Ufilippino,Fisichella:Mimi nipo pamoja nawe;nitakulinda popote uendeko!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Askofu Mkuu Rino Fisichella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji kwa ajili ya Masuala Msingi wa Uinjilishaji duniani, ametoa mahubiri yake katika Misa Takatifu ya Shukrani katika Kanisa Kuu katika fursa ya kutangaza Jina la: “Madhabahu ya Kimataifa ya Mama Yetu wa Amani na ya Safari Njema” katika Mji wa Antipolo nchini Ufilippino Jumatatu tarehe 26 Februari 2024, saa 4.00 kamili, masaa ya Ufilipino ikiwa ni saa 9.00 usiku wa manane wa Ulaya. Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu Fisichella alisema kabla ya kufanya baadhi ya Tafakari kuhusu Neno la Mungu ambalo lilisikika, awali aliomba aruhusiwe kueleza maneno ya shukrani. Kwa njia hiyo kwanza Kaka yake Askofu wa Kanisa hilo la Antipolo, Mwashamu Askofu Ruperto Santos, kwa mwaliko wake alioutoa kwake katika fursa nyingi, ili kwamba aweze kuwa hapo katika maadhimisho. Kanisa mahalia ikiwa ni wajibu wa kuwa na Madhabahu katika ardhi yao ya Mama yetu wa Amani na Safari njema ambayo imefanywa kuwa Madhabahu ya kimataifa.
Uwepo wa madhabahu kama hiyo ni ishara ya neema ambayo inawaalika kila mmoja kuwa na imani ya kina. Askofu Mkuu akiendelea alipanua salamu zake kwa wawakilishi wa Baba Mtakatifu, hasa kwa Balozi wa Vatican nchini humo, Askofu Mkuu Charles John Brown, ambaye kwa neema amempokea na ambaye amebeba utume katika Kanisa la Ufilippino kwa kujitolea sana. Vile vile salamu za dhati, ziliwaendea maaskofu waliokuwapo, Mapadre, Mashemasi, na waseminari, watawa, viongozi wa kiraia ambao walishiriki katika wakati huo wa sherehe na wa sala; kwa wote, kaka na dada, na ni pamoja na kuwapatia salamu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye amemwamini na kumtuma awepelekee baraka kwa wote na kuwaomba pia wasali kwa ajili yake.
Askofu Mkuu Fisichella akianza kudadavua masomo yaliyochaguliwa katika fursa ya sherehe hiyo alisema kuwa “kama walivyosikia Neno la Mungu linaliakisi maisha ya kila mmoja wao na hasa kuleta mwanga wa kipekee katika adhimisho la Ekaristi walilokuwa wakiadhimisha. Tuko ndani ya Madhabahu iliyowekwa wakfu kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu anayetuombea kabla ya yote, ili amani itawale duniani kote na katika nyumba zetu. Ikiwa amani na utulivu tu vinapatikana katika familia zetu, ndipo tunaweza kutumaini kwamba itakuwepo katika ulimwengu wote licha ya jeuri ya watu ambayo daima inasababishwa waathiriwa wasio na hatia. Kwa njia hiyo, amesisitiza kwamba kwa “namna ya pekee walikuwa hapo kwa ajili ya kuomba amani kwa ajili ya maeneo hayo yote ya ulimwengu ambapo watu wanateseka isivyo haki kwa sababu ya kutawaliwa na jeuri ya vita. Vita duniani kote ni uso wa kutisha wa dhambi; ni usemi wa wale wanaomwacha Mungu na kutoisikiliza sauti yake”.
Kwa kuendelea alikumbusha kuwa maneno ya “Zaburi ambayo yalionesha huzuni fulani, isemayo kuwa “Ninapozungumzia amani, wao ni kwa vita,” kiukweli, alisema mawazo ya Mungu si yetu wenyewe; kila tunapomwacha, mitaani hujaa hofu, vurugu na vita. Na lilisikika tatangazo linalosaidia kuwa na tumaini. Sisi ni “Mahujaji wa Matumaini katika ulimwengu huu.” Kwetu sote ni wajibu wa kuwa si tu watangazaji wa tumaini la Kikristo, bali zaidi ya yote wajenzi wa tumaini, tukitengeneza ishara thabiti zinazotoa uaminifu kwa maneno yetu. Kama katika Kitabu cha ufunguzi cha Biblia, Mwanzo, katika Patakatifu hapa kuna ngazi inayopanda kwa Mungu. “
Askofu Mkuu alisema kuwa “Anayetusindikiza katika kupaa huko mbinguni ni Bikira Maria. Yeye ambaye pale msalabani aliagizwa na Yesu kumtunza kila mmoja kana kwamba sisi ni watoto wake, na ndivyo tulivyo.” Basi Askofu Mkuu aliwaomba “wafunge mioyo yao; na wakaze macho yao juu ya uso wake; watazamwe na yeye ambaye kwa upendo wa Mama hawezi kuwaacha. Hakuna haja ya kuongeza maneno yetu; tayari anajua tunachohitaji. “ “Tunahitaji kuamini msaada wake tu na kuwa na hakika kwamba ukaribu wake na kushiriki kwake havitakosekana kamwe. Tukiwa na furaha, Yeye hufurahi pamoja nasi; tukiteseka, Yeye anateseka pamoja nasi; tukishughulikia maombi yetu, Yeye hutuombea kujibiwa. Ni ujasiri na faraja kiasi gani maneno tuliyoyasikia yanaleta, “Ujue mimi nipo pamoja nawe; nitakulinda popote uendako; sitakuacha kamwe...” Mungu hatotuacha kamwe.
