Askofu Vincent Cosmas Mwagala Jimbo Katoliki la Mafinga: Utume
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 22 Desemba 2023 aliunda Jimbo jipya la Mafinga, nchini Tanzania kwa kulimega Jimbo Katoliki la Iringa na Jimbo kuu la Mbeya na kwamba, Jimbo Katoliki la Mafinga litakuwa chini ya Jimbo kuu la Mbeya. Makao makuu ya Jimbo Katoliki la Mafinga “Mafingensis" yatakuwa mjini Mafinga na Kanisa kuu la Jimbo ni Kanisa la Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, Mafinga. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu akamteuwa Mheshimiwa sana Padre Vincent Cosmas Mwagala kutoka Jimbo Katoliki la Iringa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Mafinga na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 19 Machi 2024, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria. Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora ndiye aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu ya kumweka wakfu na hatimaye kumsimika Askofu Vincent Cosmas Mwagala, Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Mafinga. Kauli mbiu yake ya Kiaskofu ni “Thesaurum istum in vasis fictilibus: Yaani “Hazina katika vyombo vya udongo.” 2Kor 4:7. Yafuatayo ni mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora katika Ibada ya kumweka wakfu na hatimaye kumsimika Askofu Vincent Cosmas Mwagala, Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Mafinga, Tanzania. Tumsifu Yesu Kristo! Tunamsifu, kwani ni yeye aliyetukutanisha hapa tunapoyashuhudia mambo makuu mawili: Kwanza ikiwa ni kuanzishwa kwa Jimbo jipya la Mafinga na pili ikiwa ni kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Monsinyo Vincent Cosmas Mwagala aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo la Mafinga. Hayo yote, tunayafanya katika siku hii ya furaha ambamo Kanisa zima linaadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mme wa Bikira Maria na Mlinzi wa Kanisa la Ulimwengu. Mtu anayeheshimika kama Mwenye haki, aliyemweka Mungu kuwa kiini cha maisha yake na hivyo kuitikia na kutimiza mapenzi ya Mungu kwa utii.
Nianze kwa kuwatakia heri ya Sherehe, wale wanaopata baraka ya kulichukua jina hili la Yosefu zikiwemo pia taasisi mbali mbali zenye kumchukua Mtakatifu Yosefu kama msimamizi wao tukiwaombea wote ili Mtakatifu huyu awalinde na kuwaelekeza kwa Bwana na Mkombozi wetu Yesu Kristo siku zote za maisha yao, akiwemo pia ndugu yetu huyu tutakayemweka wakfu na hivyo kumfanya awe mlinzi na Mchungaji mkuu wa Kanisa Mahalia la Mafinga tukimuombea kuiga Mfano wa Mtakatifu Yosefu katika kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Ndugu zangu, baraka za siku hii, zitufanye tuwe watu wa shukrani kwa mema mengi aliyotutendea Mwenyezi Mungu na hasa hilo litakalosemwa kwenye sala ya mwisho baada ya Komunio, tunapomshukuru kwa kutulisha, tukimwomba azidi kutulinda na kuyasimamia yote aliyotujalia. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atupe neema yake itakayotuwezesha kujitoa na kujiaminisha kwake siku zote za maisha yetu. Na kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu, na kabla yake, Baba yetu wa imani Ibrahimu, tunaalikwa leo tujiaminishe kwa Mungu tukiisikia sauti yake na maelekezo yake. Mtakatifu Yosefu ambaye bila woga aliyafuata maagizo ya Bwana alipomwambia kupitia kwa Malaika kuwa: “usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu,” hakusita wala kuogopa na akafanya kama Malaika alivyokuwa amemwagiza. Amemlinda na kumtunza Yesu Mkombozi wetu. Ndugu zangu wana Mafinga na sisi sote tulio hapa, tunaalikwa leo tujiweke na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu tukiamini kuwa ni yeye atakayelijenga Jimbo la Mafinga na kumwongoza Askofu Vincent na wana Mafinga katika kulikuza na kulifanikisha Jimbo hili ilimradi tu tujiweke mbele yake na kuwa tayari kuongozwa naye katika kuyatimiza mapenzi yake na si mapenzi yetu. Baba Vincent Mwagala aliyechagua kuli-mbiu ya “Tunayo hazina katika vyombo vya udongo” pamoja naye anatukumbusha ukweli kwamba tuna wajibu wa kulilinda Kanisa la Mungu ambalo si Kanisa letu, kuifanya si kazi yetu bali kazi ya Mungu katika Kristo anayetutuma na tunayemtumikia na kuwatumikia watu. Mtume wa Mataifa, Paulo ameliweka vizuri hili anaposema wazi kuwa “Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.”
