Rais wa Montenegro Akutana na Papa Francisko Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 7 Machi 2024 amekutana na kuzungumza na Rais Jakov Milatović, wa Montenegro, ambaye baadaye, amebahatika kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mgeni wake, katika mazungumzo yao ya faragha, wameridhishwa na uhusiano mwema uliopo kati ya nchi hizi mbili na baadaye wakajikita zaidi katika mada muhimu kwa kuonesha mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Montenegro.
Wamegusia pia uhusiano kati ya Kanisa na Serikali. Baadaye viongozi hawa wawili wamejielekeza zaidi katika hali halisi ambayo Montenegro na baadhi ya nchi za Balcan ziko kwenye mchakato wa kujiunga na Umoja wa Ulaya; vita kati ya Israeli na Palestina bila kusahau vita kati ya Urusi na Ukraine.