2024.02.19 Kardinali Rugambwa,Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la  Tabora-Tanzania katika Kanisa lake la Bikira Maria wa Montesanto, Roma. 2024.02.19 Kardinali Rugambwa,Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora-Tanzania katika Kanisa lake la Bikira Maria wa Montesanto, Roma.  (Vatican Media)

Kard.Rugambwa akabidhiwa rasmi Kanisa la Mtakatifu Maria wa Montesanto,Roma!

Tarehe 18 Februari 2024 katika Basilika ndogo ya Mtakatifu Maria wa Montesanto,Roma ijulikanayo kama Kanisa la Wasanii,Kardinali Rugambwa,Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora-Tanzania alisema:“Uzuri wa sanaa ni njia pekee ya uinjilishaji"kama asemavyo Baba Mtakatifu."

 Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Dominika tarehe 18 Februari 2024, hatimaye siku iliyokuwa  inasubiriwa imetimia kwa sababu Kardinali Protase Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora (Tanzania), aliongoza Misa Takatifu katika fursa ya kukabidhiwa Kanisa la Mtakatifu Maria wa Montesanto, njia ya Babuine,198 Roma. Kanisa hili kwa hakika linajulikana sana kama Kanisa la Wasanii. Kiutamaduni kabla ya kuingia Kanisani alibusu msalaba, baadaye akapiga magoti   mbele ya na kusali lakini pia kulikuwa na tendo la kuwabariki waamini kwa maji ya baraka. Na baadaye alikwenda kuvaa mavazi rasimi ya misa na kuanza misa Takatifu. Baada ya masomo ya Dominika ya Kwanza ya Kwaresima Kardinali Rugambwa alianza mahubiri yake na kusema: Wakati umetimia na Ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini Injili” (Mc 1,15). Kwa maneno haya Yesu anaanza mahubiri, akitembea kutoka Galilaya, eneo la kaskazini ambalo lilikuwa linachukuliwa kama nchi ya waasi na waliotengwa, kwa sababu wengi wa watu wa mji huo hawakuwa wakienda hekaluni Yerusalemu kwa ajili ya ibada. Anachagua eneo ambalo aliishi kwa takriban miaka thelathini, na hapo ndipo anapoanza kutangaza Habari Njema.

Siku ya Kukabidhiwa Kanisa la Roma , Kardinali Rugambwa
Siku ya Kukabidhiwa Kanisa la Roma , Kardinali Rugambwa

Kwa kukamatwa kwa Yohane Mbatizaji, ambaye alifungwa mdomo kwa mabavu ya Herode, Yesu anaelewa kuwa “wakati wake umefika.” Kati ya Yohane na Yesu, waliokuwa ndugu (mabinamu) kunatokea mwendelezo wa jukumu mintarafu utume wao kwa ajili ya Ufalme wa Mungu. Wote wamezaliwa kwa ajili ya kutangaza la Neno la Bwana lililokamilika, likileta uhai katika utasa wa Elisabeti na katika ubikira wa Mariamu. Yohane na Yesu ni mashahidi wa ufanisi wa Neno umbaji la Mungu na wanaweka maisha yao yote katika huduma ya Neno hilo. Kwa sababu hiyo, kwa kuwa “Neno la Mungu halifungwi,” kama anavyotumbia Mtume Paulo (1Tim 2,10), mara tu Yesu anaposikia habari ya kukamatwa kwa Yohane Mbatizaji, anatangaza: “wakati umetimia na ufalme wa Mungu umekaribia”(Mk1:15).

