2024.03.12:Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher aliadhimisha Misa katika Parokia ya  Swefieh huko Amman,nchini Jordan. 2024.03.12:Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher aliadhimisha Misa katika Parokia ya Swefieh huko Amman,nchini Jordan. 

Askofu Mkuu Gallagher:kuna waamini wengi wasio na huru wa kukiri imani yao

Katika misa huko Yordani,Askofu Mkuu Gallagher wakati wa kuadhimisha miaka 30 tangu uwepo uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Jordan aliwatia moyo wawe na ujari na daima kuwa na matumaini.Wito ambao aliutoa kwa Makanisa yote ya Mashairiki ya Kati.Kwa kufahamu kwamba katika baadhi ya nchi Wakristo hawawezi kusali kwa lugha yao,kujenga makanisa,hawana uhuru wa kushiriki katika maisha ya kisiasa na kijamii.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa na Mashirikia ya Kimataifa aliongoza ibada ya Misa Takafiu katika Parokia ya Kilatini ya Swefieh (Amman), tarehe 12 Machi 2024 katika fursa ya ziara yake iliyohusiana na maadhimisho ya miaka 30 ya Mahusiano kati ya Vatican na Yordan yaliyofanyika tarehe 11 Machi. Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu alianza na salamu kwa uchangamfu washiriki wote wa Baraza la Kawaida la Mashirika ya Nchi Takatifu waliokusanyika hapa Amman, na Patriaki wa Kilatini wa Yerusalemu,Kardinali  Pierbattista Pizzaballa, na alimshukuru kwa makaribisho yake mazuri. Alitoa salamu na baraka za Baba Mtakatifu Francisko kwa wote waliohudhuria - Kilatini, Melkite, Siria, Maronite, Armenian na Wakaldayo - mapadre, watawa na waamini, pamoja na familia na jumuiya zao, hasa wakimbizi Wakristo kutoka Palestina, Iraq na Siria.

Misa iliyoongozwa na Askofu Mkuu Gallagher huko Jordan
Misa iliyoongozwa na Askofu Mkuu Gallagher huko Jordan

Askofu Mkuu Gallagher alielezea alivyofika huko kutembelea Ufalme wa Hashemite wa Jordan kwa sababu, miaka 30 iliyopita, Papa Mtakatifu Yohane Paulo II na Mfalme Husayn bin al-Khalil waliamua kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia ili kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa heshima na urafiki ambao ulikuwa tayari upo kati ya Vatican  na Jordan. Kwa Vatican mahusiano ya kidiplomasia ni desturi ya kale na iliyoanzishwa vyema. Yanatumika kama chombo cha kuunga mkono uhuru wa Kanisa Katoliki nchini (libertas Ecclesiae) na utetezi na ukuzaji wa hadhi ya binadamu (dignitatis humanae), unaozingatia tunu za haki, ukweli, uhuru na upendo. Kanuni hizi daima zimeonesha uhusiano wetu wa kirafiki na Jordan. Katika nchi hiyo, Kanisa Katoliki lina bidii na ari, na linaweza kushiriki katika shughuli za kichungaji kwa njia ya kujitoa bure na yenye matunda, likitoa huduma muhimu sana kwa vijana.

Tusichoke kutangaza na kuishi Injili 

Kama wanavyojua, vijana wanahitaji Kanisa lililo hai sasa kuliko wakati mwingine wowote. Wanahitaji wachungaji na makatekista wanaojua jinsi ya kuleta uzuri wa imani katika Kristo Mfufuka, ambaye alikuja kutumikia, si kutumikiwa. Kwa kusititiza alisema “Tusichoke kamwe kutangaza na kuishi Injili ili kukuza utambulisho wetu wa kweli wa Kikristo, iwe ni katika parokia, katika shule za Kikatoliki - ambazo jamii ya Jordani inathamini sana - au katika Mahali Patakatifu.” Na nini maana ya kuwa Mkristo? “Ninainua macho yangu kuelekea milimani. Msaada wangu utatoka wapi?” Zaburi iliuliza ambayo ilisikika. Kwa hiyo alijikita kutazama Mlima ambao Yesu anatusaidia kuelewa utambulisho wa Mkristo. Heri za Mlimani zinaelezea njia ya kuwa ambayo, kama matokeo, inakuwa njia ya kutenda. Zinaboresha na kukamilisha maadili yaliyomo ndani ya Amri Kumi, hutupatia mwelekeo wazi wa maisha yetu.

Kugeuka maana yake uwepo wetu unapagwa upya

Heri za mlimani, hata hivyo, zinatuletea hali karibu ya kitendawili: ni wale wanaoteseka zaidi ndio wanaoitwa wenyeheri. Yesu alitangaza kwamba maskini, wenye njaa, wenye kiu, wanaoteswa, wasioheshimiwa na wapole wenyeheri: vigezo vya ulimwengu vimepinduliwa chini ili kuonesha mtazamo wa Mungu ni upi. Ndiyo, Kanuni za Heri hudai 'uongofu'. Kimsingi, neno uongofu linamaanisha kugeuka. Inamaanisha mambo ya ndani kugeuka kutoka katika mwelekeo ambao tungechukua moja kwa moja. Lakini uongofu huu unaleta mwanga kile kilicho safi, kilicho juu zaidi. Uwepo wetu unapangwa upya kwa njia ifaayo. Kupitia uongofu, tunawasilishwa na mtu mpya, mpango wa maisha unaoongoza kwa aina tofauti ya furaha. Furaha hiyo haitegemei hisia za muda mfupi tu, bali juu ya shangwe kuu ya kuwa pamoja na Kristo na katika Kristo, katika utumishi wa Ufalme wa Mungu.

