Tafuta

2024.02.07 Czerny Sudan KUSINI 2024.02.07 Czerny Sudan KUSINI 

Sudan Kusini,Czerny:matinki ya ugomvi tunapoteza ubinadamu wetu

Katika Misa Takatifu huko Malakal kwenye fursa ya Siku kuu ya Mtakatifu Giuseppina Bakhita,Sanjari na Siku ya Kimataifa ya sala na Tafakari dhidi ya biashara haramu ya binadamu,Kardinali Czerny ameonya juu ya miungu ya uongo:uchu,madaraka,kumiliki,utaifa ambao unapelekea kuharibu wengine.Katika misa hiyo amewaweka wakfu mashemasi watatu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kardinali Michael Czerny S.J. Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Huduma ya Maendeleo ya Fungamani ya Binadamu akiwa huko Malakal Nchini, Sudan Kusini, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Siku Kuu ya Mtakatifu Josephine Bakhita, sanjari na Siku ya Kimataifa ya sala na Tafakari dhidi ya biashara haramu ya binadamu, tarehe 8 Februari 2024. Kardinali Czerny amekuwa Nchini humo tangu tarehe 2 Februari na atarudi tarehe 9 Februari 2024 katika fursa ya kuadhimisha Mwaka mmoja tangu Papa Francisko alipotembelea nchi hiyo kuanzia tarehe 3-5 Februari 2023. Katika mahubiri yake amesema siku hizi, tunatambua kumbukumbu ya ziara ya Mtakatifu Papa Francisko nchini Sudan Kusini, katika hija na wenzake wawili kutoka Uingereza, ambao walikuja kuleta ujumbe wa amani. Mbegu ya amani ilipandwa; ni wajibu wetu kuifanya ikue. “Leo, tunamshukuru Mungu kwa wachungaji anaoendelea kuwatuma, tukianza na Kardinali mpya wa Sudan Kusini ndugu yangu Stephen Ameyu Martin Mulla wa Juba, pamoja na maaskofu, mapadre, mashemasi na wahudumu wote wa Injili hapa nchini.”

Hisitoria ya Mtakatifu Bakhita

Kwa namna ya pekee, Kardinali Czerny amemshukuru Mungu siku hiyo  kwa ajili ya ndugu  watatu hapa ambao walikaribia kuwekwa wakfu wa Ushemasi. Katika roho hii ya shukrani, alisema walikuwa wakiadhimisha pia Sherehe ya Mtakatifu Josephine Bakhita. Kardinali Czerny alisisitiza kuwa Mtakatifu huyo anapendwa sana hapo Malakal, Sudan Kusini na kwingineko, nchini Sudan na katika ulimwengu wote wa Kikatoliki. Yeye ndiye Mtakatifu mlinzi, msimamizi wa Waathiriwa wa Biashara Haramu ya Binadamu. Kwa kuunganishwa na historia yake, siku hii pia imeteuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Maombi na Tafakari kwa ajili ya Waathiriwa wa biashara haramu ya binadamu. Na tunajua kwamba Mtakatifu Josephine Bakhita aliteseka sana maishani mwake.

Akiwa mtoto, alitekwa nyara na kulazimishwa kutembea mamia ya kilomita ili kuuzwa kama mtumwa. Wakati wa safari ya kwenda El Obeid, alinunuliwa na kuuzwa mara mbili. Na baada ya El Obeid, aliuzwa mara nyingi, akikaa miaka mingi katika utumwa ulio na unyanyasaji na ugumu wa maisha. Hata hivyo, historia ya Mtakatifu Josephine Bakhita ni historia ya matumaini, kutoka utumwani hadi hatimaye kujifunza juu ya Mungu katika nyumba ya watawa. Hatimaye, alipoachiliwa, alichagua maisha ya kujitolea kamili kwa Mungu na kuingia katika maisha ya kitawa. Kama mtawa, alishiriki historia yake ya utumwa, akiwashukuru watekaji nyara wake, kwani bila wao labda hasingemjua Yesu, na wala Kanisa. Licha ya mateso yake, na hata baadaye licha ya ugonjwa aliovumilia, aliendelea kuwa mchangamfu, akifuata daima shauku za Bwana wake Yesu Kristo. Katika haya yote, Mtakatifu Josephine Bakhita anatupatia mfano mzito wa kuwa na matumaini hata katika hali ngumu.”

