Papa amewateua Maaskofu wawili wasaidizi wa Jimbo Kuu katoliki la Nairobi Kenya
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Jumanne tarehe 13 Februari 2024 amewateua Maaskofu Wasaidizi wawili (2) wa Jimbo kuu Katoliki la Nairobi nchini (Kenya): Mheshimiwa sana Padre Simon Peter Kamomoe, wa Jimbo kuu hilo hilo, ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni Msimamizi wa Kanisa Kuu la Familia Takatifu, Nairobi, huku akimkabidhi kiti cha uwakilishi wa Tubune wa Numidia; Na Padre Wallace Ng'ang'a Gachihi, Jimbo hilo hilo ambaye hadi uteuzi huo alikuwa Paroko na Mratibu wa Huduma ya Kichungaji ya Jimbo kuu kwa kumpatia makao ya Tucca wa Mauritania.
Wasifu wa Padre Simon Peter Kamomoe
Askofu Mteule, Padre Simon Peter Kamomoe alizaliwa tarehe 26 Novemba 1962 huko Gatundu (wilaya ya Kiambu), katika Jimbo Kuu la Nairobi. Baada ya kuhudhuria Seminari Kuu ya Molo, alisoma Falasama katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustine ya Mabanga na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Matthias Mulumba huko Tindinyo.
Alipewa daraja la upadre mnamo tarehe 18 Juni 1994 kwa ajili ya Jimbo Kuu la Nairobi.
Nyadhifa nyingine
Alishikilia nyadhifa na kuendelea na masomo zaidi: Msaidizi katika Seminari ya Malkia wa Mitume jijini Nairobi(1994-1995); Msaidizi katika parokia za Thigio (1995), Mang'u (1995-1996), Ndundu (1996-1997), Mtakatifu Matthias Mulumba huko Thika (1997-1998); paroko wa Mama Yetu wa Fatima huko Kiriko (1998-1999); Paroko wa Mtakatifu Petro na Paulo huko Kiambu na wakati huo huo, Makamu wa Forane na Mjumbe wa Baraza la Washauri (1999-2008). Tangu 2008 amekuwa Msimamizi wa Kanisa Kuu la Familia Takatifu Nairobi na Msimamizi wa huduma ya kichungaji ya familia.
Wasifu wa Askofu Mteule, Padre Wallace Ng'ang'a Gachihi
Askofu Mteule Wallace Ng'ang'a Gachihi alizaliwa tarehe 26 Machi 1973 huko Gatundu (wilaya ya Kiambu), katika Jimbo Kuu la Nairobi. Baada ya Majiundo katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Maria huko Molo, aliendelea na Falsafa katika Seminiari Kuu ya Mabanga na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Matthias Mulumba huko Tindinyo.
Alipewa darala la Upadre mnamo tarehe 21 Mei 2005 kwa ajili ya Jimbo Kuu la Nairobi Kenya.
Nyadhifa nyingine
Alishikilia nyadhifa kadhaa na masomo zaidi: Kuwa Paroko msaidizi katika Parokia ya Watakatifu Petro na Paulo huko Kiambu (2005-2006); Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro na Paulo huko Kiambu (2006-2009); Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Taalimungu ya Kichungaji katika Chuo Kikuu Katoliki cha Afrika Mashariki-CUEA (2009-2011) na, wakati huo huo, kuwa Msaidizi wa Parokia ya Malkia wa Mbingu ya Karen (2009-2015); mnamo 2015 amekuwa Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme huko Embakasi na, tangu 2011, Mratibu wa Huduma ya Kichungaji Jimbo kuu. Yeye ni mwanachama wa Baraza la Washauri.