Hakuna aliye mkamilifu

Heri zinatuambia kwamba Mkristo anapaswa kuwa mtu mpole asiyeona haya kulia, mwenye moyo safi na wa neema uwezao kusamehe, anayehitaji Mungu daima, anayetafuta “chakula na maji ya kweli” ya haki ambaye ni mpenda na mhamasishaji amani, na asiyeogopa mateso kwa ajili ya Injili. Sifa hizi zote zinazopaswa kuwa sifa ya mwanafunzi pia ni taswira ya Kristo. Akitazama umbali uliopo Askofu Mkuu alisema “Maili chache kutoka hapo, kwenye ukingo wa Yordani, mbingu zilifunguka na Roho wa Mungu akashuka kama njiwa juu ya Yesu, na sauti kutoka mbinguni ikasema: “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye(Mt,3:17). Kadiri tunavyotafakari juu ya Heri, ndivyo tunavyotambua zaidi utambulisho wa Mpendwa wa Baba, Mwokozi, Yesu Kristo. Wapendwa kaka na dada, mnashuhudia ukweli kwamba kuwa wadogo wengi kuliko walio wengi sio kuwa Mkristo mdogo. Kinyume kabisa! Ikiwa sisi ni wachache kwa idadi, ina maana kwamba tunahitaji kuonesha kwa uhalisi zaidi na mara kwa mara kwamba hatuogopi kuishi Injili. Hakuna hata mmoja wetu ambaye ni mkamilifu au safi. Hata hivyo, sisi ni kundi la watu ambao, licha ya dhambi, tuko tayari kutoa maisha yetu kwa ajili ya Kristo, kulingana na wito tuliopokea.

Kuwa jasiri na matumaini

Muwe jasiri! Na daima kuwa na matumaini! Alitoa mwaliko huo kwa Makanisa yote ya  Mashariki ya Kati. Wanafahamu kwamba katika baadhi ya nchi Wakristo hawawezi kuomba kwa lugha yao wenyewe, katika nchi nyingine hawawezi kujenga makanisa, katika nchi nyingine hawana uhuru wa kushiriki katika maisha ya kisiasa na kijamii, katika nyingine wanapata mateso ya kweli na ya jeuri. Licha ya hayo, Yesu anatufariji akisema “Furahini na kushangilia, kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni” (Mt 5:12a). Ni lazima tuwe na mshikamano na mateso yao. Tuendelee kufanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya utii wao huru kwa Kristo na kuwaombea.” Kwa njia hiyo Askofu Mkuu Gallghaer  aliweza kukuhakikishia kwamba Papa Francisko ana wasiwasi wa pekee kwa Mashariki ya Kati nzima. Anafuatilia kwa umakini mkubwa kile kinachotokea Israel na Palestina na, kama wanavyojua, anawasiliana mara kwa mara na jumuiya ya Kikatoliki huko Gaza.

Kufurahi kwa utii na uamini wa ushirika na Roma

Askofu Mkuu Gallagher aidha alisema kuwa tarehe 13 Machi 2024 ilikuwa ni tarehe ya kumbukumbu yake ya miaka 11 tangu kuchaguliwa kwake kuwa Papa, kwa hiyo aliwaliwakaribisha kuungana naye katika kumkumbuka kwa namna ya pekee wakati wa Misa hii Takatifu,  ili Mungu amweke katika afya njema, amlinde na kumpa nguvu. Bwana Yesu aliweka Petro na waandamizi wake kama mwamba ambao angejenga Kanisa lake juu yake. Kupitia ukuu huu, Papa ndiye kanuni inayoonekana ya umoja wa Kikristo. Tufurahi, kwa utii wa uaminifu, katika ushirika huu uliopo kati ya Roma na Wakatoliki wote ulioenea duniani kote. Aina nyingi za nidhamu za kikanisa, ibada za kiliturujia, na kitaalimungu na kiroho zilizorithiwa kwa Makanisa mahalia, zilizounganishwa katika jitihada za pamoja, zinaonesha kwa uzuri zaidi ukatoliki wa Kanisa lisilogawanyika”(LG 23).

Mungu aipake nafsi yote mafuta ya huruma yake

Askofu Mkuu zaidi aliendelea katika mahubiri yake kuwa “Leo, zaidi ya hapo awali, tunahisi umoja huu mkuu katika sala inayotuleta sote pamoja, Kanisa Katoliki zima lililotawanyika ulimwenguni kote: sala ya amani! Baba Mtakatifu Francisko, pamoja na Kanisa zima, anaomba kwamba katika Israeli na Palestina, na katika eneo lote silaha zikome kurusha risasi, watu wasiuawe tena, mateka waachiliwe, waliojeruhiwa wasaidiwe na msaada huo itawafikia wale wanaohitaji. Miaka kumi iliyopita, hapo Amman, Baba Mtakatifu Francisko alisema: “Tumwombe Roho Mtakatifu aitayarishe mioyo yetu kukutana na ndugu zetu, ili tuondokane na tofauti zetu zinazojikita katika fikra za kisiasa, lugha, utamaduni na dini. Tumuombe aipake nafsi yetu yote mafuta ya huruma yake, yenye kuponya majeraha yatokanayo na makosa, kutoelewana na mabishano. Na tumuombe neema ya kutupeleka mbele, kwa unyenyekevu na upole, katika njia inayodai lakini yenye utajiri wa kutafuta amani.”

Mahubiri ya Askofu Mkuu Gallagher
14 March 2024, 16:14