Papa Francisko: 'hii ni fursa ya Bakhita'

Tarehe 11 Oktoba 2023, Baba Mtakatifu Francisko alitoa hotuba yake, katika Katekesi ya  kila Jumatano kuhusu maisha na ushuhuda wa Mtakatifu Josephine Bakhita. Alisema: “Hii ni nafsi ya Bakhita. Kiukweli, kuhurumia kunamaanisha kuteseka pamoja na waathiriwa wa ukatili mkubwa ulimwenguni na pia kuwahurumia wale wanaofanya makosa na dhuluma, sio kuhalalisha, lakini ubinadamu. Haya ndiyo mabembelezo anayotufundisha: kufanya ubinadamu.” Kardinali Czerny aliendelea kusema kuwa: “Tunapoingia kwenye mantiki ya kupigana, ya mgawanyiko kati yetu, ya hisia mbaya, moja dhidi ya mwingine, tunapoteza ubinadamu wetu. Na mara nyingi sana tunafikiri tunahitaji ubinadamu, kuwa na utu zaidi. Na hii ndiyo kazi ambayo Mtakatifu Bakhita anatufundisha: kufanya ubinadamu, kujifanya kuwa binadamu na kuwafanya wengine kuwa binadamu.” Tukigeukia sasa Sudan Kusini ya leo, kila mahali unahitaji kuwa makini sana, ili kubaki waaminifu kwa Mungu wa Yesu Kristo, ambaye ni Mungu wa amani, Mungu wa Upendo, Mungu wa msamaha, Mungu wa upatanisho Mungu wa hali njema na Mungu wa wema wa kweli na furaha ya kweli.”

Miungu ya madaraka na  ukabila inaua 

Kardinali akijikita katika masomo ya siku alisema katika somo la kwanza, kutoka kwa 1 Wafalme(11:4-13), tunasikia kwamba Sulemani, mtu ambaye alipaswa kuwa na hekima, alifuata mfano wa baadhi ya wake zake na kuugeuza moyo wake kutoka kwa Mungu wa Baba zake aliabudu miungu ya uwongo ya wake zake. Akichukua hatua hata zaidi kutoka katika ibada ya kweli, Sulemani alijenga madhabahu kwa miungu ya wake zake. Mungu alichukizwa na kumfunulia Sulemani matokeo ya ibada yake ya miungu. Vishawishi vya kuabudu miungu vinaendelea leo. Miungu ya uwongo ya leo, ambayo inatuzuia tusifuate Mungu wetu na Bwana Yesu Kristo, ni tofauti na ile ya siku za Sulemani, lakini ni hatari sana, nayo inakuja kwa namna tofauti-tofauti na kwa majina tofauti, kama vile: Mungu wa tamaa ya mali/fedha, ambayo hutufanya kuwanyima wengine manufaa ya kawaida; ambapo rasilimali zinazokusudiwa watu wengi zinatumiwa na wachache tu, au hata na mmoja. Ni kama kama ifuatavyo: Mungu wa njaa ya mamlaka, udhibiti na utawala, sio tu katika ngazi ya kitaifa lakini hata ndani ya jumuiya zetu za mitaa, vijiji na ngazi zote za shirika la kibinadamu. Mungu wa ukabila au utaifa, ambao unatusukuma kuwatenga wengine na kuwachukulia kama watu wa chini, au hata kuwaua, kama baadhi yenu mmeshuhudia.”

