Sikukuu ya Mtakatifu Don Bosco, Baba, Mwalimu na Rafiki wa Vijana wa Kizazi Kipya
Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB., - Vatican.
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, ni mwaka mwingine tena ambapo tunasherehekea Sikukuu ya Mtakatifu Yohane Bosco ambae Mama Kanisa ametupatia kama Baba, Mwalimu na Rafiki wa vijana. Sikukuu hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 31 Januari. Kwetu sisi kama Familia ya Kisalesiani ulimwenguni kote ni jambo linaloleta furaha hasa tukikumbuka yale aliyoyaishi na aliyotuachia Mtakatifu huyu. Kama ilivyo ada kila mwanzo wa Mwaka Mkuu wa Shirika la Wasalesiani ulimwenguni hutoa ujumbe kwa wanafamilia wote wa Kisalesiani ambao huwa ni Kauli mbiu inayotuongoza katika kutafakari na kuishi kikamilifu kile ambacho Mtakatifu Yohane Bosco ametuachia kama zawadi katika maisha yake. Mwaka huu ni mwaka wa kipekee sana ambapo tuna enzi miaka 200 tangu kijana Yohane Bosco alivyopata ndoto akiwa na umri wa miaka tisa yaani mnamo mwaka 1824. Ndoto hii ndiyo iliyomfanya aweze kutambua wito ambao Mwenyezi Mungu amemwita. Ni ndoto ambayo Don Bosco mwenyewe aliendelea kuwa nayo akilini na moyoni mwake katika maisha yake yote. Hivyo basi Mkuu wetu wa Shirika Mwadhama Angel Kardinali Fernandes Artime. Ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 30 Septemba 2023 Baba Mtakatifu Francisko alimteua Mheshimiwa sana Padre Angel Fernades Artime kuwa Kardinali, ambaye mwaka huu wa 2024 anatualika kutafakari Kauli Mbiu isemayo: “Ndoto ikuleteayo Maono”: Moyo unaowabadilisha Mbwa Mwitu kuwa Wanakondoo.” Je, ndoto hii ilikuwa inahusu nini? Don Bosco Mwenyewe anasimulia: Katika ndoto hii, nilikuwa karibu na uwanja mkubwa sana nyumbani kwetu. Kundi la watoto walikuwa wanacheza huku Baadhi yao walionekana wakifurahi, wakicheza michezo mbalimbali, na baadhi walikuwa wakiongea lugha chafu. Niliruka mara moja kati yao na kujaribu kuwazuia kwa kutumia maneno na ngumi. Wakati huo, Mwanaume aliyevaa vizuri na kwa heshima alitokea. Alikuwa amevaa kanzu nyeupe na uso wake uliang’aa na hivyo sikuweza kumtazama moja kwa moja. Aliita jina langu, akaniambia niwajibike kwa watoto hawa, na kuongeza maneno haya: "Utawashinda hawa marafiki zako si kwa makofi na ngumi bali kwa upole na upendo. Anza mara moja kuwafundisha ubaya wa dhambi na thamani ya fadhila." Nilijawa na hofu. Wakati huo huo, watoto wale waliacha kupigana, kupiga kelele, na kuongea lugha chafu; wakakusanyika karibu na yule Mtu aliyekuwa akizungumza nami.
Niliuliza, "Wewe ni nani, kuniamuru kufanya jambo lisilowezekana?" "akaniambia… kwa nguvu zako mwenyewe hautoweza… hivyo lazima ufanye iwezekanavyo kupitia utii na kupata maarifa." "Wapi, kwa njia gani, naweza kupata maarifa?" "Nitakupa mwalimu. Chini ya mwongozo wake, unaweza kuwa mwenye hekima. Bila yeye, hekima yote ni upumbavu." "Lakini wewe ni nani unayesema hivyo?" "Mimi ni mwana wa mwanamke ambaye mama yako amekufundisha kumsalimu mara tatu kila siku." "Mama yangu huniambia nisiwe karibu na watu nisiowajua isipokuwa nikiwa na ruhusa yake. Basi niambie jina lako." "Uliza mama yangu jina langu ni nani." Wakati huo, nilimwona mwanamke mwenye umbo lenye hadhi akisimama karibu naye. Alikuwa amevaa vazi lilofunika kote na linalong'aa kama nyota nzuri. Akanikaribisha kumkaribia, akanichukua kwa upole kwa mkono na kusema, "Tazama." Nikatazama pande zote, nikagundua kwamba vijana wote hawapo na wamekimbia, waliochukua nafasi yao walikuwa mbuzi, mbwa-mwitu, na wanyama pori wengine. "Huu ndio uwanja wa kazi yako. Jifanye kuwa mnyenyekevu, imara na Hodari. Na kile utakachokiona kikitokea kwa wanyama hawa baadaye, ndicho unachopaswa kukifanya kwa watoto wangu." Nikatizama tena, na mahali ambapo awali niliona wanyama pori, sasa niliona kondoo wenye upole. Walikuwa wote wakiruka na kufurahi. Wakati huo, bado nikiwa kwenye ndoto, nilianza kulia. Nilimsihi mwanamke yule azungumze ili niweze kumwelewa, kwa sababu sikujua maana ya haya yote. Kisha akaweka mkono wake kichwani mwangu na kusema, "Wakati mwafaka utaelewa kila kitu." Baada ya hapo, kelele ziliniamsha na kila kitu kikatoweka. Nilikuwa nimechanganyikiwa kabisa. Kumbukumbu ya yule mwanaume na yule mwanamke, na mambo yaliyosemwa na kusikika, yalichukua nafasi kubwa akilini mwangu hivi kwamba sikupata usingizi tena usiku huo. Niliwaeleza kwanza ndugu zangu, ambao walicheka sana, na kisha mama na bibi yangu. Kila mmoja alitoa tafsiri yake mwenyewe.
