Padre W.H.Kibozi ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dodoma,Tanzania
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jumatatu tarehe 12 Februari 2024 Kanisa nchini Tanzania linayo furaha kubwa kwa kumpata Askofu mwingine mpya, kwa sababu, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma nchini Tanzania, Mheshimiwa sana Padre Wilbroad Henry Kibozi, wa Jimbo Kuu hilo hilo, ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni Makamu Gambera na Profesa wa Seminari kuu ya Familia Takatifu, Kahama, kwa kumpatia makao ya Zallata.
Wasifu wake
Askofu Mteule, Padre Wilbroad Henry Kibozi alizaliwa mnamo tarehe 30 Aprili 1973 mjini Dodoma. Majiundo yake baada ya sekondari alisoma Falsafa katika Seminari Kuu ya Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Kipalapala Jimbo Kuu Katoliki la Tabora. Baada ya kufanya shughuli za kichungaji kwa muda wa mwaka mmoja katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji huko Chalinze (Dodoma), aliendelea na masomo na kupata leseni na Shahada ya Udaktari wa Taalimungu katika Kitivo cha Taalimungu cha Italia ya Kati huko Firenze.
Daraja la Upadre
Alipewa daraja takatifu la Upadre mnamo tarehe 9 Julai 2010 kwa ajili ya Jimbo lake kuu, Dodoma Tanzania.
Nyadhifa
Alishika hata nyadhifa nyingine kama vile: Paroko msaizidi wa Lumuma (2010-2012); Mkurugenzi wa Miito Jimbo Kuu la Dodoma (2012-2014); Muungamishi katika Nyumba ya Malezi huko Livorno, Italia (2017-2019); Mkufunzi wa Waseminari katika Chuo Kikuu cha Jordan, Morogoro (2019-2020); tangu 2020, amekuwa Makamu Gambera na Profesa katika Seminari Kuu ya Familia Takatifu ya Kahama, Tanzania.