Mons.Balestrero,Geneva:Maendeleo ya kweli ya binadamu yana tabia ya kimaadili!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika taarifa yake Askofu Mkuu Ettore Balestrero, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika kwa Umoja wa Mataifa na Mashirika Mengine ya Kimataifa huko Geneva Uswiss katika Kikao cha 55 cha Kawaida cha Baraza la Haki za Binadamu juu ya ripoti ya Kamishna Mkuu juu ya mabadiliko ya tabianchi tarehe 13 Machi 2024 alisema kuwa “ Katika mwaka 2023, zaidi ya watu milioni 333 walikabiliwa na viwango vikali vya uhaba wa chakula, na inakadiriwa kuwa idadi hii itaongezeka hadi karibu milioni 600 ifikapo 2030. Mabadiliko ya tabianchi ni sababu kuu ya kuongezeka kwa njaa kwa sasa, isiyo na kifani. Ujumbe wa Vatican una hakika kwamba kushikilia haki zinazohusiana za chakula na mazingira safi na yenye afya kunapaswa kuwa msingi wa sera za kiuchumi na hali ya hewa. Kama ilivyobainishwa katika ripoti ya Kamishna Mkuu, “tuna uwezo wa kulisha ulimwengu.” Vatican inaamini kabisa kwamba kulaumu maskini au viwango vya juu vya kuzaliwa kwa mabadiliko ya tabianchi na uhaba wa chakula ni kupotosha, uongo, na haikubaliki. Watoto ni rasilimali, sio shida, wanaboresha maisha, sio kuyapunguza.
Uzalishaji wa hewa chafuzi ni wa nchi tajiri
Uzalishaji wa hewa chafuzi kwa kila mtu wa nchi tajiri ni wa juu zaidi kuliko ule wa nchi masikini. Ni ukweli kwamba hawa wa mwisho, ambao ni karibu nusu ya idadi ya watu duniani, wanawajibika kwa karibu 10% ya uzalishaji wa sumu. Hata hivyo, athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi huathiri vibaya watu maskini na kuzidisha matatizo yaliyopo ya njaa na utapiamlo. Papa Francisko amependekeza mara kwa mara kuanzishwa kwa mfuko wa kimataifa wa kumaliza njaa, kwa kutumia rasilimali nyingi zinazotengwa kwa sasa kwa silaha na migogoro. Hatua madhubuti za kibinadamu ni muhimu kushughulikia mabadiliko ya hali ya tabianchi kwani kimsingi husababishwa na shughuli za wanadamu. Hatua za kupunguza ambazo zinashughulikia udhalimu mkubwa zinapaswa kupitishwa, pamoja na mifumo ya usalama wa kijamii ambayo inashughulikia hatari na athari za tabianchi.
Maendeleo ya kweli ya binadamu yana tabia ya kimaadili
"Uharibifu wa mazingira ya mwanadamu ni mbaya sana, sio tu kwa sababu Mungu ametukabidhi ulimwengu sisi wanaume na wanawake, lakini kwa sababu maisha ya mwanadamu yenyewe ni zawadi ambayo inapaswa kulindwa dhidi ya aina mbalimbali za udhalilishaji. […]. Maendeleo ya kweli ya binadamu yana tabia ya kimaadili.” Inaonyesha heshima kamili kwa mwanadamu, lakini lazima pia ihangaikie ulimwengu unaotuzunguka na ‘kutilia maanani asili ya kila kiumbe na uhusiano wake wa pande zote katika mfumo uliopangwa.’