Papa amemteua Padre Gabriel Blamo Jubwe kuwa Askofu Mkuu wa Monrovia,Liberia
Na Angella Rwezaula - Vatican.
Baba Mtakatifu Jumatano tarehe 28 Februari 2024 amemteua kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Monrovia nchini (Liberia) Mheshimiwa sana Padre Gabriel Blamo Jubwe, wa Jimbo kuu hilo la Monrovia na ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni msimamizi wa jimbo Kuu hilo na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Pio.
Askofu Mkuu Mteule Gabriel Blamo Jubwe, alizaliwa tarehe 7 Septemba 1958 huko Lagos (Nigeria). Baada ya kumaliza majiundo yake katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo huko Gbarnga, Liberia, tarehe 18 Desemba 1983 alipewa Daraja Takatifu la Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Monrovia.
Nyadhifa
Alishika nyadhifa mbalimbali na kuendelea na masomo: nafasi za kichungaji katika Jimbo kuu (1983-1986); Shahada ya Uzamivu katika Liturujia, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Anselmo jijini Roma (1986-1991); Msimamizi wa Kanisa Kuu la Monrovia, Mkurugenzi wa Kituo cha Kichungaji cha Jimbo, Mjumbe wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Makanisa la Liberia na Baraza la Dini Mbalimbali la Liberia (1992-1996)
Gambera wa Seminari Ndogo ya Malkia wa Mitume na Seminari ya Maandalizi ya Mtakatifu Karoli Lwanga ya Monrovia (1996-1999); Paroko wa Kanisa Kuu la Jimbo Kuu la Monrovia (1996-2000); Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Liberia(1998-2001); mkurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa(1999-2004); Mkuu wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo huko Gbarnga(2001-2007); Mwanachama wa Baraza la Washauri la Jimbo Kuu la Monrovia(2006-2021).
Na ni mwandishi wa baadhi ya machapisho, pamoja na matangazo ya radio na ni mjumbe wa bodi mbalimbali. Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Pio X, tangu 2021 amekuwa Msimamizi wa Jimbo Kuu la Monrovia.