Ratiba ya maadhimisho ya kipapa mwezi Machi na inaanza na Dominika ya Matawi Machi 24
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kutoka katika Ofisi ya Mshereheshaji wa Liturujia ya Kipapa, Askofu Mkuu Diego Ravelli ametoa ratiba ya liturujia za kipapa kwa mwezi Machi 2024 kuanzia na Dominika tarehe 24 Machi ambayo ni Siku ya Matawi na kuanza kwa Juma Takatifu la Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. Katika siku hiyo kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican saa 10.00 kamili majira ya Italia, Baba Mtakatifu anatarajia kuadhimishwa misa kwa kuanza na maandamano ya kumbukumbu ya kuingia kwa Bwana huko Jerusalemu.
Alhamisi Kuu 28 Machi
Tarehe 28 Machi 2024 ni siku ya Alhamisi Kuu ya Juma Takatifu, ambapo katika Basilika ya Mtakatifu Petro itaona maadhimisho ya Misa Takatifu ya Misa ya Krisma asubuhi saa 3.30.
Ijumaa Takatifu 29 Machi
Na tarehe 29 Machi 2024 ni siku ya Ijumaa Kuu ya Mateso ya na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo katika Juma Kuu. Jioni ya saa 11.00 kamili inatarajiwa kufanyika maadhimisho ya Ibada ya Mateso ya Bwana Wetu Yesu Kristo Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.
Itafuatia usiku huo huo wa Ijumaa Njia ya Msalaba katika Magofu ya Kale ya Kirumi mahali ambapo wakristo wa kwanza waliteswa kwa kutetea imani yao (Colosseo) majira ya saa 3.15, usiku.
Jumamosi Kuu 30 Machi na mkesha
Jumamosi Kuu tarehe 30 Machi 2024 ndiyo mkesha wa Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambapo katika Basilika ya Mtakatifu Petro saa 1.30 usiku kutakuwa na Mkesha Mtakatifu wa Pasaka ili kuingia usiku mtakatifu wa Dominika ya Pasaka ya ufufuko wa Bwana.
Dominika 31 Machi ni Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo
Tarehe 31 Machi, ndiyo siku ya Dominika ya Pasaka ya Ufufuko wa Bwana ambapo katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, saa 4.00 kamili asubuhi, misa Takatifu ya ufufuko wa Bwana itaadhimishwa na kufuatia saa 6 kamili mchana Baraka ya Urbi et Orbi.