Tafuta

Kardinali  Sean Patrick O'Malley Kardinali Sean Patrick O'Malley 

Kard.O’Malley:Tunataka watoto wawe salama!

Kufuatia na Mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko katika Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto,Kardinali Seán O’Malley,Rais wa Tume hiyo akizungumza na vyombo vya habari vya Vatican,alisema kuwa:"imani ni muhimu ili Kanisa lifanikiwe katika uinjilishaji."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika kipindi cha miaka kumi tangu kuanzishwa kwa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto wadogo(PCPM) na Baba Mtakatifu Francisko, imezidi kuongezeka kwa kiasi kikubwa, kutoka kikundi kidogo cha watu wa kujitolea na wafanyakazi hadi kikundi cha wanaume na wanawake wenye sifa za juu waliojitolea kulinda Watoto katika Kanisa. Tumebarikiwa sana na kujitolea kwa ajabu kwa wajumbe wa Tume. Haya ni maelezo ya Rais wa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto (PCPM) Kardinali Seán O'Malley akizungumza na waandishi wa Vyombo vya habari vya Radio Vatican/Vatican News, katika mahojiano kufuatia na Mkutano kati ya  Tume na Baba Mtakatifu siku ya Alhamisi tarehe 7 Machi 2024. Katika mahojiaono hayo Kardinali alisisitiza juu ya thamani ya walei wa Tume, hasa wanawake, pamoja na michango muhimu ya wahanga na wazazi wao.

Tume imefanya mengi

Akipitia kwa ujumla juu ya shughuli za Tume hiyo (PCPM)katika muongo mmoja uliopita, Kardinali O’Malley aliakisi mikutano iliyoandaliwa na Tume kati ya Papa Francisko na wahanga wa nyanyaso; mapendekezo kuhusu uwajibikaji wa maaskofu uliosababisha kutunga sheria ikiwa ni pamoja na Barua ya Motu Proprio Come una madre amorevole yaani Kama Mama Mwenye Upendo, na Vos estis lux mundi yaani Ninyi ni Mwanga wa Dunia; na kilele cha Mkutano wa marais wa Mabaraza ya Maaskofu duniani kuhusu Nyanyaso katika Kanisa. Kardinali pia alidokeza mpango unaoendelea wa "Kumbukumbu," unaolenga kutoa msaada kwa nchi zisizo na rasilimali watu na nyenzo muhimu kwa ajili ya ulinzi mzuri. Mpango huo unatoa fedha kwa ajili ya kulinda kazi na kusaidia kuhakikisha uwepo wa wafanyakazi kwa ajili ya uchunguzi na mafunzo ya wafanyakazi wa kichungaji na pia kwa ajili ya uchungaji wa waathirika. Kumbukumbu na mipango kama hiyo inalenga kujenga uhusiano na Maaskofu na Mabaraza ya Maaskofu, ili Tume ionekane kama mshirika badala ya kuwa adui katika kukuza “Utamaduni wa Ulinzi ndani ya Kanisa.” Rais wa PCPM, kwa maana hiyo aliongeza kusema kuwa: "Kwa hivyo nadhani Tume hii  imetimiza mengi." 

Tunataka watoto wawe salama

Kardinali O’Malley akiendelea na maelezo yake alibainisha kuwa sehemu kubwa ya mwelekeo wa Tume kwa sasa ni kusini mwa dunia, akitumaini kuhakikisha kwamba Makanisa mahalia yana rasilimali na mafunzo muhimu ili kukabiliana na unyanyasaji. "Hii inahusisha kuendeleza sera na miongozo ili kuhakikisha jibu ambalo ni thabiti katika Kanisa lote, na linaloheshimu mahitaji na haki za waathirika, watuhumiwa, jamii, Kanisa, na serikali ya kiraia." Kardinali pia alisisitiza "umuhimu wa kampeni kubwa ya elimu kila mahali kuhusu masuala ya ulinzi na kujikita katika kuzuia nyanyaso. "Tunataka watoto wawe salama," Kardinali O'Malley alisema. "Tunataka watoto na wazazi wawe na imani kwamba watoto wao wanapokuwa katika shule ya Kikatoliki au katika Parokia za Kikatoliki, wako salama." Akijibu wazo kwamba kulinda ni kuvuruga utume wa Kanisa, Rais wa PCPM alisisitiza kuwa: “Hatutaweza kufanikiwa katika utume wetu wa kuinjilisha ikiwa hatuna imani na watu, ikiwa hatuwezi kuwathibitishia kwamba wao ni muhimu kwetu na usalama wa watoto wao ni kipaumbele kwetu.”