Miungu ya uongo imeharibu Sudan

Miungu hii ya uwongo imeharibu sana Sudan Kusini, na ni wakati wa kuinuka na kuishutumu. Baba Mtakatifu Francisko alipofika Sudan Kusini, “aliongozwa na Roho Mtakatifu kuwakumbusha watu wote wa nchi hiyo kwamba Mungu anawaita wote kutembea katika njia ya amani. Uwepo wake na maneno yake yalichochea moto wa bidii, akawasha hapa moto. Aliwasha roho inayopelekea Sudan Kusini kujulikana kwa amani na sio vita. Kila mtu nchini Sudan Kusini ana wajibu wa kudumisha moto huo, wajibu wa kuwasha moto huo katika maisha na mioyo ya wengine”. Papa Francisko alikwenda kati yao kama mtumishi wa Injili. Ziara yake iliashiria mwanzo mpya nchini Sudan Kusini. Kwa hiyo wana wajibu wa kufuata mfano wake. “Leo, tukipigana, tupiganie amani na umoja kama familia moja iliyobarikiwa ya Mungu, kama ndugu wote.” Kardinali ameongeza kusema kuwa “Katika maneno ya Somo la Pili leo, “Nyinyi nyote mmekuwa wana [na binti] wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu, kwa maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hakuna Myahudi wala Mgiriki, mtumwa wala huru, mwanamume wala mwanamke, kwa maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu (Wagalatia 3:26-28).”

Umoja ni silaha

“Umoja ni silaha tuliyo nayo ya kupigana na chochote kinachotutenganisha na kutuondolea amani,” alisisitiza Kardinali. Umoja ni ulinzi wetu dhidi ya yote yanayotishia amani hapa Sudan Kusini. Yesu alipokataliwa na viongozi wa kidini wa siku zake, nyakati fulani alirudi katika nchi ya wageni, ambako walimkaribisha na hata kumtafuta ili awasaidie. Tunao mfano wa hili katika Injili ya leo. “Mwanamke Mgiriki alimwomba Yesu amponye binti yake. Imani yake katika Yesu ilikuwa yenye nguvu sana hivi kwamba, hata Yesu alipompinga akisema, “si sawa kutwaa mkate wa watoto na kuwatupia mbwa,” mwanamke huyo aliweza kudumu katika sala yake ya kuomba msaada. Mwanamke huyo alielewa vya kutosha kwamba Yesu hakuwa akimlinganisha na mbwa, badala yake alikuwa akimpatia nafasi ya kueleza imani yake hata kwa mkazo zaidi. Licha ya kile kinachoweza kuonekana kuwa hivyo juu ya uso, alikuwa akimulika ubinadamu wake. Mazungumzo yake pamoja naye yalikuwa ushuhuda wa heshima ya Yesu kwake na yangeshtua Wayahudi wenzake wengi. Mara nyingi watu wa siku za Yesu waliwabagua wageni, Watu wa Mataifa, na kuwaona kuwa watu wasio safi. Walimwita Yesu mwenye dhambi kwa kufanya urafiki nao. Lakini Yesu aliwajumuisha watu wa mataifa mengine katika huduma yake ili kuwaonesha Wayahudi wenzake kwamba watu wa mataifa mengine pia wana nafasi katika Ufalme wa Mungu. Yeyote tunayemwona kuwa mgeni anaalikwa kwenye Ufalme kama sisi tulivyo.”

Kwa Mashemasi 3 wapya

Kardinali Czerny akiwageukia mashemasi wapya alisema: “Ndugu wapendwa Mikaeli, Emmanuel na Mathayo: kwa kuwekewa mikono na sala ya kuwekwa wakfu, mtawekwa wakfu kwa huduma takatifu ya ushemasi, mnaitwa kujenga ustaarabu wa upendo na amani duniani leo. Mtafanya hivyo kwa kumwiga Yesu Kristo, Bwana ambaye alikuja, si kutumikiwa, bali kutumikia. Huduma yenu inapaswa kukazia kwake yeye, mkiepuka kila aina ya ubatili ambayo inaweza kuwakengeusha. Hii ina maana ya kuepuka kila aina ya uroho, njaa ya madaraka, mali, ukabila au hata utaifa usiofaa. Kukabiliana na magumu ya zama zetu, ni lazima uzungumze juu ya Yesu, umshuhudie Yesu, kwa matumaini, uchangamfu na furaha, hasa mnapokutana na maskini na wanaoteseka. Kwa kuzingatia haya, na mengine, changamoto maalum ambazo mtakutana nazo katika maisha na huduma yenu yote, ninawaelekeza kwa ahadi mtakazoweka tunapoadhimisha Ibada hii ya kuwekwa wakfu kuwa mashemasi. Alieleza jinsi ambavyo angewauliza maswali kadhaa, ambayo yanaelezea majukumu mapya ambayo waaaanza mara moja. La kwanza linahusu kujitolea kwao kutekeleza shughuli za shemasi kwa unyenyekevu na upendo, kusaidia askofu na mapadre na kuwatumikia watu wa Mungu. Jambo la pili ni kushika fumbo la imani kwa dhamiri safi, kama Mtume anavyohimiza, na kuitangaza imani hii kwa maneno na matendo kama inavyofundishwa na Injili na mapokeo ya Kanisa.”