Katika hali yoyote tunayoweza kujikuta anabaki karibu nasi. Maria alisimama karibu na msalaba Yesu alipoteseka na kufa.” Moyo wa Mama yake, hata hivyo, ulikuwa na hakika kwamba maneno ya Mwanawe yangetimizwa: “Baada ya siku tatu nitafufuka.” Ni tumaini kiasi gani Maria lazima alikuwa na moyoni mwake katika siku hizo tatu. Ndani yake kulikuwa na nyakati za kupishana za huzuni na huzuni nyingi, lakini pia zikiambatana na tumaini la ufufuko. Mama wa Mungu anarudia vivyo hivyo kwa kila mmoja wetu hapa leo katika kaburi lake, ambapo ikoni inang'aa kwa uzuri wake wote na kukusanya sala za mamilioni ya waamini wanaokuja kwake kusali na kufarijiwa. Je, tunaweza kupata maneno yenye nguvu na kusadikisha zaidi kuliko haya ambayo Mungu Mwenyewe anatuambia leo? Atakuwa nasi milele; Baba wa Yesu Kristo hatutupi kamwe. Ujumbe unaotoka katika hekalu la Antipolo unakuwa ujumbe wa kweli wa amani kwa sababu unatuhakikishia kuwapo kwa Mungu na ukaribu wake milele katika maisha yetu. Yeyote anayepitia ukaribu wa Mungu anakuwa chombo cha ukaribu kwa wale wanaohitaji.”
Kuna matokeo ya lazima kwa wale wanaohiji kwenye Madhabahu: uzoefu wa neema inayoishi hapa unahitaji kuwasilishwa na kupitishwa kwa wengine. Hatuishi kwa ajili yetu wenyewe, bali sisi ni waeneza injili daima. Mhujaji katika Madhabahu ya Mama Yetu wa Amani na Safari Njema anajua kwamba hawezi kuondoka bila kuchukua pamoja naye ujumbe wa amani ambao Mama wa Mungu amempatia. Hakika ni ujumbe kwa ajili yake mwenyewe, lakini pia unakuwa wajibu kwa ajili yake kuwa pamoja. Hija katika Madhabahu ya Kimataifa ina dhamira ya kuwaunganisha Wakristo kiroho na waamini wote waliotawanyika duniani kote. Kuwa mahali patakatifu pa kimataifa sio tu fursa ambayo inatolewa, lakini utume ambao lazima ushirikishwe.”
Kama andiko lililotiwa saini kuthibitisha madhabahi hiyo linavyosema kuwa: “watu waamini wa Ufilipino wameona katika Madhabahu ya Kitaifa ya Antipolo Mama Yetu wa Amani na Safari Njema kuwa chanzo kisichoisha cha msukumo na, katika shule ya Bikira Maria anakwenda kumtembelea Elizabeth, tangazo la amani ya Masiha, wanaendelea na safari yao ya kushikamana na imani na ushuhuda wa Kikristo.” Kwa hiyo, “Madhabahu ya Kimataifa ya Mama Yetu wa Amani na Safari njema” yamefunguliwa kwa dhamira ya kutokuwa na mipaka, lakini badala yake inafungua milango yake kwa ajili ya kuwakaribisha wote, hasa maskini zaidi na wale wanaohitaji faraja na amani.
Askofu Mkuu Rino alisisitiza kuwa "Leo Bikira Maria anarudia kwa kila mmoja wetu maneno yale yale aliyoyasikia Yakobo, “Jueni ya kuwa mimi ni pamoja nanyi; nitakulinda popote uendapo; Sitakuacha kamwe....” Kwa kila mmoja wetu, pia, ni muhimu kupanda ngazi inayoelekea mbinguni ili kuishi kwa utimilifu uzima wa milele ambao tulipewa siku ya ubatizo wetu na. ambao kila siku tuna jukumu la kuwashirikisha kaka na dada zetu wanaofika kwenye Madhabahu hii. Kwa hiyo, nyumba hii ya Mungu na iwe mahali ambapo: imani inakuwa na nguvu zaidi kwa sababu ya sala isiyokoma inayokwenda kwa Baba kwa maombezi ya Bikira Maria; tumaini linaimarishwa kwa sababu ya safari tunayopaswa kufanya hadi lengo la mwisho lifikiwe; upendo huishi kwa wingi wa moyo katika kutambua ainambalimbali za huruma ambazo Bwana ametuachia.” Alihitimisha."