Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu malezi na makuzi ya watoto sanjari na kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu malezi na makuzi ya watoto sanjari na kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.   (Vatican Media)

WAWATA Wapongezwa Kwa Malezi na Makuzi ya Utoto Mtakatifu Nchini Tanzania

Mama Evaline Malisa Ntenga, anasema, Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu malezi na makuzi ya watoto sanjari na kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Dalmas G. Gregory, M/Kiti Halmashauri Walei Jimbo la Zanzibar anasimulia yale yaliyomgusa. Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa VIWAWA, Taifa, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka kupitia kwa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Imegota takribani miaka 12 tangu Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania alipotembelea mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 19 Januari 2012. Katika mazungumzo ya dakika kumi na tano, viongozi hawa wawili waligusia kuhusu: Majadiliano ya kidini, amani katika eneo la Maziwa Makuu, Afya, Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni katika muktadha wa kujenga na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican, tarehe 12 Februari 2024, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baadaye, Rais Samia amebahatika pia kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Katika mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika ishirini na tano, wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania; mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania, hususan katika sekta ya: elimu, afya, ustawi wa jamii pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa. Baadaye, wamejielekeza zaidi katika masuala ya kijamii nchini Tanzania; masuala ya kikanda na Kimataifa na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa katika kujikita katika kudumisha amani ulimwenguni. Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara hii ya kitaifa, alikuwa ameambatana na Mama Evaline Malisa Ntenga, ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa ni Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania. Prof. Deogratias Rutatora, Mwenyekiti Halmashauri ya walei, Taifa; Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, Taifa, VIWAWA; Dalmas Gregory, Mwenyekiti Halmashauri Walei, Jimbo Katoliki la Zanzibar pamoja na Theresia Paschas Seda, Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza WAWATA kwa malezi na makuzi kwa Utoto Mtakatifu.

Papa Francisko, Rais Samia na Waamini walei kutoka Tanzania
Papa Francisko, Rais Samia na Waamini walei kutoka Tanzania

Mama Evaline Malisa Ntenga, Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anapenda kuonesha furaha kutoka katika sakafu ya moyo wake kwa heshima waliyopewa waamini walei kuungana na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania katika ziara yake ya kikazi mjini Vatican. Pamoja na mambo mengine, Rais Samia Suluhu Hassan amekazia umuhimu wa kujenga, kuendeleza pamoja na kudumisha maridhiano ili kuendeleza misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya Tanzania. Mama Ntenga anampongeza Rais Samia kwa juhudi zake za kukuza: Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kusonga mbele; mambo yanayofumbatwa katika falsafa ya “Four R.” Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Mama Ntenga amekazia umuhimu malezi na makuzi ya watoto sanjari na kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Amewasihi waamini walei waendelee kushikamana na kutembea pamoja kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi nchini Tanzania; ujenzi ambao kimsingi unafumbatwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume. Ameipongeza Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kwa malezi na makuzi ya Utoto Mtakatifu nchini Tanzania.

Theresia Paschas Seda akisalimiana na Papa Francisko
Theresia Paschas Seda akisalimiana na Papa Francisko

Dalmas G. Gregory, M/Kiti Halmashauri Walei Jimbo la Zanzibar. Mambo niliyo jifunza katika ziara Vatican pamoja Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tukiwa wawakilishi wa Watanzania Wakatoliki ambao kwa idadi ni zaidi ya milioni kumi na tano: Rais aliambatana nasi yaani: Prof Deogratias F Rutatora M/Kiti Halmashauri walei Taifa. Everline Malisa Ntenga M/Kiti WAWATA Taifa na Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika. Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, Taifa, VIWAWA; Theresia Paschas Seda Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Tanzania pamoja na Dalmas G. Gregory M/Kiti Halmashauri ya Walei Jimbo Katoliki Zanzibar. Ili mpendeza Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kutupa fursa ya kuogozana naye kama sehemu ya ujumbe wa Tanzania kwa Baba Mtakatifu Francisko. Tumejionea mambo mengi ambayo ki uhalisia tumekuwa tukisoma kwenye vitabu na mafundisho ya Kanisa kuhusu Imani yetu, Makazi ya Baba Mtakatifu ambapo pia ni Makao makuu ya Kanisa Katoliki Ulimwenguni yalivyo. Mambo tuliojifunza na kujionea ni pamoja na; Upendo na unyenyekevu walio nao watendaji wa kwenye makazi, tume pokelewa kwa upendo mkubwa na kubadilishana mawazo na wasaidizi wa Baba Mtakatifu. Namna Kanisa lilivyojijenga katika misingi mizuri ya umoja (Cordination). Uzuri wa makazi ya Baba Mtakatifu pamoja na viunga vyake. Namna watu wanavyo safari kutoka maeneo mengi kuja kuhiji katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mapokezi kutoka kwa Baba Mtakatifu yaliyosheheni tabasamu la “kukata na shoka; na ukarimu kwa ujumbe wa Mheshimiwa Rais pamoja na sisi tuliokuwa kwenye msafara huu. Tumeonja upendo wa Watanzania wanaofanya utume wao mjini Vatican hususan Radio Vatican.