Kudumia na kuimarisha roho ya sala na mtindo wa maisha

Tatu ni kudumisha na kuimarisha roho ya sala inayolingana na mtindo wao wa maisha na, kulingana na kile kinachohitajika kwao, kuadhimisha kwa uaminifu liturujia ya saa kwa Kanisa na kwa ulimwengu wote. Wametafakari juu ya maswali haya na wamealikwa kuyajibu kwa sauti ya msisisitiza: “Ndiyo nitafanya.” Kwa kutambua umuhimu wa adhimisho la Ekaristi Takatifu katika maisha ya Kanisa, na katika maisha ya Mashemasi, Ibada hiyo pia inawaasa kutengeneza mtindo wao wa maisha daima kufuatana na kielelezo cha Kristo, ambaye mwili wake na damu yake ililimwagika kwa ajili ya watu. Hatimaye, kwa njia ya kweli kabisa, ahadi zote hizi zinatokana na ahadi yao ya heshima na utii kwa Askofu Mahalia na waandamizi wake.”

Kardinali aliendelea kusema “ Ndugu wapendwa Michael, Emmanuel na Mathayo, jambo la kawaida katika sala na ibada leo, utambulisho wa shemasi, ni huduma. Ushemasi ni huduma ya huduma inayohitaji ukaribu na Kristo, Askofu na mapadre, mashemasi na watu wa Mungu, hasa maskini na wanaoteseka. Ninakumbuka tena hotuba ya Papa Francisko kwenye katekesi ya tarehe 11 Oktoba 2023 kuhusu Mtakatifu Josephine Bakhita. Alibainisha njia ambayo aliona huduma.” Kwa kukazia Kardinali Papa alisema: “Bakhita aliweza kupata huduma, si kama utumwa, lakini kama maonesho ya zawadi ya bure ya kujitegemea.” Kwa hili na kwa njia nyingi sana, amewaalika wajifunze kutoka kwa mtakatifu huyo mkuu anayetokea sehemu hii ya dunia.”

Kwa Askofu mapadre na mashemasi

Kardinali akiwageukia Askofu/mapadre na mashemasi: wamewakwa wakfu kuwa watangazaji wa Injili. Wameitwa kuwaonesha watu njia ya Yesu Kristo, njia ya Mungu, njia ya utimilifu wa uzima (Yohana 10:10). Wakilegea katika jukumu hili, wakisitasita katika huduma hii, miungu mibaya ya uwongo itajaribu kudai watu wa Mungu na kuwapoteza. Wananchi wakipotoka, matatizo ya nchi hii yataendelea bila kupingwa na kutatuliwa. Kardinalia maesema kuwa wao wana wajibu mkubwa wa kila shemasi, kushiriki Habari Njema na kuwahudumia maskini na wahitaji. Kwa hiyo, amewaomba kuwaombee hawa watu watatu wanapopokea Sakramenti kuu ya Daraja Takatifu na kukubali majukumu yao mapya ya kichungaji. Na pamoja na Baba yetu Mtakatifu, Papa Francisko, tuombe ili sote tuwe kitu kimoja katika Kristo Yesu. Kwa maana umoja na maridhiano ni njia ya amani ya kudumu nchini Sudan Kusini.”

Mahubiri ya Kardinali Czerny katika fursa ya Siku Kuu ya Mt.Bakhita huko Malakal,Sudan Kusini
08 February 2024, 10:04