Utambulisho wa  dhati wa kukabidhiwa Kanisa Kardinali Rugambwa
Utambulisho wa dhati wa kukabidhiwa Kanisa Kardinali Rugambwa

Yesu anamaanisha nini kwa kusema “wakati umetimia”? Ni vigumu kueleza maana halisi ya kauli hiyo kwa Kigiriki. Ni kama vile anasema kuwa wakati umefika akilenga wakati unaofaa, wakati muhimu na wa maamuzi umefika katika historia ya mwanadamu. Wakati wenye umuhimu usio na kifani katika mpango wa Mungu wa wokovu wa mwanadamu. Mtume Paulo anazungumzia “utimilifu wa nyakati” (Wagalatia 4,4) akirejea wakati wa utimilifu wa ahadi ambao unafikia kilele chake. Kwa kusema “wakati umekamilika,”maandiko yanarejelea zaidi wakati wa sasa, wakati huu; yaani, leo ya maisha yetu, ambapo mabadiliko muhimu yanaweza kutokea kwa ajili ya mustakabali wetu wote. Yesu anatualika kutumia vizuri fursa hii ya wakati tunaokuwa nao, hii kairòs, yaani, wakati wa wokovu ambao umewadia kwa wote. Ndiyo maana anakazia kwamba “Ufalme wa Mungu u karibu.” Hivyo basi, ni wakati muafaka kwa sababu ujio wa Ufalme wa Mungu u karibu. Kimsingi, utawala wa upendo wa Mungu kwa mwanadamu tayari umeanza. Kama vile ilivyokuwa katika mahubiri ya Yohane Mbatizaji, kwa Yesu vivyo hivyo, Ufalme wa Mungu ndio ujumbe msingi. Lakini katika habari njema inayotangazwa na Kristo, Ufalme tayari upo na unafanya kazi katika nafsi Yake mwenyewe. Kwa hivi, “wakati umekamilika” na "Ufalme wa Mungu u karibu,” Yesu anatuhimiza: “tubuni na kuamini Injili.”

Misa ya Kukabidhiwa Kanisa , Kardinali Rugambwa
Misa ya Kukabidhiwa Kanisa , Kardinali Rugambwa

Ndugu zangu wapendwa, hilo ndilo Neno ambalo Bwana wetu anatupatia katika Jumapili hii ya kwanza katika safari yetu Kwaresima. Kwa unyenyekevu wote tuyatazame kwa makini maisha yetu, tukijua kwamba Kristo leo anapiga hodi katika milango ya mioyo yetu, akitualika kutubu, anatualika kuongoka. Tunaposikia mwito huu wa toba, tunahimizwa kutafakari juu ya mambo yote ambayo tunahitaji kufanya ili kubadilika na kuwa kama Bwana anavyotaka. Toba na wongofu, kwa nafasi ya kwanza, ni matunda ya kazi ya Mungu ndani yetu na Roho Mtakatifu mtendaji wa kazi hiyo, sio sisi peke yetu. Tunawiwa kuupenda, kuutamani, kuomba kuupokea, na tukiruhusu Kristo Bwana mwenyewe aitimize ndani kazi hiyo ndani yetu. Kuongoka si tu kubadilisha mwelekeo, kugeuza njia kurudi kwenye njia kuu, zaidi sana ni kupokea mwanga mpya kutoka kwa Mungu, ambao unaturuhusu kubadilisha mtazamo wetu, kwenda zaidi ya njia yetu ya kawaida ya kufikiri na kuhusiana na Bwana wetu, na watu wengine, na mambo yetu ya kila siku. Jumatano iliyopita, wakati wa kupakwa majivu, tulipewa mwaliko: “tubu na uamini Injili.” Ndugu zangu wapendwa, pengine tunajiuliza: ni kwa jinsi gani basi kazi ya toba inaweza kuanza mioyoni mwetu? Jibu lake basi ni kuamini Injili, kuchukua kwa uzito Habari Njema ya wokovu, na kukubali kupokea upendo wenye huruma wa Mungu Baba anayesamehe na kuokoa. Toba ni jambo linalowezekana leo na linapatikana kwa kila mmoja wetu, ikiwa tutataka.

