwa kwamba, kuanzia tarehe 24 - 30 Novemba 2015 Baba Mtakatifu Francisko alitembelea: Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Ilikuwa ni fursa kwa viongozi wa kisiasa na kidini nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mchakato wa amani na utulivu, kwa kujenga madaraja ya watu kukutana, tayari kusimamia ustawi, maendeleo na mafao yao kwa kuanza maisha mapya dhidi ya vita, chuki na mipasuko ya kisiasa inayopekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wakutana na Papa
Ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wakutana na Papa

Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ilikuwa ni kiini cha Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika, ili kuwatia shime waweze kuvuka kutoka katika hali yao ya sasa tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha. Baba Mtakatifu alipenda kwenda Afrika ambako kunaonekana na wengi kuwa ni pembezoni mwa jamii, ili kuihamasisha Familia ya Mungu Barani Afrika kusimama kidete kupambana na umaskini, ujinga na maradhi daima wakiambata utu na heshima ya binadamu, msingi wa maendeleo kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu alipokuwa anazungumza na kundi la vijana; wakleri na watawa alikuwa anaweka pembeni hotuba aliyokuwa ameandaa ili kuwashirikisha watu hawa kile kilichokuwa kimefichika katika sakafu ya moyo wake. Uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei Kuu ya Huruma ya Mungu ni kati ya matukio yaliyoacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Alifungua Lango la Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo kuu la Bangui, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Afrika ya Kati, kukimbilia ili hatimaye, kuambata huruma, upendo, msamaha, haki na upatanisho unaobubujika kutoka katika undani wa maisha yao.

Papa Francisko alitembelea Afrika 24-30 Novemba 2015
Papa Francisko alitembelea Afrika 24-30 Novemba 2015

Kwa kitendo hiki, Bangui ikawa ni mji mkuu wa maisha ya kiroho, huko kwenye shida na magumu, kwenye changamoto na kinzani za maisha, huko ndiko Kanisa linakotumwa kwenda kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko na Rais wa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin-Archange Touadéra walijikita pia katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiutu, kwa kuonesha umuhimu wa ushirikiano na mshikamano wa Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Imekuwa ni fursa pia ya kubadilishana zawadi kati yao.

Afrika ya Kati
31 January 2024, 15:26