Tafuta

Ni mlinzi na mwombezi wa Ireland na Mama Kanisa anafanya kumbukumbu yake kila mwaka ifikapo tarehe 17 Machi. Hii ndiyo siku alipofariki dunia yaani tarehe 17 Machi 461. Ni mlinzi na mwombezi wa Ireland na Mama Kanisa anafanya kumbukumbu yake kila mwaka ifikapo tarehe 17 Machi. Hii ndiyo siku alipofariki dunia yaani tarehe 17 Machi 461.  (Vatican Media)

Sikukuu ya Mtakatifu Patrick: Ujumbe Kwa Watu wa Mungu

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya kumbukizi ya Mtakatifu Patrick, tarehe 17 Machi 2024 Askofu mkuu Eamon Martin wa Jimbo kuu la Armagh, nchini Ireland anasema, Mtakatifu Patrick anaweza kuhesabiwa kuwa ni Mlinzi na Mwombezi wa wakimbizi na wahamiaji. Kuna wananchi wengi wa Ireland ambao wamehamia ugenini, hii ni changamoto kwa Ireland kuonesha moyo wa huruma na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mtakatifu Patrick ni mmisionari aliyesadaka maisha yake kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini Ireland. Ni mlinzi na mwombezi wa Ireland na Mama Kanisa anafanya kumbukumbu yake kila mwaka ifikapo tarehe 17 Machi. Hii ndiyo siku alipofariki dunia yaani tarehe 17 Machi 461. Historia inaonesha kwamba, akiwa na umri wa miaka 16 alitekwa nyara na Maharamia na kupelekwa utumwani nchini Ireland. Baada ya kufanikiwa kuwatoroka watesi wake na kupata malezi na majiundo ya Kipadre, kunako mwaka 418 alipewa Daraja ya Ushemasi na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu mwaka 432. Papa Celestine wa kwanza akamtuma rasmi kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini Ireland sanjari na kuziimarisha Jumuiya ndogondogo za Kikristo. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya kumbukizi ya Mtakatifu Patrick, tarehe 17 Machi 2024 Askofu mkuu Eamon Martin wa Jimbo kuu la Armagh, nchini Ireland anasema, Mtakatifu Patrick anaweza kuhesabiwa kuwa ni Mlinzi na Mwombezi wa wakimbizi na wahamiaji. Kuna wananchi wengi wa Ireland ambao wamehamia ugenini, hii ni changamoto kwa Ireland kuonesha moyo wa huruma na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji katika ulimwengu mamboleo.

Mtakatifu Patrick, Mlinzi na Mwombezi wa Ireland
Mtakatifu Patrick, Mlinzi na Mwombezi wa Ireland

Ili kufikia hatua hii, kuna haja kwa Ireland kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi kwani leo hii kuna vijana wengi kutoka Ireland wameihama nchi yao ili kutafuta: ustawi na maendeleo zaidi. Inakadiriwa kwamba, kunako mwaka 2023 watu 64, 000 walihama kutoka nchini Ireland, lakini mara nyingi wanarejea nchini Ireland wakiwa wamebeba tunu msingi za maisha kutoka ughaibuni, uzoefu na mang’amuzi mapya ya maisha, huku maisha yao yakiwa yameboreka maradufu na kwamba, wazazi na walezi wanaendelea kuwaombea watoto wao walioko ughaibuni, wakitambua kwamba, Bwana ndiye mlinzi wao; atawalinda na mabaya yote, atazilinda nafsi zao na kwamba, Bwana atawalinda watokapo na waingiapo, tangu sasa na hata milele. Rej. Zab 121. Leo hii kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, kuna baadhi yao wamelazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita, dhuluma pamoja na hali ngumu ya kiuchumi. Lakini kuna baadhi ya watu wanajikuta wakiwa wametumbukizwa huko kutokana na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake.

Maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Patrick nchini Ireland
Maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Patrick nchini Ireland

Ni katika muktadha huu, Mtakatifu Patrick anaweza kuhesababiwa kuwa ni Mlinzi na Mwombezi wa Wakimbizi na Wahamiaji. Ni Mtakatifu aliyeonja adha ya kutekwa nyara na kuuzwa utumwani; hali ya kuwa utumwani pasi na wazazi au walezi; ni mtu aliyefanyishwa kazi za suluba; akawatoroka watesi wake na kuwa mhamiaji na mwanafunzi katika nchi ya ugenini. Mtakatifu Patrick alivumilia magumu mengi katika maisha na utume wake; chuki, uhasama pamoja na kejeli. Lakini baada ya kuwatoroka watesi wake alirejea tena miongoni mwa watu wa Mungu nchini Ireland na kukaribishwa kwa moyo wa upendo na ukarimu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea kwa kulinda na kudumisha: utu wao. Kuwalinda katika haki zao msingi; Kuwaendeleza ili waweze kujifunza tamaduni, lugha na hatimaye kupata fursa za ajira na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha!

Ujumbe kwa watu wa Mungu, Sikukuu ya Mtakatifu Patrick
Ujumbe kwa watu wa Mungu, Sikukuu ya Mtakatifu Patrick

Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Ireland kujenga na kudumisha upendo na ukarimu kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, ili kweli Ireland iweze kuwa ni nchi inayosimikwa katika ukarimu ili kutoa hifadhi kwa watu wanaobisha hodi wakiomba msaada na hifadhi. Ireland inapaswa kuwa ni nchi yenye mfano bora wa kuigwa kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotamani kuishi nchini humo, wakiwa wanapatiwa huduma msingi. Mtakatifu Patrick ni mfano bora wa huruma na upendo wa Mungu, aliyejisadaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; huruma na upendo wa Mungu, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Ireland kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi, wahamiaji na maskini. Ni changamoto kwa watu wa Mungu Nchini Ireland kuganga na kuponya chuki ya chuki, uhasama na ubaguzi wa rangi; daima wajitahidi kumwona Kristo Yesu anayeteseka kati ya wafungwa, wakimbizi na wahamiaji.

Mt. Patrick 2024
16 March 2024, 13:56