Mapadre wakati wa Misa ya kukabidhiwa Kanisa Kardinali Rugambwa
Mapadre wakati wa Misa ya kukabidhiwa Kanisa Kardinali Rugambwa

Tumwombe Kristo Bwana katika kipindi hiki cha Kwaresima, atupe neema ya toba na wongofu wa kweli mioyoni, ili tuweze kuendelea vizuri na safari yetu ya maisha tukiitazama dunia na historia yetu kwa macho mapya. Asiwepo yeyote wa kusakamwa na huzuni na kukata tamaa hata kudhani kwamba ni vigumu kuanza upya katika maisha. Tunaweza daima kuinuka na kuendelea na safari, hata kama tumekuwa tukijikwaa mara nyingi na bado tunateseka. Katika safari hii ya toba, ambapo tunajifunza kumtegemea Bwana, majaribu hayatakosekana. Tumesikia jinsi Yesu mwenyewe alivyokuwa anajaribiwa na Shetani, wakati wa kukaa kwake siku arobaini jangwani, ili kujifunza kujitambua na kutambua mapenzi ya Mungu. Ni muhimu kwamba baada ya ubatizo katika mto Yordani, kabla ya kuanza kwa utume wake hadharani, Yesu anaenda jangwani kusali ili kuelewa jinsi ya kuishi kama Masiha, kulingana na mpango wa Baba. Injili ya Marko inaandika kwamba mara tu baada ya ubatizo, alikuwa ni Roho aliyempeleka jangwani. Jangwa kwa Yesu haikuwa kwamba ni jambo la ghafla tu lililojitokeza katika safari ya utume wake, bali ni Roho aliyemwongoza huko baada ya kuwa amesikia sauti ya Baba yake pale kwanye mto wa  Yordani: "wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu nimependezwa nawe” (Mk 1,11). Baada ya kupokea uteuzi huu kutoka kwa Mungu, Yesu anajaribiwa na yule mwovu na anabaki siku arobaini jangwani.

Kardinali Rugambwa wakati wa kuhubiri
Kardinali Rugambwa wakati wa kuhubiri

Majaribu yake matatu yanajumuisha majaribu yetu yote. Tusihofu mbele ya majaribu. Hayatoki kwa Mungu, bali hutoka kwa adui na yanatufikia kupitia mawazo, mawaidha, picha, shutuma, maneno na kadhalika. Yana nia ya kutufanya tuuwekee shaka upendo na uaminifu wa Mungu kwetu na hivyo kutuchochea kutokuwa na imani kwa Bwana, kutokuwa na imani na upendo wake. Tumwombe Kristo atufundishe kujibu mawazo hayo mabaya kwa kutumia Neno la Mungu, kama alivyofanya yeye mwenyewe, ili tuweze kudumisha uhakika wa upendo wa Mungu usio na mwisho katika maisha ya kila mmoja wetu. Ndugu zangu wapendwa Ninayo furaha kupokea wadhifa huu chini ya Bikira Maria wa Montesanto ambao Bwana amenipatia kwa matashi ya Baba Mtakatifu Papa wetu Fransisko ambaye ninamshukuru kwa dhati. Ninawashukuru nyote pia kwa sala zenu na makaribisho yenu mazuri. Uwepo wetu hapa leo unahamaishwa na sababu nyingine muhimu ya shukrani. Kikanisa, leo ni kumbukumbu ya kiliturujia ya Mwenyeheri Angelico, aliyekuwa msanii mkubwa na ambaye ni msimamizi na mwombezi wa wasanii. Kwa maombezi yake, napenda kumwombea kila mmoja wetu, ili siku zote tujibidiishe kuwa mashuhuda wa uzuri wa Mungu.

Kardinali Tagle alikuwa miongoni mwa walioshiriki katika misa ya kukabidhiwa Kanisa
Kardinali Tagle alikuwa miongoni mwa walioshiriki katika misa ya kukabidhiwa Kanisa

Kama ambavyo mnafahamu, sehemu kubwa ya utume wangu imekuwa katika kuratibu shughuli za uinjilishaji, na  uanzishaji wa makanisa mapya mahalia ulimwenguni. Papa Francisko alitaka niendelee na huduma hii, nikijitoa kabisa kwa kazi ya kutangaza Injili katika nchi yangu, Tanzania, na kumsaidia Baba Mtakatifu katika utume wa kiulimwengu, kama Kardinali. Baba Mtakatifu mwenyewe anatukumbusha katika waraka wake wa Evangelii gaudium ( Injili ya Furaha) na katika mkutano wake na wasanii mbalimbali siku chache zilizopita, ambako alisema kwamba uzuri unaong’aa katika sanaa ni mbinu fanisi muhimu ya uinjilishaji (via pulchritudinis! Kimsingi, “Kumtangaza Kristo maana yake ni kuonesha kuwa kumwamini na kumfuasa ni jambo ambalo licha ya kuwa la kweli na sahihi, bali pia ni la kuvutia [...]. Katika mtazamo huu, namna zote za kuonesha uhalisia wa uzuri wa kweli, zinaweza kutambulika kama njia zinayosaidia kukutana na Bwana Yesu” (rej.Evangelii Gaudium na.167).