Dalma G. Gregory, M/Kiti Halmashauri Walei Zanzibar
Dalma G. Gregory, M/Kiti Halmashauri Walei Zanzibar

SHUKRANI: Tunamshukuru sana Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kutembea na waamini Walei ili kujifunza na kujionea misingi ya imani yetu, hii imeonesha ni jinsi gani Mh. Rais ni Rais wa watu wa aina zote. Shukrani kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kuridhia ombi la Mama Samia Suluhu Hassan la kuambatana nasi waamini walei. Shukrani nyingine ni kwa Mh. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. January Yusuph Makamba na watendaji wote wa Wizara ya Mambo ya Nje, shukrani hizo pia ni kwa Balozi wa Tanzania mjini Vatican pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Italia pamoja na watendaji wote Serikalini walio husika kwa namna moja au nyingine kutufikisha mjini Vatican. Naishukuru pia familia yangu na hasa “asali ya moyo wangu na ubavu wangu wa kuli” mke wangu Everline, wanangu Daniel, Mark, Elly, Rose na Rozane. Nimewakumbuka na kuwaombea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni mimi Dalmas G. Gregory, M/Kiti Halmashauri Walei Jimbo la Zanzibar.

Leonardi Mapolu, Mwenyekiti VIWAWA, Taifa
Leonardi Mapolu, Mwenyekiti VIWAWA, Taifa

Kwa upande wake, Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, Taifa, VIWAWA, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka kupitia kwa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuweza kukutana, kusalimiana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko na hivyo kuandika historia ya hija kubwa katika maisha na utume wake. Hii ni changamoto ya kuendelea kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano bora kati ya Serikali na Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania na Ulimwengu katika ujumla wake. Leonard Mapolu, anapenda kuchukua fursa hii kuwaasa vijana wenzake kujikita katika maisha ya sala sanjari na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu kila hatua ya maisha yao! Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 yataadhimishwa Jimbo kuu la Seoul nchini Korea ya Kusini, kielelezo makini cha mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa na ndoto ya umoja na mshikamano wa watu wa Mungu, ndoto ambayo vijana wa kizazi kipya ni mashuhuda wake.  Itakumbukwa kwamba, Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na Siku ya 41 ya Vijana Ulimwenguni itaadhimishwa Jimbo kuu la Roma kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 3 Agosti 2025 kwa kunogeshwa na kauli mbiu Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Baba Mtakatifu anawaalika vijana wa kizazi kipya kuhudhuria kwa wingi katika maadhimisho haya.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025: Utamaduni wa amani
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025: Utamaduni wa amani

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, VIWAWA, Taifa, anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika Vijana Wakatoliki nchini Tanzania kuanza kujipanga, ili waweze kuhudhuria maadhimisho haya kwa wingi zaidi. Alipokutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, ameonja unyenyekevu mkuu kutoka kwa Baba Mtakatifu ambaye amemwomba amkumbuke katika sala zake. Kwa hakika anasema, Leonard Mapolu kutoka Jimbo Katoliki la Shinyanga kwamba, katika ziara hii ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameonja wema na ukuu wa Mungu katika maisha yake. Ili shughuli mbalimbali ziweze kuendelea kuna haja ya kujikita katika misingi ya hali, amani, ustawi na maendeleo ya watu. Anawaalika vijana kuendelea kumtegemea Mungu kwa kusali. Anamshukuru Mungu, Rais Samia Suluhu Hassan, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Jimbo la Shinyanga, Mwajiri wake, familia pamoja na Jumuiya ndogo ndogo anakosali kwa kupata fursa hii adimu.

Waamini Walei Tanzania
19 February 2024, 15:33