Umuhimu wa Majiundo Endelevu Kwa Maisha na Utume wa Mapadre: Liturujia ya Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kuanzia tarehe 6 Februari hadi tarehe 10 Februari 2024 linaadhimisha Mkutano wake wa Mwaka kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Nendeni, mkatuandalie Pasaka tupate kuila” na kwa Lugha ya Kilatini “Euntes parate nobis Pascha” Lk 22:8. Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa majiundo endelevu kwa Makleri na Waamini walei, ambao hapo tarehe 8 Februari 2024 watakutana na Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni muda muafaka kwa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kujadiliana kuhusu: fursa, matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika majiundo ya Liturujia katika Kanisa kwa sasa. Hii ni fursa ya kutafakari kuhusu Katiba ya Liturujia ya Kanisa, kama inavyobainishwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati yake ya “Sacrosanctum Concilium” yaani kuhusu Liturujia ya Kanisa. Hii ni hati inayojadili pamoja na mambo mengine kuhusu: Kanuni za jumla za marekebisho na ukuzaji wa Liturujia Takatifu; Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sakramenti nyingine na Visakramenti; Liturujia ya Vipindi vya Kanisa, Mwaka wa Liturujia ya Kanisa, Muziki Mtakatifu; Sanaa Takatifu na Vifaa Vitakatifu pamoja na nyongeza. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanahimiza malezi ya Kiliturujia na ushiriki hai wa waamini katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa kuzingatia marekebisho ya Liturujia Takatifu. Rej. SC, 16. Sanjari na kuendeleza malezi na majiundo endelevu kwa Wakleri pamoja na waamini walei. Rej. SC 16. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafafanua nafasi ya Liturujia katika fumbo la Kanisa kwa kusema kwamba, maana kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu.” Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waoneshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo Yesu na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli.
Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana lakini lenye mambo yasiyoonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye kuhiji. Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya kimungu, yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo yaelekee mji ujao tunakoelekea. Hivyo Liturujia kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa wawe hekalu takatifu la Bwana, makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo. Wakati huohuo kwa namna ya ajabu Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumhubiri na kumshuhudia Kristo Yesu; na kwa njia hiyo inawaonesha wale walio nje [nalo,] Kanisa lililo ishara iliyoinuliwa juu kati ya mataifa, ambayo chini yake watoto wa Mungu waliotawanyika wakusanyika katika umoja mpaka liwepo zizi moja chini ya mchungaji mmoja. Rej. SC, 2. Yote haya ni mambo yanayohitaji majiundo endelevu ya Liturujia ya Kanisa. Kongamano hili litawasaidia Maaskofu kukuza na kudumisha mpango mkakati wa shughuli za kitume na kichungaji, lengo ni kumwilisha mapendekezo haya kwa Makanisa mahalia. Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lilijadiliwa katika mkutano wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, likapelekwa kwa Baba Mtakatifu na hatimaye, akaridhia lichapwe kwa kuweka saini yake tarehe 18 Desemba 2023. Tamko hili linajadili kwa kina na mapana kuhusu: Baraka katika Sakramenti ya Ndoa, Maana ya baraka katika Maandiko Matakatifu, Uelewa wa baraka kitaalimungu na kichungaji, nani anaweza kuomba baraka. Baraka kwa watu wenye “ndoa tenge” na watu wa ndoa za jinsia moja. Kanisa ni Sakramenti ya upendo wa Mungu.