Waamini wakiwa wamekaa katika Basilika ndogo ya Maria wa Montesanto
Waamini wakiwa wamekaa katika Basilika ndogo ya Maria wa Montesanto

Kwa sababu hiyo, Baba Mtakatifu Fransiko anaendele kutukumbusha kuwa: “Ni muhimu kwamba kila Kanisa mahalia likuze matumizi ya sanaa katika uinjilishaji, katika mwendelezo wa utajiri wa zamani, lakini pia katika utofauti na wingi wa namna zake za kisasa, ili kuirithisha imani katika lugha ya kisasa”. Watu wa nyakati hizi zetu wanahitaji kugundua tena uzuri halisi, unaong'aa katika uso wenye huruma wa Kristo Yesu mwokozi wa ulimwengu. Tafuteni daima uzuri huu, bila kukata tamaa na kuvunjika moyo, mkiendelea kutoa ushuhuda wa utafutaji huo kwa maisha yenu na kazi zenu za sanaa. Bikira Maria ambaye tunamheshimu hapa kama Mama wa Montesanto na kumshangilia katika kung'aa kwa Karmeli, atuombee kwa Mwanae sisi sote na wasanii wote! Ee Bwana wa uzuri, “utuwezeshe kuwasaidia watu wako kugundua uwepo wako kupitia sanaa zetu. Utuangaze kwa upendo na neema yako, ili sanaa iwe mabawa adhama ya kutuwezesha kupaa kuja kwako na kubaki nawe” Amina.

Jumuiya ya Watanzania wakati wa misa
Jumuiya ya Watanzania wakati wa misa

Ndugu msikizaji/ Msomaji, Mwisho mwa maadhimisho, baada ya kusainiwa kwa tendo, Msimamizi wa  Basilika  hiyo Monsinyo Walter Insero alionesha: “hisia na furaha ya jumuiya nzima.  Hata hivyo Dominika hiyo alisema: “ilikuwa siku ya kihistoria kwa Basilika yetu. Katika karne 4 za historia ya basilika hii, wewe ndiye Kardinali wa kwanza wa wadhifa huu,” Mkuu wa Kanisa hilo  alimwambia Kardinali Rugambwa,  huku  akizingatia juu ya  kupewa hadhi ya  kanisa hilo hadi  kuwa Basilika ya Kipapa  kwamba ni “ishara ya tahadhari na ubaba wa Papa Francisko.” Akiendelea alisema kuwa: “Katika adhimisho hili, ukatoliki, kwa hiyo ulimwengu wa Kanisa na roho ya kimisionari ilitetemeka ndani yetu. Sasa wewe ni Askofu na Kardinali mmisionari. Jimbo la Tabora ni kubwa kuliko Burundi na Uganda kwa pamoja.” Alisema Monsinyo Insero kwa kutaka kuelezea ukubwa wa Jimbo Kuu katoliki la Tabora.

Mapadre wakati wa Misa
Mapadre wakati wa Misa

Kanisa la Mtakatifu Maria wa Montesanto lilianzishwa kuwa Kanisa la Wasanii mnamo mwaka 1953 wakati mwanzilishi wake alipoanzisha na hivyo aliongeza: “Leo mapacha wamezaliwa kati ya jumuiya yetu na Jimbo lako.  Tutajipanga ili kuishi roho hii ya umisionari, na pia kwenda kumtembelea kwa sababu wote tumeitwa  katika hali ya kimisionari kuanzia lakini hapa.” Aidha alisisitiza jinsi ambavyo Kardinali Rugambwa alipochaguliwa na Papa, alimwambia kuwa hasiache kamwe kutabasamu, na hivyo wao wataendeleza hilo, kwa sababu ya furaha ya imani, ari na utamaduni wa Kanisa lake hasa kama walivyosikia hata nyimbo Kanisani za Lugha ya Kiswahili, na hivyo ilikuwa ni “tukio kubwa kusherekea naye.” Mkuu wa Kanisa hilo pia alihitimisha kwa kuwaomba  waamini wainuke kusali sala ya Wasanii ambayo, msanii mmoja alisali kwa sauti ya kisanii.