Wana Mafinga na Kanisa lote la Tanzania, tutakuwa kwenye hatari kama tutashindwa kukiri kuwa mweza yote ni Mungu na ndiye mwanzilishi na anayeielekeza historia yetu kwenye mafanikio na furaha ya kudumu. Na ndiye mwenye Kanisa na na lolote linalofanyika humo likiwa ni lake. Endeleeni kuamini katika Mungu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Ni yeye pekee anayetupenda kama tunavyotegemea na kuamini kuwa ndiye pekee anayeweza kukidhi haja zetu na kuyafanya maisha yetu yawe salama. Lakini ndugu zangu tusikae tu na kubweteka!!! Lazima tushirikiane naye. Tuyakumbuke maneno ya Mtakatifu Augustino aliyesema kuwa, Mungu aliyekuumba bila wewe, hawezi kukukomboa bila wewe... Lazima tushirikiane naye katika yote tunayotaka na atakayotaka yafanyike. Ni katika muktadha huo napenda niwaalike nyote tuwashukuru wale wote waliosukumwa na neema ya Mungu wakachangia kwa namna moja au nyingine kuleta imani, kuisambaza na kuikuza, tukayashangilia na kuyafurahia matunda yake tulipomshukuru Mwenyezi Mungu katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 125 ya uinjilishaji Jimboni Iringa, iliyotukutanisha huko Kihesa, mwaka 2023. Hili la kuanzishwa kwa Jimbo jipya la Mafinga ni hakika matokeo ya kazi hiyo ya uinjilishaji inayopaswa kuendelezwa tukisukumwa na mahitahi ya kichungaji na hata kijamii ya wakati huu. Tunawashukuru Wamisionari wote walioifanya kazi hii wakiweka msingi wa yote yanayofanyika na tunayoendeleza. Asante sana Baba Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa unayewawakilisha watangulizi wako Maaskofu kwa kazi mliyofanya mkisaidiwa na wachungaji Mapadri, wawekwa Wakfu na hata waamini wote walioshirikiana nanyi.
Tumshukuru sasa Baba Askofu mteule, Vincent Mwagala aliyeitika wito na kuwa tayari kuliongoza Jimbo la Mafinga akiwa ni Askofu wa kwanza. Kwa mfano wa Mtakatifu Yosefu tunayemkumbuka leo, tunakuombea uifanye kazi hii kwa uaminifu, na kwa maombezi yake ujaliwe nguvu na hekima ya kulitumikia Kanisa la Mafinga na kokote kule utakakotumwa au utakakohitajika. Nawaalikeni wana-Mafinga kumpokea kwa furaha na shukrani. Tumheshimu na kumstahi kama Wakili na Mjumbe wa Kristo miongoni mwetu; kama mhudumu wa matakatifu ya Mungu, aliyeteuliwa na Bwana mwenyewe kudumisha na kuendeleza kazi yake ya kufundisha, kuwatakatifuza na kuwachunga kondoo wake, na hivyo kulilinda Kanisa lake kwa uaminifu na bila kuchoka. Nawe ndugu yetu tutakayekuweka wakfu leo, kwa kuwekwa mikono na kupata utimilifu wa Sakramenti ya Daraja, unaenda kufanya kazi ya Bwana wetu Yesu Kristu aliye Nabii, kuhani na kiongozi atakaye watumikia watu kama Kristu ambaye hakuja kutumikiwa bali kutumikia, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi. Mk. 10:45. Kanisa linakualika uwapende wote uliokabidhiwa hasa Mapadre na Mashemasi walio wenzi wako, wawekwa wakfu na waamini wote ambao yapaswa kuwahimiza washirikiane nawe katika kazi za kitume na usikatae kuwasikiliza kwa wema, ikiwa ni pamoja na kuwatazama hata wale ambao hawajajiunga na zizi moja la Kristu. Ni kuwa tayari kwenda kokote na kupeleka ukombozi wa Kristu kila unakohitajika. Na mwisho unaalikwa kulitunza, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kundi zima unalokabidhiwa kwa jina la Baba, la Mwana na la Roho Mtakatifu anayelitia uzima Kanisa la Kristu na kuponya udhaifu wetu kwa nguvu yake mwenyewe.
