Tafuta

Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania. WAWATA. Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania. WAWATA.  (Vatican Media)

Mama Evaline Malisa Ntenga: Maadhimisho Siku ya Wanawake Duniani 2024

Tunao Ujumbe kutoka kwa Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Ulimwenguni. Wanawake Wapandao Mbegu za Amani na Kuchochea Makutano: Wanawake wanao wajibu mkubwa katika malezi na makuzi ya watoto wao; utunzaji bora wa mazingira na wajenzi wa amani duniani.

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, Dar es Salaam, Tanzania.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna wanawake wengi wasiofahamika, lakini wamekuwa mstari wa mbele kuleta mageuzi katika familia na jamii zao kwa njia ya nguvu ya ushuhuda. Mama Kanisa anawahitaji wanawake kama hawa kwani Kanisa lenyewe kimsingi ni “Mama na Mwalimu, Ni Dada na Mchumba, mwaliko kwa Mama Kanisa kuendelea kufanya mang’amuzi, likiwa sikivu kwa Roho Mtakatifu, aminifu na lenye kudumisha ushirika, ili kutambua njia muafaka ili hatimaye kutambua na kuthamini nafasi ya wanawake miongoni mwa watu wa Mungu. Mintarafu utume wa wanawake katika Kanisa, Baba Mtakatifu amekazia zaidi mtindo wa maisha na majiundo. Katika ulimwengu huu ambao umesheheni vita, ghasia, chuki na hasira, kuna haja ya watu wa Mungu kujisikia kuwa wanapendwa na huu ndio mchango maalum kutoka kwa wanawake, wanaofahamu kuunganisha upendo unaosimikwa katika huruma. Kimsingi mwanamke kutokana na uwezo wake wa kipekee wa huruma, uangavu na tabia yake tangu asili ya kutunza anafahamu kwa njia kuu kuwa kwa jamii inayomzunguka: akili na moyo unaopenda na kuunganisha, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa upendo kwani mahali ambapo hakuna upendo, hapo mwanadamu anahangaika kujitafuta. Naye Monsinyo Juan Antonio Cruz Serrano, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Jumuiya ya Nchi za Amerika, OAS kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2024 anasema, kuna umuhimu wa kuwatambua na kuwaheshimu wanawake waliojisadaka kwa kuonesha ushupavu katika kutetea utu, heshima na haki msingi za wanawake duniani. Wanawake wanapaswa kushirikishwa kwenye vikao vya maamuzi ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Kuna wanawake shupavu ambao wameweza kujenga matumaini pasi na kukata wala kujikatia tamaa, kwa ajili ya kutetea haki ambazo hazikuwa zimetambulikana. Kumbe, kwa sasa Vatican inakazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika ujenzi wa: haki, usawa na udugu wa kibinadamu.

Wanawake wapandao mbegu za amani na kuchochea makutano
Wanawake wapandao mbegu za amani na kuchochea makutano

Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania ana haya ya kusema: Wapendwa Wanawake Wenzangu, Tunapoadhimisha Siku ya Wanawake Duniani (IWD) chini ya kaulimbiu "Kuhamasisha Ujumuishaji" sambamba na kaulimbiu ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO) "Wanawake Wapandao Mbegu za Amani na Kuchochea Makutano," tunakumbushwa juu ya wajibu msingi ambao wanawake wanafanya katika kujenga dunia yenye kukumbatia na kufurahia kuwawezesha wengine kujikomboa kutokana na changamoto za kila siku za mwanamke wa kawaida hasa yule aliyesukumizwa pembezoni. Ujumbe huu unachambua jinsi tunavyoweza kutumia kaulimbiu hizi kwa ustawi wa familia zetu na mazingira yetu, kujenga utamaduni unaojali zaidi Ujumuishaji kwa amani ya dunia nzima. Jukumu letu kama wanawake Wakristo ni kuwekeza kwenye mazingira jumuishi na kuwezesha mazungumzo na mijadala ya kimataifa katika kutatua changamoto za wanawake katika ulimwengu mamboleo ikiwa ni pamoja na nyanyaso za kijinsia, biashara haramu ya binadamu, wakimbizi, baa la njaa na nyingine nyingi. Kwa kuushi upendo, kuwa na moyo wa Huruma na msamaha kwetu binafsi na kwa wengine, na kujenga mazingira yanayolenga kutetea usawa katika imani yetu, tunaweza kuwafikia wengi waliokwisha kukata tamaa na kupoteza tumaini. Kaulimbiu ya "Kuhamasisha Ujumuishaji" inatualika kuwekeza katika desturi njema ya kuwafikiria wengine na kujenga mazingira ambayo yataruhusu kila mwanamke, bila kujali asili au hali yake, kupata nafasi ya kusikilizwa na kushirikishwa hivyo kujisikia kuwa ni wa thamani. Kwa kufanya hivyo, siyo tu kwamba  tutafurahia mafanikio ya wanawake wenzetu tu, bali pia tutakuwa tumeweka msingi wa ujumuihwaji na ushirikishwaji ambapo watoto wetu wanaweza kufanikiwa katika jamii inayothamini utu na kuwajumuisha watu wote.