Tukuheshimu na Kukuabudu Ee Bwana Mungu
Tukuheshimu na Kukuabudu Ee Bwana Mungu

Sala ya Wasanii

“Ewe Bwana wa uzuri, Mwenyenyezi Muumba wa kila kitu, Wewe uliyeviumba viumbe kwa kuvitia alama ya ajabu ya utukufu wako, Wewe uliyemulika vilindi vya kila mwanadamu kwa nuru ya uso wako, tuelekeze macho yako na utuhurumie, juu ya udhaifu wetu, ya  umasikini  na elekeza macho yako kwenye kazi zetu, kwenye juhudi zetu za kila siku, utuangalie sisi ni wasanii, wasanii wako. Sisi ni wachoraji, wachongaji, wanamuziki, waigizaji, washairi, wacheza dansi, sisi ni watoto wako tunapenda kuishi kwenye mbawa za ushairi ili kuweza kuwa karibu na wewe, na kuwasaidia ndugu zetu kutazama juu zaidi katika ambingu  yako na ndani zaidi ndani ya mioyo yao.

Wakati wa Sadaka
Wakati wa Sadaka

Utusamehe kama sisi ni wadhaifu na wasio na msimamo, lakini tu wanadamu, utupe nguvu zako, tunachogundua katika Neno lako, kile tunachohisi katika neema yako, tunachopokea kutoka katika Ekaristi yako, kutoka katika mkate uliomegwa ambao ni ushirika, udugu na furaha. Tunakuomba kwa ajili yetu, kwa ajili ya wasanii wote, kwa ajili ya ulimwengu uliochanganyikiwa, ufanye tuwasaidie watu wote kugundua kitu kuhusu wewe, kupitia sanaa yetu. Maisha yetu yawe wimbo wa sifa kwa uzuri wako na kazi zetu miale ing'aayo inayoangazia njia za wanadamu. Utupe msamaha wako na ukarimu wako, utupe Roho yako ya hekima na uzuri, ututie moyo kwa upendo wako na neema yako, na utupe mbawa za ajabu ili kwa njia ya  sanaa tuinuke hadi kwako. Tunakuomba kwa njia ya Yesu Kristo, Bwana na kaka  yetu.”

Shangwe nje ya Kanisa na picha
Shangwe nje ya Kanisa na picha

Kardinali Protase, kabla ya Baraka ilitiwa saini, juu ya andiko la tukio lote, la kukabidhi Kanisa hilo kuanzia na: kubusu msalaba, kubariki waamini kwa maji ya baraka, kupiga magoti na sala, misa, mahubiri na maandishi hayo yalitiwa saini, na baadhi ya wana Parokia,makardinali waliokowapo, Kardinali Luis Antonio Gokim TagleMwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Kitengo cha Unjilishaji, Kardinali Robert SarahMwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, Kardinali Fernando Filoni, alyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji na sasa ni Mkuu wa Shirika la Ulinzi wa Kaburi Takatifu Yerusalemu, na baadhi ya maaskofu  na vile vile kuzawadia nakala ya picha iliyowekwa kwenye kikanisa kidogo. Ilifuatiwa  Baraka,wimbo wa mwisho wa “Tunaukimbia Ulinzi wako…”, ulioimbwa na Jumuiya ya Watanzania Roma.