Wapendwa katika Kristo, ili kufanikisha utume wake, Mpendwa wetu huyu anahitaji sana ushirikiano wenu na sala zenu, vikitanguliwa na upendo wenu kwake na kwa Kanisa la Mafinga na la Ulimwenguni mzima. Mwisho, Baba Askofu mteule na ndugu waamini wote wa Mafinga, napenda kuwaalika tuwe na nia moja na moyo mmoja wa kuwa tayari kutumikia si katika furaha tu bali hata katika mateso ili mradi yote tuwe tunayafanya kwa ajili ya utukufu wa Mungu, kama anavyotukumbusha Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Wakorintho wa kwanza (1Kor. 10:31). Tuwe tayari kuupokea na kuuchukua Msalaba pamoja na Kristo katika utumishi wetu. Yeye aliyetuita na kutupa nafasi hii ya kushiriki katika utume wake kama Waamini kwa kubatizwa na Wachungaji kwa Sakramenti ya daraja, naamini atatupatia na nguvu za Roho wake atayetusaidia kuzifanya kazi zinazokuja huko usoni. Yote tunayaweza katika yeye anayetupa nguvu, kama anavyosema Mtume Paulo anapowaandikia Wafilipi. (Fil. 4:13). Kwenu nyote wana-Mafinga, kwa maombezi ya Mama Maria Konsolata, Mungu awabariki na kuwalinda, awape neema ya kutembea mkimwelekea na kuyafanya yote kama atakavyo yeye ili muweze kuzaa matunda anayotarajia kutoka kwenu na mwisho wa yote mpate furaha ya kubaki naye milele na milele. Amina.
Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa ndiye aliyewaongoza watu wa Mungu kusali Masifu ya kwanza ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 18 Machi 2024. Katika Ibada hii ya Masifu ya Jioni, Askofu mteule Vincent Cosmas Mwagala alikabidhiwa funguo za Kanisa la Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, Mafinga, akakiri Imani ya Kanisa Katoliki na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Naye Askofu Ngalalekumtwa katika mahubiri yake yaliyojikita katika wasifu wa Mtakatifu Yosefu, amemwomba, Askofu Vincent Cosmas Mwagala awe kweli ni mlezi wa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Mafinga, Mtetezi na Mlinzi wa imani kama alivyokuwa Mtakatifu Yosefu. Awe na msimamo, ari na uadilifu, kama Mchungaji mkuu katika kulea, kutetea na kulinda imani. Awe mstari wa mbele kulitunza Kanisa la Kristo Yesu: Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume. Atekeleze yote kwa hekima, upendo na uvumilivu wa kichungaji. Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Mafinga “Mafingensis” lina jumla ya Parokia 17 zitakazokuwa zinahudumiwa na Mapadre wa Jimbo 30, Mapadre Watawa 11. Lina watawa wa kiume ni 5 na watawa wa kike ni 136. Waseminari walioko Seminari kuu ni 52, lakini Jimbo lina utajiri mkubwa wa Makatekista wapatao 350. Jimbo Katoliki la Mafinga linaundwa na Parokia za: Mafinga, Sadani, Mdabulo, Mgololo, Kibao, Ikwega, Nyakipambo, Nyololo, Itengule, Usokami, Mapanda, Ibwanzi, Igowole, Nadibira, Ujewa, Chosi pamoja na parokia ya Mbarali.