Watu wa Mungu wenye imani thabiti wanaweza kupokea baraka za Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa na kwamba, Kristo Yesu ni kielelezo cha baraka kuu kutoka kwa Mungu, baraka ambayo ni chemchemi ya wokovu. Baraka katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu: Kiini cha ndoa ya Kikristo ni maagano baina ya mume na mke au ukubaliano wao wa hiari usiotanguka. Muungano huo wa mume na mke na manufaa ya watoto wao huwataka wawe na uaminifu kamili kati yao. Kwa asili yake ndoa na mapendo ya wenye ndoa yamewekwa kwa ajili ya kuzaa watoto na kuwalea; nao ni taji yao. Kwa kweli watoto ni zawadi kuu ya Ndoa na tunu kubwa ya wazazi wenyewe. Haya ndiyo Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Ndoa na kamwe hayawezi kubadilishwa. Wakati wa kutoa baraka, Kanisa lina wajibu na dhamana ya kuhakikisha kwamba halichanganyi madhehebu ya kutoa baraka, ili kusitokee mkanganyiko na kwamba, Kanisa halina mamlaka ya kutoa baraka kwa watu wa ndoa za jinsia moja. Mama Kanisa anatamani sana waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya Kiliturujia kwa utimilifu, kwa ufahamu na utendaji. Jambo hili linadaiwa na tabia ya Kiliturujia yenyewe na pia kwa sababu ya Ubatizo, ni haki na wajibu wa Wakristo ambao ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu. Liturujia ni chemchemi ya kwanza na ya lazima ambayo toka kwake waamini wanaweza kuchota roho kweli ya kikristo. Kwa hiyo wachungaji wa roho katika kazi zao zote za kitume, wanapaswa kushughulikia bila kukoma kwa njia ya mafundisho yafaayo! Kumbe, maadhimisho ya Mkutano huu mkuu ni muda muafaka wa kusali na kutafakari; kuchambua na kupembua pamoja na kujadiliana katika makundi madogo madogo “Circul minores.”
Akichangia hoja, Kardinali Lazzaro You Heung-sik, “Yu Hung Shik” Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makleri, amekazia umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza katika malezi na majiundo ya Kipadre, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo pamoja na kupokea fursa zinazojitokeza, ili hatimaye, kutekeleza dhamana na nyajibu zao kwa moyo wa furaha. Kanisa lina Mapadre wema, watakatifu na watenda kazi hodari, lakini pia kwa upande mwingine, wamo waliojichokea na kujikatia tamaa kutokana na changamoto za maisha na utume wa Kipadre. Kumbe, kuna haja ya kuwasaidia Mapadre kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa kuwapatia kwanza kabisa mahitaji yao msingi. Kumbe, kila mshiriki kwenye majiundo haya analo jambo la kuchangia, ili kweli Mapadre waweze kupata malezi na majiundo bora zaidi. Majiundo ya Kiliturujia ni kati ya changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa kwa sasa kadiri ya tafiti zilizofanywa!
Kwa upande wake, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu amekazia umuhimu wa malezi na majiundo endelevu katika maisha na utume wa Mapadre: kwa kujikita katika: masomo, maisha ya sala, nidhamu na maisha ya kiroho, ili kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa Mungu, Kanisa na watu wake. “Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.” Mdo 20:28-29. Majiundo endelevu yanawataka Mapadre kujitunza kwanza wao wenyewe sanjari na kusimama kidete kulinda imani yao! Huu ni mwaliko wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ili mchakato wa Uinjilishaji uweze kutoa mwanga kwa changamoto mamboleo kuhusiana na Mungu, wengine pamoja na tunu msingi za Kiinjili. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, ameonya kuhusu ukabila na utaifa usiokuwa na mashiko, ustawi na maendeleo kwa Kanisa na kwamba, watu wote wa Mungu wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kujenga na kudumisha ushirika kati yao, hali inayohitaji toba, wongofu wa ndani ili kuwa kweli mashuhuda na vyombo vya ushirika na umoja wa Kanisa. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle amewapongeza Makleri wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa maamuzi mbele, vita, ubaguzi, nyanyaso za kijinsia, wakimbizi na wahamiaji pamoja na waathirika wa mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Kumbe, malezi na majiundo endelevu yasaidie kuganga na kuponya madonda ya ukatili ambayo yanaweza kugeuka na kuwa ni chanzo cha kulipiza kisasi, chuki na uhasama! “Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.” Kol 3: 8. 12-15. Ikumbukwe kwamba, walezi na walelewa wote kwa pamoja wanahitaji malezi na majiundo endelevu!