Watawa wajiandaa na Jubilei ya 2025,Kard.De Aviz:ni katika mtindo wa Sinodi!
Bianca Fraccalvieri na Angella Rwezaula, - Vatican.
Zaidi ya wawakilishi 300 wa masharika ya maisha ya kuwekwa wakfu mbali mbali kutoka zaidi ya nchi 60 Duniani watakutana mjini Roma kuanzia tarehe 1 hadi 4 Februari 2024 kwa ajili ya mkutano wa maandalizi ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu 2025. Hawa ni watawa wa kike na kiume mashirika na taasisi za Ulimwenguni na vile vile za waliowekwa wakfu wa Ordo Virginum kwa kila nchi ambapo watakuwa na hatua mpya katika safari ya kuelekea Mwaka Mtakatifu ili kubadilishana uzoefu wa maisha na utume, kwa lengo la kurejea katika nchi zao na dhamana ya kuendelea kuwa ishara ya upatanisho kati ya watu.
Hija ya watawa Oktoba 8-9,2025:Mahujaji wa matumaini katika njia ya amani
Kauli mbiu ya Jubilei ya hija ya Watawa ni “Mahujaji wa matumaini, katika njia ya amani" itakayofanyika mjini Roma kuanzia tarehe 8 na 9 Oktoba 2025. Kwa hiyo wanaume na wanawake waliowekwa wakfu wanataka kutafakari hitaji kuu la amani, udharura wa wakati wetu na kujibu wito wa Papa Francisko wa kujenga, kwa njia ya safari ya Jubilei, hali ya matumaini na uaminifu kama ishara ya kuzaliwa upya kwa binadamu wote. Hayo yalisisitizwa na Kadinali João Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Vyama vya Harakati ya Maisha ya Kitume. Kwa kufafanua zaidi alisema “Tulitaka kujihusisha pamoja na watu wengine wote katika Kanisa katika maandalizi madhubuti ulimwenguni kote kwa sababu tupo ulimwenguni kote kwa ya Jubilei ya 2025. Mkutano huu ni wa kwanza kati ya mfululizo wa matukio ambayo yanaleta pamoja mabara matano. Ulitayarishwa kwanza mtandaoni lakini pamoja. Kila kitu ambacho ni mpango, kila kitu ambacho tutapata, tulifanya pamoja. Na tutajaribu kuishi kama kikao cha kwanza cha Mkutano wa Sinodi kwa kuketi karibu na meza, tukisikilizana kwa makini, katika nuru ya Neno la Mungu.”
Maisha ya wakfu yanaishi sinodi kila siku
Maisha ya wakfu kimsingi yanakutana na Sinodi kwa hiyo ni “Mtindo mpya wa kuandaa wakati muhimu sana kwa Kanisa kama vile Jubilei, ambayo hutuleta karibu na uzoefu wa Mungu", alisisitiza Kardinali Braz de Aviz, huku akihakikishia hamu ya sote tuliowekwa wakfu kutayarisha na kujitayarisha vizuri kwa ajili ya tukio hilo. Kardinali alisema “Tuko katika wakati wa mageuzi, ya kufanywa upya maisha ya kuwekwa wakfu, yenye matatizo mengi na ni kweli lakini pia mabadiliko mengi katika kumfuata Kristo. Tuko na tunataka kuwa zawadi kwa Kanisa, lazima tupumue na kuishi na Kanisa na kwa hivyo tunataka kuanza mara moja, kisha tutakuwa na mikutano mingine ya kina.”
Mpango wa mkutano huo na mada zake kuu 4
Mpango huo utaendelezwa kupitia mada nne kuu: tarehe 1 Februari 2024 ni Kuamini katika matumaini; tarehe 2 Februari ni Kukua katika upendo; tarehe 3 Februari ni Kwa nguvu ya imani; na hatimaye tarehe 4 Februari mada itakuwa ni Tumaini la Kushuhudia. Ili kuimarisha mazungumzo hayo, wawakilishi wa Mabaraza ya Curia Romana pia watakuwepo, akiwemo Padre Paulin Batairwa Kubuya, katibu wa Baraza la Kipapa la Mazungumzo ya Kidini na Sista Alessandra Smerilli, Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu.
Tembea na kila mmoja
Kardinali alisema kuwa “Kwa wakati huu njia nzima ambayo Kanisa inapitia na ambayo Papa Francisko anaifanya ni njia ambayo lazima tugeuke, yaani, mtindo mpya wa kutembea pamoja, tukiwa na hakika kwamba hii ndiyo njia ya kuwa Kanisa.” Kwa kusisitiza Kardinali De Aviz alisema “Leo haijalishi kwamba nina wito wangu na kwamba mwingine ana wito pia, lakini, sisi sote kwa pamoja tunaunda ukweli wa Kanisa.” Kulingana na Kardinali, mtindo huu unaweza kujifunza. Na lazima tujifunze hili wakati ambapo ubinafasi imeingilia hali ya kiroho. Kwa hiyo tunahitaji ishara za leo hii ambazo ni ishara za mawasiliano na ya kuwa pamoja. Hata hapa ndani ya Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na vyama vya Kitume baada ya kikao cha kwanza cha Sinodi, mara moja walianza kushirikishana mambo kati yao , hawa wao kama waratibu na watu wote wanaofanya kazi huko, karibu 40 ... “Tunafanya kazi kwa wazo kwamba 'ninyi ni sehemu ya wengine, mnaamua na mwingine, mnatembea na mwingine'. Hii, kwa maoni yake, itazaa matunda mengi katika siku zijazo.”
Sherehe na Papa mnamo 2 Februari 2024
Tukio hilo jijini Roma pia lifanyika katika siku ambazo kila tarehe 2 Februari ni Siku ya walio wekwa wakfu. Siku hiyo Papa Francisko ataongoza sherehe za kawaida katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican misa. Kardinali Braz de Aviz alieleza kuwa: “Tuna furaha sana kwa sababu Baba Mtakatifu amethibitisha kwamba atakuja kusherehekea pamoja nasi. Tutakuwa pamoja kutekeleza matayarisho ya Jubilei, kulingana na tunu ambazo Papa mwenyewe amezibainisha kwa ajili yetu na kwamba ni kuwa 'mahujaji wa matumaini' wakati ambapo maisha yanataabika na vita na magonjwa". Tumaini la mkuu wa Baraza la Kipapa hilo ni kwamba “kutokana na matatizo haya fadhila aliyo nayo Mkristo ya matumaini moyoni mwake inajitokeza. Tunaongeza kwa hili hamu ya kujiandaa kwa Mwaka Mtakatifu tukiwa na hamu ya amani katika jumuiya zetu na katika ulimwengu mzima."