Wito wa Dharura Kwa Wanawake Kulinda na Kutunza Mazingira Nyumba ya Wote
Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - Vatican.
Mama Evaline Malisa Ntenga, ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa ni Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa “WUCWO” “World Union of Catholic Women's Organisations, WUCWO” Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, Taifa, katika makala hii anapembua kwa kina na mapana juu ya wito wa dharura wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; dhamana na wajibu wa Wanawake katika utunzaji bora wa mazingira; Muhtasari wa Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” uliochapishwa tarehe 4 Oktoba 2023. Wapendwa marafiki, katika mkutano mkuu uliofanyika Mei 2023 huko Assisi pamoja na vipaumbele vingi, lilipitishwa, azimio la kufanya kazi kurekebisha changamoto ya sasa ya chakula ulimwenguni kwa kukazia uwajibikaji zaidi na kupunguza matumizi mabaya ya chakula. Kipaumbele hiki kinaoneesha kwamba Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, wanapaswa kushiriki katika wito wa haraka wa kuchukua hatua zilizojumuishwa katika Hati ya “Laudato si” kuhusiana na masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi na kukuza wongofu wa kiikolojia.Awali ya yote niyapongeze majimbo ambayo tayari yanaitikia wito huu kwa bidii na ninawasihi wasiache desturi hiyo njema ya kutunza kazi ya uumbaji. Ili kuendeleza hamasa na kuamsha ari ya wito huu mkubwa kwa majimbo yote na ulimwengu mzima, ninawaalika kutuma shughuli mliizofanya kwa mfumo wa maandishi na au picha za mnato au za kutembea (picha na video) kwenye ofisi ya WAWATA Taifa. Kumbukumbu ya kazi hizo nzuri zilizofanyika kuitikia wito wa Baba Mtakatifu Francisko wa kutunza mazingira nyumba ya wote, zitasambazwa kwenye vyombo vya mawasiliano vya "Vatican News", tovuti rasmi ya habari ya Vatican ili kuhakikisha zinawafikia wanawake wengine duniani na kuendelea kuamsha ari ya wanawake wengi kushiriki na kuwajibika zaidi katika kuheshimu na kutunza kazi ya uumbaji.
Miaka 8 imepita sasa tangu Baba Mtakatifu Mtakatifu Francisko achapishe Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Inasikitisha, kuendelea kuona uharibifu wa mazingira unazidi kuongezeka na madhara makubwa tunayashuhudia kila siku. Mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri na yanaharibu maisha ya maelfu na maelfu ya watu, hasa walio katika mazingira magumu zaidi. Athari hizi na wasiwasi wa kuona mazingira yanaendelea kuharibiwa ndiyo yaliyopelekea Baba Mtakatifu Francisko kuchapisha Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” uliochapishwa tarehe 4 Oktoba 2023, Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi na mwanzo wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Waraka huu wa Kitume umechapishwa baada ya miaka minane tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochapisha Waraka wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Kumbe, Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” unakita ujumbe wake juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi duniani, upinzani na hali ya kuchanganyikiwa, shughuli za kibinadamu, Uharibifu na hatari zake; kukua kwa dhana ya kiteknolojia, tathmini mpya ya matumizi bora ya madaraka; Udhaifu wa sera za kimataifa na umuhimu wa kusanidi upya mfumo wa pande nyingi. Mikutano ya Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi, ufanisi na kuanguka kwake; Matarajio ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP28 huko Dubai, 2023. Motisha za maisha ya kiroho: katika mwanga wa imani sanjari na kutembea kwa pamoja katika ushirika na uwajibikaji.
Tunaweza kuona wazi kwamba, azimio lililopitishwa huko Assisi, Italia, liliona mbali na kupelekea kuwa ndio mwelekeo wa Kanisa. Ni jambo lisilopingika kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi zitaendelea kuathiri maisha na familia za watu wengi kama hatua madhubuti zisipochukuliwa kwa haraka. Tunaona athari zake katika maeneo ya huduma za afya, vyanzo vya ajira, upatikanaji wa rasilimali, makazi, uhamiaji, nk." (LD 2). "Mabadiliko ya tabianchi ni moja ya changamoto kuu zinazoikabili jamii na Jumuiya ya Kimataifa. (LD 3) Ninaguswa sana na sehemu ambayo Baba Mtakatifu anasema: "Katika jaribio la kurahisisha ukweli, kuna wale ambao wataweka wajibu kwa maskini, kwa kuwa wana watoto wengi, na hata kujaribu kutatua tatizo kwa kuwanyamazisha wanawake katika nchi change zaidi duniani.” Kama kawaida, inaonekana kwamba kila kitu ni kosa la maskini. Ni ukweli kwamba asilimia kubwa ya hewa ya ukaa inazalishwa na nchi zilizoendelea kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia pamoja na shuhguli za kiuchumi ukilinganisha na nchi maskini au zinazoendelea. (LD 9) Baba Mtakatifu anatuonya kuhusu kiwango cha kutisha cha ongezeko la joto duniani linalosababisha hali mbaya ya hewa na majanga ya asili kuongezeka zaidi na zaidi. Amesema kuwa, jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto hii ya athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo inatishia binadamu wote. Nchi na jumuiya ya Kimataifa lazima sasa ziendeleze sera na mifumo ya kisheria ambayo itatoa adhabu kali kwa ukiukwaji wa kanuni za kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko hakuweza kushiriki katika Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 kuanzia tarehe Mosi Desemba hadi 3 Desemba 2023 na badala yake Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican alimwakilisha. Hii ingekuwa ni mara ya kwanza kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1995 hivyo anatutaka tuweke "shinikizo lenye manufaa", kwani kila familia inapaswa kutambua kwamba mustakabali wa watoto wao uko hatarini." (LD 58).