Wekeza katika mazingira jumuishi kwa wanawake: Ongeza kasi ya maendeleo
Wekeza katika mazingira jumuishi kwa wanawake: Ongeza kasi ya maendeleo

Katika kuadhimisha siku hii muhimu, kaulimbiu ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani WUCWO inasema, "Wanawake Wapandao Mbegu za Amani na Kukuza Makutano.” Ujumbe uliobebwa na kaulimbiu hii unasisitiza jukumu letu kama walezi na walinzi /watetezi wa uhai. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa siku ya Wanawake Duniani kwa 2024 anasema “Wanawake Katika Kanisa: Waumbaji wa Ubinadamu.” Wanawake tuna wajibu mkubwa katika malezi na majiundo kamili ya watoto wetu. Tunaalikwa kupanda mbegu za amani ndani ya familia na katika jamii kwa kukuza majadiliano, uelewa, na huruma na ili kufanikiwa lazima kuanza na ‘mimi’. Matendo ya kila mmoja ikiwa yatatanguliza upendo kwa kila kilichoumbwa na Mungu, ni ushuhuda kamili wa Ukristo wetu na yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika jitihada za kumkomboa mwanamke na kudumisha haki na amani. Wito wa kutunza mazingira nyumba ya wote ni wa muhimu na wa msingi. Mabadiliko ya tabianchi yatokanayo na uharibifu wa mazingira vinatishia maisha kwenye sayari yetu, na hivyo tunayo dhamana ya kulinda na kuhifadhi mazingira kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kuchukua hatua za kupunguza athari zetu kwa mazingira na kutetea uhai zinapaswa kuwa endelevu kwani wanaoathirika na madhara yatokanayo na uharibifu wa sayari yetu ni masikini na wale waliosukumizwa pembezoni.

Wanawake pandeni mbegu ya haki, amani na ustawi
Wanawake pandeni mbegu ya haki, amani na ustawi

Kuwekeza kwenye usawa wa kijinsia, kujenga amani, na mikakati endelevu ya kutunza mazingira nyumba ya wote si juhudi zinazojitegemea bali zinazotegemeana katika kufikia ndoto ya kuifanya Dunia kuwa mahali bora zaidi pa kuishi kwa kila kiumbe. Kwa kukuza Ujumuishaji, tunajenga mazingira ambapo amani inaweza kukua na kuchanua na hivyo kuhakikisha mustakabali endelevu kwa vizazi vijavyo. Tunaalikwa kujisadaka bila ya kujibakiza pamoja na kuhimiza ujumuishaji katika familia, jumuiya, na taifa lote la Mungu, kupanda mbegu za amani kama namna ya kuitikia wito wa utakatifu wa maisha. Pamoja, tufanye kazi kwa bidii katika kuijenga dunia ambayo kila mwanamke, kila familia, na kila kiumbe hai kinaweza kustawi. Katika Siku ya Wanawake Duniani na ziku zote, tujitahidi kuwekeza katika ujumuishaji, na kupanda mbegu ya amani. "Wekeza katika mazingira jumuishi kwa wanawake: Ongeza kasi ya maendeleo."

Siku ya Wanawake Duniani
08 March 2024, 16:17