Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya 110 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 2024
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Maadhimisho ya Siku ya 110 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani tarehe 29 Septemba 2024 yananogeshwa na kauli mbiu "Mungu hutembea na watu wake." Kaulimbiu hii ni kielelezo cha Mama Kanisa anayesafiri mintarafu wahamiaji na wakimbizi, hii ni picha makini ya Kanisa linalosafiri hapa Ulimwenguni. Hii ndiyo njia inayopaswa kutekelezwa mintarafu maadhimisho ya Sinodi, tayari kushinda vitisho na vikwazo vyote, ili kufikia nchi yetu ya kweli kwa pamoja. Wakati wa safari hii, popote ambapo watu wa Mungu wanajikuta, ni muhimu kutambua uwepo angavu wa Mwenyezi Mungu ambaye hutembea na watu wake, akiwahakikishia mwongozo na ulinzi Wake katika kila hatua. Lakini ni muhimu vile vile kutambua uwepo wa Kristo Yesu yaani, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, katika kila: mkimbizi na mhamiaji anayebisha hodi kwenye mlango wa mioyo yetu na kutoa fursa ya kukutana.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. LG 1. Chimbuko la Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ni kutokana na: mahangaiko pamoja na mateso ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kutokana na madhara makubwa ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Papa Pio X, kunako mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji duniani. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 ikaanza kusherehekewa na Kanisa la Kiulimwengu.
Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akawa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki kuanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, kama sehemu ya sera na mbinu mkakati wa Kanisa katika shughuli za kichungaji ili kusikiliza na kujibu kwa dhati kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii itaendelea kumwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso; mambo ambayo kimsingi yanasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tangu mwaka 1952, Siku hii ilikuwa ikiadhimishwa Dominika baada ya Sherehe ya Tokeo la Bwana. Lakini kunako mwaka 2018, Baba Mtakatifu Francisko baada ya kusikiliza maoni na kuridhia maombi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia akaamua kwamba, Siku hii iadhimishwe Dominika ya mwisho ya Mwezi Septemba na kwa mwaka huu, inaadhimishwa tarehe 29 Septemba 2024.