Aidha, Mkutano wa Amani ya Dunia uliofanyika Dubai siku za hivi karibuni uliwaleta pamoja viongozi wa dini tofauti zipatazo 30 ambao walisaini tamko la pamoja lililoelekezwa kwa wajumbe wa Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28. Katika mkutano huo, aliwataka viongozi wa dunia kuchukua hatua kulinda sayari yetu yaani dunia tunamoishi Kwa hakika hii ilikuwa fursa ya kukuza umoja kati ya imani tofauti kwa lengo moja. Wanawake Wakatoliki wanaweza kufanya nini? Wanawake Wakatoliki wanayo mengi ya kufanya katika nafasi na mazingira yao. Mabadiliko ya uhakika na ya kudumu yanaweza kupatikana tu kwa kuanza kubadili mtazamo na mawazo juu ya mazingira na umuhimu wake. Mabadiliko chanya yanaanza na mtu binafsi katika ngazi ya kaya/familia, jumuiya, kanda, Kigango, Parokia, Dekania, Jimbo, taifa na hatimaye dunia nzima. Ninawaalika wanawake wote kushiriki yafuatayo: Kuombea na kushiriki mikakati chanya ya kutengeneza na kuhuisha mazingira yetu. Katika hili, kuendelea kuombea COP28 ili iweze kufikia malengo ambayo ni muhimu katika kulinda nyumba ya wote ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia. Kutambua umuhimu wa kutunza mazingira na kuchukua mabadiliko chanya katika kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu mazingira bora kwa jamii zinawazunguka. Kuimarisha Umoja na ushirikiano na taasisi na asasi mbalimbali za kiserikali na kiraia (za kidini na siziso za kidini) zinazojikita katika uelimishaji na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya pamoja.
Kutumia vipawa na karama mbalimbali katika hali na mazingira tuliyopo kuitikia wito wa Baba Mtakatifu Francisko katika kukuza utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira ambao unawajibisha katika kutumia rasilimali asilia na utunzaji wa ujumla wa mazingira nyumba ya wote. Kuunga mkono kazi za Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani hasa mradi wa WWO kwa njia ya sala, juhudi na rasilimali katika kuwasikiliza, kuwaleta nuruni na kubadilisha maisha ya maelfu na maelfu ya wanawake na watoto ambao, ni waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi na ambao wamejikuta wameachwa peke yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo waume zao au wengine kulazimika kuhama pamoja na watoto wao/familia zao, kutokana na viashiria vinavyolenga kuhatarisha usalama wao wenyewe, uadilifu wa kibinafsi na wa watoto wao. Kushiriki kampeni kushinikiza/kusukuma serikali na mashirika ya Kimataifa kuchukua hatua madhubuti zaidi za kukomesha ongezeko la uzalishaji wa joto duniani, linalosababishwa na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote ikiwa ni pamoja na kutekeleza maazimio ya COP28. Kuwa mstari wa mbele katika kutoa na kupokea mafunzo mbalimbali kwa jamii ili kukabiliana na changamoto hizi kubwa. Ninawasihi wanawake wote kuchukua hatua binafsi na za jumla katika kuokoa mazingira nyumba yetu ya pamoja. Ili kuendelea kujifunza juu ya mipango na jitihada zinazofanywa, kusoma makala na kujifunza Ushauri mpya wa Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” tafadhali tembelea tovuti ya Vatican: Vatican website. Na tovuti ya Jukwaa la Hatua la Laudato si, https://laudatosiactionplatform.org/.
Hitimisho: Napenda kuhitimisha ujumbe huu kwa moja ya aya za sala nzuri ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameitumia kuhitimisha Waraka wake wa Laudato si'. Ninawaalika wote tusali kila siku, hasa tunapoendelea kutekeleza maazimio ya Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28. “Mungu wa upendo, tuoneshe nafasi yetu katika ulimwengu huu, Kama njia ya upendo wako kwa viumbe vyote vya dunia hii. Kwa maana hakuna hata mmoja wetu anayesahauliwa mbele yako. Wape nuru wale walio na nguvu na fedha ili waepuke dhambi ya kutojali, ili wapende kutunza yale yenye manufaa kwa wote, waendeleze wanyonge, na kutunza ulimwengu huu ambao tunaishi. Tuwe na ujasiri wa kujibu kilio cha Dunia Mama pamoja na Maskini. Ee BWANA, utushike kwa nguvu zako na nuru yako, Utusaidie kuokoa maisha ya wote, Kujiandaa kwa ajili ya maisha bora ya baadaye, Kwa ajili ya kuja kwa ufalme wako wa haki, amani, upendo na uzuri. Utukuzwe Mungu wetu! Nawatakia utume mwema katika Kristo Yesu. AMINA.