Askofu Jean Claude Rakotoarisoa Jimbo la Tsiroanomandidy Madagascar
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 9 Machi 2024 amemteuwa Monsinyo Jean Claude Rakotoarisoa wa Jimbo Katoliki la Tsiroanomandidy kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Miarinarivo, nchini Madagascar. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Jean Claude Rakotoarisoa alikuwa ni Makamu Askofu Jimbo la Tsiroanomandidy na Mkurugenzi mkuu wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS nchini Madagascar. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Jean Claude Rakotoarisoa wa Jimbo Katoliki la Miarinarivo, alizaliwa kunako tarehe 4 Oktoba 1971.
Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 29 Agosti 1999 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Kuanzia Mwaka 2010 hadi mwaka 2016 alitumwa mjini Roma kwa masomo ya juu na hatimaye, akajipatia Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa. Na kati ya Mwaka 2017 hadi 2021, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Tsiroanomandidy. Hadi kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 9 Machi 2024 kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Miarinarivo alikuwa ni Makamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Tsiroanomandidy na Mkurugenzi mkuu wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS nchini Madagascar.