Fiducia supplicans:baraka zisizo za kiliturujia na tofauti ya Ratzinger
Na Andrea Tornielli
Katika Tamko la (Fiducia Supplicans:On the Pastoral Meaning of Blessings,)kuhusu maana ya Baraka za kichungaji lililochapishwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa mnamo Desemba iliyopita, kama kila mtu ajuavyo na kama inavyosisitizwa na wengi, halibadili fundisho la kimapokeo kuhusu ndoa, ambalo hutoa baraka za ndoa tu kwa mwanamume na mwanamke wanaojongea katika ndoa. Kile ambacho hati inachunguza, kwa kukubali uwezekano wa baraka rahisi za hiari hata kwa wanandoa wasio wa kawaida, wachumba sugu au wale wanaojumuisha watu wa jinsia moja, bila kuashiria kubariki muungano wao au kuidhinisha njia yao ya maisha, badala yake ni asili ya baraka.
Fiducia Supplicans hutofautisha kati ya baraka za kiliturujia au sala za ibada na zile za hiari au za kichungaji. Kuna njia mbili ambazo hapo awali, baraka za kiliturujia, zinaweza kueleweka. Kuna maana pana, ambayo inazingatia kila sala inayofanywa na mhudumu aliyewekwa rasmi kuwa ya “liturujia,” hata ikiwa inatolewa bila mtindo wa ibada na bila kuzingatia maandishi rasmi. Na kuna maana finyu zaidi, kulingana na ambayo sala au maombi juu ya watu ni “liturujia” tu inapofanywa “kiibada,” na kwa usahihi zaidi inapotegemea maandishi yaliyoidhinishwa na mamlaka ya kikanisa.
Baadhi ya wakosoaji ambao wametilia shaka Tamko la hivi karibuni wanaona maana pana tu inaruhusiwa na kwa hiyo hawakubali tofauti kati ya sala au baraka za “kiibada” na “maombi” na “kichungaji” na “sala” au baraka za “pamoja.” Miongoni mwao, wengine wanapinga kwamba hata liturujia ina umuhimu wa kichungaji. Lakini ni muhimu kutambua kwamba Fiducia Supplicans inahusisha maana maalum kwa neno “mchungaji.” Yaani, ile ya namna fulani ya umakini iliyoelekezwa maalum kwa kuwasindikiza wale wanaopewa baraka, kwa mfano wa “Mchungaji Mwema”ambaye hapumziki mpaka ampate kila mmoja wa wale waliopotea.
Wengine wanasema kwamba sala zote ni za “kiliturujia,” na kwa hivyo zote ziko chini ya matakwa ya liturujia ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko mwenyewe alijibu pingamizi hili katika hotuba yake kwa washiriki wa kikao cha Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa tarehe 26 Januari, akisisitiza juu ya uwepo wa baraka za kichungaji au za hiari ambazo “ziko nje ya muktadha na muundo wowote wa kiliturujia” na “ hazihitaji ukamilifu wa maadili ili kupokelewa.”
Maneno ya Papa hivyo yanathibitisha maana finyu ya baraka za kiliturujia. Kuna mfano muhimu kuhusu tofauti kati ya kile ambacho ni kiliturujia na kisichokuwa cha kiliturujia. Inapatikana katika (Instruction)yaani Mwongozi wa mwaka 2000, uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho ya Imani la wakati huo, uliotiwa sahihi na Kardinali Joseph Ratzinger na kuidhinishwa na Papa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.
Mwongozo ulikuwa juu ya sala ya uponyaji. Kipengele cha pili cha sehemu ya kwanza ya waraka huo kinakumbusha kwamba: “Katika (De benedictionibus of the Rituale Romanum) ibada za baraka ya kiroma, (Ordo benedictionis infirmorum,) ambamo kuna maombi mbalimbali ya uponyaji.” Katika sehemu ya mwisho ya mwongozo uliowekwa kwa kanuni za nidhamu, kuna kifungu cha (2) kinachosema: “Maombi ya uponyaji yanachukuliwa kuwa ya kiliturujia ikiwa ni sehemu ya vitabu vya kiliturujia vilivyoidhinishwa na mamlaka yenye uwezo wa Kanisa; Kinyume chake sio za kiliturujia.” Kwa hiyo, imethibitika kwamba kuna maombi ya uponyaji ambayo ni ya kiliturujia au maombi na mengine ambayo hayajakubaliwa lakini bado yanakubaliwa kihalali.
Kifungu kinachofuata kinakumbusha kwamba sala hizo za “kiliturujia” huadhimishwa kulingana na utaratibu uliowekwa na kwa mavazi matakatifu yaliyooneshwa katika Mwongozo wa baraka za ibada ya wagonjwa (Ordo benedictionis infirmorum ya Rituale Romanum.) Nukuu hizi kutoka katika maandishi yaliyotiwa saini na Kardinali Ratzinger na kuidhinishwa na Papa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, yanaonesha kwamba maana ya neno“liturujia” linalotumiwa katika Fiducia Supplicans kufafanua baraka za ibada, ambazo ni tofauti na zile za kichungaji, hakika ni maendeleo mapya lakini yaliyoingizwa ndani ya mfumo wa Majisterio ya miongo iliyopita. Miongoni mwa baraka, kuna tofauti nyingine: baadhi huwakilisha kuwekwa wakfu, au muhuri wa sakramenti inayoadhimishwa na wanandoa (katika muktadha wa baraka ya harusi); nyingine huwakilisha maombi yaliyoinuliwa kwa Mungu; na nyingine bado (kama vile kutoa pepo) zina madhumuni ya kuepusha maovu.
Fiducia Supplicans kwa mara nyingine inafafanua kwamba kutoa baraka ya kichungaji au ya hiari - bila kipengele chochote kinachohusiana na ndoa - kwa watu wasio wa kawaida,” wachumba sugu, ambao wanakaribia kuhani au shemasi haimaanishi na haiwezekani kuwakilisha kwa njia yoyote idhini ya muungano kati ya wawili. Kama inavyosema hati, haiwezi kuchukuliwa kama kutoa “aina ya uhalali wa kimaadili kwa muungano unaodhaniwa kuwa ndoa” au “tendo la ngono nje ya ndoa.” Badala yake, maana yake ni ile ya ombi la kumwomba Mungu aruhusu mbegu za wema zikue kuelekea upande anaoutaka Mungu.