Tafuta

2023.04.06 Giovedì della Settimana Santa â   Santa Messa del Crisma

Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma ya Upendo

Papa atabariki Mafuta ya Wakatekumeni na Mafuta ya Wagonjwa pamoja kuweka wakfu Mafuta ya Krisma; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo na wanapowekwa wakfu kuwa Mapadre na Maaskofu. Haya ni mafuta yanayotumika pia kutabaruku Kanisa kwa kupata Altare na kuta za Kanisa kuonesha kwamba, Jengo hili, yaani Kanisa limetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya mambo matakatifu ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa Alhamisi kuu tarehe 28 Machi 2024 kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuweka wakfu Mafuta ya Krisma ya Wokovu. Ibada hii itaadhimshwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3:30 kwa saa za Ulaya, sawa na Saa 5:30 kwa Saa za Afrika Mashariki. Baba Mtakatifu atabariki Mafuta ya Wakatekumeni na Mafuta ya Wagonjwa pamoja kuweka wakfu Mafuta ya Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo na wanapowekwa wakfu kuwa Mapadre na Maaskofu. Haya ni mafuta yanayotumika pia kutabaruku Kanisa kwa kupata Altare na kuta za Kanisa kuonesha kwamba, Jengo hili, yaani Kanisa limetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya mambo matakatifu ya Mungu. Mama Kanisa anafundisha kwamba, Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha Mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya upendo, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Akataka pia kuwapatia amana ya upendo huu na kuendelea kubaki kati yao na kuendelea kuwashirikisha Fumbo la Pasaka, aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kielelezo cha sadaka, shukrani, kumbukumbu endelevu na uwepo wake kati yao katika alama ya Mkate na Divai!

Alhamisi Kuu: Daraja Takatifu ya Upadre
Alhamisi Kuu: Daraja Takatifu ya Upadre

Alhamisi kuu ni Siku ambayo Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu ya Upadre inayopata utimilifu wake katika Daraja ya Uaskofu. Hii ni siku ambayo Kristo Yesu aliwaweka Mitume wake, wawe wafuasi wake wa karibu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, hii ni siku ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre na kuwashukuru Mapadre kwa sadaka na majitoleo yao. Huu ni mwaliko kwa Mapadre kuishi mintarafu ya Daraja Takatifu ya Upadre, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wa Kipadre, wakitambua kwamba, kwa njia ya Daraja Takatifu ya Upadre wanashirikishwa maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mapadre wanapaswa kusimama kidete ili kuweza kuishi fadhila za maisha na utume wa Kipadre, kwa kujitahidi kuishi kama Kristo mwingine “Alter Christus” ili kwamba, waamini waweze kumtambua Kristo Yesu ndani mwao. Hii pia ni Siku ambayo Mapadre wanarudia tena ahadi pamoja na viapo vyao, jambo wanalopaswa kulifanya kutoka katika sakafu ya nyoyo zao.

Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma
Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma

Huu ni muhtasari wa mahubiri yaliyotolewa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam, tarehe 26 Machi 2024 wakati wa kubariki mafuta ya wagonjwa na wakatekumeni yaliyobarikiwa baada ya Sala ya Ekaristi Takatifu pamoja na kuweka wakfu Mafuta ya Krisma ya Wokovu mwishoni mwa Ibada ya Misa Takatifu. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi amewataka Wakristo wote kuwa macho na watu wanaogawa au kupaka watu mafuta, kwani wanawadanganya na kutaka kuwanyonya. Hii ni changamoto kwa Mapadre kuzingatia Ukuhani walioshirikishwa na Kristo Yesu. Wajipange kufundisha kufundisha mafundisho sahihi ya imani, katekesi makini na kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha na wito wao wa Kipadre, ili kweli waweze kuwa ni mfano bora wa kuigwa na waamini wao, ili hatimaye, waamini hao waweze kumfahamu, kumpenda na kumfuasa Kristo Yesu, tayari kumshuhudia kwa dhati kabisa. Baraka itolewe kwa msingi na uelewa wa mafundisho ya Kanisa Katoliki. Sakramenti za Kanisa ziadhimishwe kwa ibada na uchaji, ili kuzuia kufuru dhidi ya Sakramenti hasa ya Ekaristi Takatifu. Mapadre wasimame kidete kutoa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu pale inapostahili na kutumika kama inavyopaswa kadiri ya mafundisho ya Kanisa Katoliki. Mapadre washikamane na Kristo Yesu, kiasi kwamba, waamini waweze kumtambua Yesu ndani mwao. Alhamisi kuu ni siku ambayo pia Mapadre wanarudia ahadi, maagano na viapo vyao vya Kikuhani, changamoto ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuishi kadiri ya maagano haya, ili kweli waweze kuwa ni baraka katika Kanisa la Mungu.

Ujenzi wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo
Ujenzi wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo

Kwa upande wake, Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki Moshi, Tanzania katika Ibada ya kubariki Mafuta ya Wakatekumeni, Wagonjwa pamoja na kuweka wakfu Mafuta ya Krisma ya Wokovu, Jumanne, tarehe 26 Machi 2024 amewataka Mapadre kufanya mabadiliko chanya katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, kwa kuhakikisha kwamba, Ibada ya Misa Takatifu inaadhimishwa kwa Ibada, uchaji na imani zaidi ili kupyaisha imani, kujenga na kudumisha moyo wa sala na ibada. Mapadre wajitahidi kuhubiri kwa viwango, waelimishane, waalikane na watambue kwamba, wanaunganishwa na kushikamanishwa na Sakramenti ya Daraja Takatifu ya Upadre. Kumbe, Mapadre wanapaswa kupendana, kushikamana na kutembeleana. Mapadre waoneshe mabadiliko chanya katika kuchapa kazi kwa kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma makini kwa watu wa Mungu. Mapadre wayafahamu maeneo yao ya utume na wayahudumie kwa ari, moyo mkuu na upendo. Wawe ni waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, huku wakijitahhidi kuipyaisha ile kauli mbiu ya Mwaka wa Mapadre: Uaminifu wa Kristo, Uaminifu wa Padre. Hii iwe ni dira na mwongozo wa maisha na utume wao kama Mapadre. Wajitahidi kuinjilisha kwa njia ya ujenzi wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo.

Alhamisi Kuu
27 March 2024, 15:01