Kardinali alipewa zawadi ya Picha ili aipeleke Tabora
Kardinali alipewa zawadi ya Picha ili aipeleke Tabora

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kuhusiana na tukio hilo la kukabidhiwa Kanisa la Mtakatifu Maria wa Montasanto la Kardinali Protase Rugambwa siyo jambo geni, hata kama watu wengi katika mitandao ya kijamii wamekuwa na maoni tofauti, hasa ya kutokuelewa ni nini maana yake. Wengi wao walifikiri kwamba tendo la kukabidhiwa Kanisa mjini Vatican ni kama vile anarudi tena huku Roma. Hapa ninataka kufafanua kwa ufupi kuhusu tendo hilo kwa kifupi. Kukabidhiwa Makanisa ya kwaida katika mji wa Roma ni desturi ya kale sana na inaonesha wazi kabisa juu ya uhusiano wa karibu kati ya Askofu wa Roma, ambaye ni  Papa, na makadinali wake ulimwenguni kote.

Wakati wa shangwe baada ya misa
Wakati wa shangwe baada ya misa

Kwa kawaida Kardinali hashiriki katika shughuli za kila siku za parokia hiyo anayokabidhiwa, wala hana mamlaka ya kuwateua hata wachungaji au kufanya maamuzi muhimu katika parokia. Kwa njia hiyo Parokia ya Roma, kwa maana nyingine ni kama  nyumba ya pili  kwa makadinali, ambao wanakaribishwa kila wakati kuadhimishwa Misa katika makanisa yao ya kawaida na kushughulikia mahitaji yao ya kiroho, kila mara wanapokuja Roma. Kwa upande wa Tanzania, hata Hayati Kardinali Laurean Rugambwa, alikuwa na Kanisa lake mjini Roma  lililoitwa Mtakatifu Francis wa Assisi huko Ripa Grande,jijini Roma na Kardinali Policarp Pengo Kanisa lake ni Mtakatifu Maria wa Salette,Roma.

Kardinali Rugamba akiwa na kundi la Watawa
Kardinali Rugamba akiwa na kundi la Watawa

Tukirudi katika Kanisa ambalo alipewa Kardinali Rugambwa, jina la Kanisa hilo linatokana na ukweli kwamba lilibadilisha na  kanisa dogo ambalo lilikuwa la mapadre wa Wakarmeli wa jimbo la Monte Santo huko Sicilia kisiwani Italia. Ujenzi ulianza mnamo 1662 kwa mpango wa Papa Alexander VII. Kufuatia kifo cha Papa mwaka 1667, kazi za ujenzi zilikatizwa na kisha kuanza tena, zilizofadhiliwa na Kardinali Girolamo Gastaldi kuzikwa huko, mwaka 1673 chini ya uongozi wa Carlo Fontana na usimamizi wa Bernini, hadi kukamilika kwa mapambo yote ya ndani mwaka 1679. Na ilikuwa mnamo Julai 1825 Papa Leo XII aliiinua hadi hadhi ya Basilika ndogo.

Kardinali Rugambwa akiwa katikati ya Waseminari
Kardinali Rugambwa akiwa katikati ya Waseminari

Na tangu 1953 Kanisa hilo limekuwa kiti cha “Misa ya Wasanii”, mpango wa umoja uliobuniwa mnamo 1941 na Ennio Francia; baada ya kubadilisha sehemu kadhaa za kuabudia, tukio la kiliturujia lilifanyika katika kanisa  kwenye Uwanja  wa Watu ( Piazza del Popolo) ambapo kila Dominika , kwa zaidi ya miongo sasa, adhimisho hili la Ekaristi Takatifu  linaadhimishwa ambapo wawakilishi wa ulimwengu wa utamaduni na sanaa hushiriki. Zaidi ya hayo, ni katika kanisa hilo ambapo mazishi ya watu wanaohusishwa na ulimwengu wa utamaduni na televisheni mara nyingi huadhimishwa. Na ndiyo sababu hizo kujuilikana sana kama “Kanisa la Wasanii.”  Katika kikanisa cha upande wa kulia kuna madhabahu ya Karamu ya Emmau (1982) iliyochorwa na Riccardo Tommasi Ferroni.

Misa kwa ajili ya kukabidhiwa Kanisa kwa Kardinali P.Rugambwa
19 February 2024, 15:07