Jukumu la Tume

Alipoulizwa kuhusu ukosoaji wa Tume hiyo, Kardinali O’Malley alitambua kwamba baadhi ya watu hawana subira na kasi ndogo ya majibu ya Kanisa kwa mgogoro wa unyanyasaji ndani ya Kanisa. Kuhusiana hasa na Tume hiyo ya PCPM, Kardinali alisema matarajio yasiyo ya kweli yanayotokana na kutoelewa uwezo wa Tume "yametuweka katika njia panda." Na zaidi alibainisha kuwa "Tume haikuanzishwa kushughulikia kesi fulani: Huo haukuwa uwezo wetu kamwe." Badala yake, Tume ilipewa jukumu la kutoa mapendekezo na mengine kuhusu jinsi gani ya kuboresha mwitikio wa Kanisa kwa unyanyasaji wa kijinsia. Hata hivyo, Tume imefanya kazi ya kuwasaidia waathirika kwa kuwasaidia kuwasiliana na wale wanaoweza kuwasaidia. Hakika, kusikiliza sauti ya waathiriwa ni sehemu muhimu sana ya  utume wetu," Kardinali O'Malley alisema.

Kusaidia Makanisa mahalia

Wakati huo huo, sehemu muhimu ya mamlaka ya PCPM ni kusaidia Makanisa mahalia katika kukabiliana na waathirika, na pia kuwasaidia katika kuzuia na mafunzo. Katibu wa PCPM Padre Andrew Small, OMI, alibainisha “mkataba wa maelewano” mwingi uliotiwa saini kati ya Tume na Mabaraza ya Maaskofu wa kitaifa hadi sasa. Haya yanalenga kukuza mwitikio thabiti wa “Kanisa Moja”, kuhakikisha kwamba rasilimali zipo katika Makanisa mahalia ili kuwasindikiza waathirika. "Hilo ni jambo gumu kwa yale [Makanisa] ambayo ni maskini wa rasilimali na hayana wataalam wote" wanaohitajika "kukaribisha" waathiriwa. "Tunasaidia kurekebisha hilo," Fr. Small alisema, na kuongeza, "Hiyo haitatokea mara moja, lakini tunapiga hatua kubwa."

Haki ya kuambiwa ukweli

Kardinali O'Malley pia alibainisha juhudi za kutoa uwazi zaidi katika Kanisa kuhusiana na kushughulikia unyanyasaji, akizungumzia mapendekezo ya awali ya kufanya mabadiliko kwa kile kinachoitwa "siri ya kipapa" pamoja na jitihada zinazoendelea za kutoa ufafanuzi wakati maaskofu wanaondolewa kutoka katika ofisi. "Kwa hivyo, ndiyo, uwazi ni muhimu sana," Kardinali alisisitiza, akiongeza kuwa, "Uaminifu hauwezi kurejeshwa isipokuwa tuwe na uwazi katika ngazi zote za Kanisa." Padre  Small alikubaliana na hilo, akisema kwamba imedhihirika kuwa “wanachotaka watu zaidi ya kitu kingine chochote ni kuambiwa ukweli.” "Nadhani watu wana haki ya kuambiwa ukweli. Na wakati mwingine, kama viongozi, tunaogopa kuamini watu na ukweli, lakini hatuwezi kuwa hivyo. Ikiwa hatuwaamini watu kiukweli, hawatatuamini. Na nadhani hiyo ni aina ya mipaka karibu na uwazi, uaminifu na uwazi ambao tunahitaji kufanyia kazi zaidi."

Sauti ya waathirika

Hatimaye katika mahojiano hayo Kardinali O’Malley alisisitiza kuwa: “Sehemu muhimu zaidi ya utume wetu ni kujaribu kuwa sauti kwa waathirika na kufanya kazi kwa bidii ili jambo hili liwe kipaumbele kila mahali katika Kanisa. Kwa kurudia alisema: " Uinjilishaji utakuwa kazi isiyowezekana ikiwa hatuwezi kurejesha imani ya watu kwetu kwa kuwathibitishia watu kwamba watoto wao ndio kipaumbele chetu na usalama wao ndio lengo letu kuu."

Mkuu wa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto
09 March 2024, 17:02