'Katika uzee wangu usiniache' ni mada ya Siku ya IV ya Babu/bibi na Wazee duniani 2024
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Alhamisi tarehe 15 Februari 2024, Kardinali Kevin Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei Familia na Maisha, ametoa kauli mbiu iliyochaguliwa kwa Siku ya IV ya Babu/bibi na Wazee. Katika taarifa yake amesema kuw: “Dominika tarehe 28 Julai 2024 itaadhimishwa Siku ya IV ya Babu/bibi na Wazee Ulimwenguni. Kauli mbiu iliyochaguliwa na Baba Mtakatifu ni “ Katika uzee wangu usiniache”(Zab71,9), ambayo inataka kusisitiza jinsi ambavyo upweke kwa bahati mbaya ni mchungu ukisindikiza maisha ya wazee wengi na mara nyingi,ni waathiriwa wa utamaduni wa kubagua.”
Katika taarifa hiyo aidha inabanisha kuwa: “Katika mwaka wa maandalizi ya Jubilei ambayo Baba Mtakatifu amechagua kujikita kwa sala, Kauli mbiu ya Siku hii imetolewa katika Zaburi ya 71 ambayo ni sala ya mzee anayepitia historia yake ya urafiki na Mungu.” Kwa mujibu wa Kardinali Kevin Farrell, amesisitiza kuwa: “Maadhimisho ya Siku, haya yanathamanisha karama za babu/ bibi na Wazee na uhusiano wao na maisha ya Kanisa, ambayo inataka kusaidia jitihada za kila Jumuiya ya Kanisa katika kujenga uhusiano kati ya kizazi na kupambana na upweke kwa utambuzi kuwa kama maandiko yanavyothibitisha: “ Sivizuri binadamu kuishi peke yake”(Mw 2,18).