Ndugu yangu Yosefu alisema, "Utakuwa mlinzi wa mbuzi, kondoo, na wanyama wengine." Mama yangu alisema, "Nani anajua, labda utakuwa padre." Kaka yangu Antoni alisema kwa kunyamaza tu, "Labda utakuwa kiongozi wa wezi." Lakini bibi yangu, ingawa hakuweza kusoma wala kuandika, alifahamu teolojia ya kutosha na kutoa hukumu ya mwisho akisema, "Usiipe kipaumbele ndoto." Nilikubaliana na bibi yangu. Walakini, sikuweza kuondoa ndoto hiyo akilini mwangu. Hii ndio ndoto ambayo alikuwa nayo Don Bosco, ndoto iliyomfunulia mambo mengi kuhusu wito wake na maisha yake ya baadae. Ndoto ya kinabii na yenye thamani sana si kwake tu bali hata katika Familia nzima ya Don Bosco. Katika ndoto hii tunaona wahusika wakuu ni vijana, ambao hawasemi neno wala kuzugumza chochote lakini yote huzunguka katikati yao na kwa ajili yao. Vijana ambao wapo kama walivyo katika shughuli na harakati zao, wengine wakiwa ni wenye ukali, magomvi, kutokuvumiliana (kama mbwa-mwitu), lakini ujio wa Mwanamke wa Ndoto, ambaye ni Mama Maria na mbele ya macho ya kijana Yohane wanabadilika na kuwa vijana wazuri (kama kondoo), walio watulivu, wenye urafiki na wakarimu. Kumbe ni muhimu kutafakari na kukumbuka kuwa mchakato wa mabadiliko daima unawezekana, kutoka kuwa mbwa-mwitu hadi kuwa kondoo, na kutoka kuwa kondoo hadi kufurahia uwepo wa Yesu na Maria katika maisha yao. Na ndivyo tunaalikwa kila mmoja wetu hasa Familia nzima ya Don Bosco kuwa na uvumilivu na kuamini kuwa katika kijana kuna thamani kubwa na mabadiliko ya kweli yanawezekana. Sharti ni moja tu kama lile aliloambiwa kijana Yohane Bosco: Jifanye kuwa mnyenyekevu, imara, na hodari.
Uwepo wa Mama Bikira Maria katika ndoto hii ni kitu cha muhimu sana. Hili tunaliona kupitia kawa Yesu (mwanaume katika ndoto) anapomwambia kijana Yohane kuwa “Nitakupa mwalimu. Chini ya mwongozo wake, unaweza kuwa mwenye hekima. Bila yeye, hekima yote ni upumbavu”. Kumbe Mama Maria ndiye Mwalimu aliyekabidhiwa kwake kijana Yohane Bosco na ambaye atakuwa mstari wa mbele kama mtu muhimu katika wito wake. Kumbe, karama yetu ya Kisalesiani inatokana na uwepo muhimu wa Mama Maria. Mama huyu amekuwa daima katika maisha ya Mt Yohane Bosco, amekuwepo pale katika kumshauri kwa njia nyingi za ndoto, katika miujiza na neema nyingi. Bikira Maria ni kila kitu kwa Don Bosco, hivyo nasi pia tunaalikwa kuwa na ibada ya kweli kwa Mama huyu. Katika kuelimisha vijana lazima tukumbuke kwa “Sio kwa ngumi wala mabavu” maneno ambayo Bikira Maria anamwambia kijana Yohane katika ndoto, bali kwa upole na upendo. Tukumbuke kwamba njia ya nguvu na ukatili haitoi muongozo sahihi wa malezi kwa vijana. Baba Gambera Mkuu wa Shirika anatualika nasi kuwa na maono, kuwa na ndoto kwa maana bila ndoto hakuna maisha. Umaskini mbaya zaidi ni ule wa kumzuia mtu kuota, kuwa na maono. Kila mmoja wetu ni ndoto ya Mwenyezi Mungu. Ni muhimu kujua ndoto yangu ni nini, ni ndoto gani Mwenyezi Mungu anayo kwangu. Na hivyo ni lazima tujaribu kuikuza, kuifanikisha kwa sababu inahusu furaha yetu na ndugu zetu. Enyi wazazi, walimu, na wote tuliopatiwa jukumu la kulea, tusiwakatishe tamaa watoto wetu, vijana wetu katika zile ndoto ambazo wanazo katika maisha, tuwasaidie kusikiliza mioyo yao, kutambua mienendo yao ya ndani. Tuzidi kuwapatia vijana fursa za kukutana na Yesu, ambae ni chanzo cha uzima na furaha kwa kila kijana. Tukumbuke maneno ya Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana kuhusu wito wao: “Mimi ni utume duniani; ndio maana nipo hapa duniani. Hivyo, kila aina ya shughuli za kichungaji, malezi na utakatifu vinapaswa kuonekana katika mwanga wa wito wetu wa Kikristo” (ChrV 254). Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, natumaini tafakari hii itatujenga kila mmoja wetu hasa vijana kujua na kutambua wito wetu katika maisha. Tusiache kuwa na maono na ndoto maana ni katika ndoto ndipo Mwenyezi Mungu anaongea nasi. Bikira Maria Msaada wa Wakristo aendelee kuwa Mama na Mwalimu wetu wa kweli, aendelee kutuongoza na kutushika mkono. Nawatakia heri na Sikukuu njema ya Mtakatifu Yohane Bosco kwenu nyote na Familia nzima ya Kisalesiani, na Maadhimisho mema ya miaka 200 tangu kijana Yohane Bosco alipopata ndoto akiwa na umri wa miaka tisa.